Real Madrid yatishia kuigomea FIFA

Muktasari:

  • Fifa imefanya maboresho makubwa kwenye michuano hiyo sasa itashirikisha timu 32 na itafanyika Marekani mwishoni mwa msimu ujao.

MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imepanga kugomea mwaliko wa kwenda kucheza kwenye michuano mipya ya Klabu Bingwa Dunia.

Fifa imefanya maboresho makubwa kwenye michuano hiyo sasa itashirikisha timu 32 na itafanyika Marekani mwishoni mwa msimu ujao.

Lakini, kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti alisema timu yake inaweza kugomea mwaliko wa kucheza kwenye michuano hiyo.

Ancelotti alisema: “Fifa inasahau kwamba timu hazitacheza kwenye michuano mipya ya Klabu Bingwa Dunia.

“Mechi moja ya Real Madrid thamani yake ni Pauni 20 milioni na Fifa inataka kutupa kiasi hicho cha pesa kwa michuano yote.

“Tutakataa huo mwaliko.”

Fifa imeripotiwa ilipofanya mazungumzo ya majadiliano ya zawadi ya pesa na klabu, Real Madrid haikufuatwa kutoa maoni.

Michuano hiyo mipya ya Klabu Bingwa Dunia imepangwa kufanyika kuanzia juni 15 hadi Julai 13, 2025.

Timu za kutoka mabara sita zitashiriki michuano hiyo, ambapo kwa Ulaya, timu zilizofuzu kwa michuano hiyo ni Chelsea, Manchester City, Real Madrid, Bayern Munich na Juventus.

Lakini, michuano hiyo tayari imeshakabiliana na pinzamini kutoka kwa chama cha wanasoka wa kulipwa Fifpro kutokana na hali ya wachezaji kutokana na kuchezeshwa mechi nyingi na kuhatarisha afya zao.

Bosi wa LaLiga, Javier Tebas alisema ana wasiwasi Fifa inataka kulazimisha ligi za ndani kupunguza timu kutoka 20 na kuwa 18.

Tebas alisema: “Kama hatutachukua hatua hii tasnia itakuwa kwenye hatari kubwa sana. Fifa wao wanaona suluhu ni kuja na michuano mipya.

“Lakini, hili likitokea kwa upande wetu, ili kuweza kushiriki kwenye michuano hiyo, basi itabidi tuondoe timu mbili kwenye La Liga. Na hilo likitokea basi utakuwa umeua ajira za wachezaji 70. Tunahitaji kumaliza hili tatizo kabla ya kuanzisha michuano mipya.”

Bosi wa PFA, Maheta Molango alisema mastaa wa Ligi Kuu England wapo tayari kuitisha mgomo kuliko kucheza michuano hiyo. Na sasa kinachoelezwa ni kwamba klabu pamoja na umoja wa vyama vya wachezaji wanafikiria kufungua kesi ya kupinga michuano hiyo ya Klabu Bingwa Dunia, wakitaka ifutwe.