Ramos yupo pazuri kuinunua Sevilla
Muktasari:
- Gwiji huyo wa soka wa Hispania na Real Madrid, 39, hana klabu kwa sasa tangu alipoondoka katika kikosi cha Monterrey ya huko Mexico mwezi uliopita.
SEVILLE, HISPANIA: SERGIO Ramos ameongeza dau kubwa la fedha kwa lengo la kuinunua klabu yake ya zamani, Sevilla.
Gwiji huyo wa soka wa Hispania na Real Madrid, 39, hana klabu kwa sasa tangu alipoondoka katika kikosi cha Monterrey ya huko Mexico mwezi uliopita.
Ramos alikanusha wazo la kustaafu baada ya kuwa mchezaji huru, lakini inaonekana mipango ya maisha baada ya soka inaanza kuwekwa. Na iwapo atakuwa mbia mkubwa katika klabu aliyokulia, hatakosa shughuli za kujaza muda wake.
Kwa mujibu wa The Athletic, Ramos anaongoza jaribio la kununua Sevilla kwa dau linalokaribia Pauni 350 milioni.
Beki huyo mwenye hasira uwanjani, ambaye utajiri wake unakadiriwa kufikia Pauni 58 milioni, hatakuwa mwekezaji mkubwa zaidi katika muungano huo, ambao pia unajumuisha kampuni ya uwekezaji ya Marekani Five Eleven Capital.
Hata hivyo, Ramos ndiye sura ya umma ya pendekezo hilo, ambalo sasa linachukua hatua madhubuti kuelekea kukamilika. Inaripotiwa kuwa Ramos na washirika wake wamewasilisha barua ya nia, jambo linalofungua kipindi cha miezi mitatu cha upekee kwao kukamilisha dili hilo.
Hata hivyo, bado kuna uchunguzi mkubwa wa kufanyika kabla ya mshindi huyo wa Kombe la Dunia kukamilisha dili hilo.
Waombaji wa ununuzi wameanzisha ukaguzi wa nje wa kifedha ili kupata picha halisi ya hali ya fedha za Sevilla, ambazo zimeendelea kudorora katika miaka ya hivi karibuni. Klabu ilipata hasara ya Pauni 71 milioni na kukopa Pauni 94 milioni msimu wa 2023–24, huku deni lao la jumla likikadiriwa kufikia karibu Pauni 156 milioni. Kundi jingine la wawekezaji lilijiondoa kwenye mchakato wa ununuzi mwaka jana baada ya kufanya tathmini zao wenyewe.
Ramos, ambaye alikutana na wanahisa mbalimbali wa Sevilla pamoja na timu yake ya kisheria mapema mwezi huu, alikulia katika eneo hilo na alipata nafasi yake ya kwanza ya kikosi cha wakubwa na klabu hiyo mwaka 2004. Baadaye alitumia miaka 16 na Real Madrid na misimu miwili Paris Saint-Germain kabla ya kurejea Sevilla kwa awamu ya pili. Katika taaluma yake iliyong’ara, Ramos amecheza zaidi ya mechi 1,000 na kufunga mabao 150.