Jitihada za watu binafsi zinavyoibeba Senegal
Muktasari:
- Wanasema hakuna nchi ambayo imewahi kutwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na shule za watoto za soka.
NDIYO. Yapo mafanikio yanayotokana na kufurukuta, lakini hutokea kwa nadra sana. Mafanikio yanatokana na mikakati thabiti na uwekezaji mzuri. Ukiyaweka hayo, basi hata usipopata mafanikio uliyokusudia, utakuwa umefikia kiwango fulani kizuri cha kukupa ujasiri wa kufanya vizuri baadaye.
Wanasema hakuna nchi ambayo imewahi kutwaa Kombe la Dunia bila ya kuwa na shule za watoto za soka.
Hispania ilisumbuka sana kutafuta ubingwa wa dunia pamoja na kuwa na klabu zilizokuwa zikitetemesha dunia kama Real Madrid na Barcelona, lakini ni kizazi cha kina Andre Iniesta na Sergio Ramos kilichokulia kwenye shule za soka ndicho kilichoipa ubingwa wa kwanza mwaka 2010.
Kwa hiyo uwekezaji katika soka ni lazima uanzie kwenye soka la watoto na si vijana kama wengi wanavyotaka iwe kwa kuwa hadi kufikia ujana mchezaji anakuwa ameshajijengea misingi mibovu kama hakupata mafunzo sahihi akiwa utotoni. Na ni vigumu mno kwa kijana kama huyo kumbadili aanze kufuata misingi sahihi.
Mapema mwezi huu Senegal ilikamilisha juhudi zake za kutafuta umwamba wa soka Afrika ilipotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kuishinda timu ngumu ya Morocco katika fainali.
Hii ni mara ya pili kwa Senegal kutwaa taji hilo baada ya kulitwaa mwaka 2021 kwa kuishinda Misri, timu nyingine ngumu Afrika.
Unaweza kujiuliza ni vipi Senegal, moja ya nchi maskini Afrika iliyojaa vijana wazururaji imepata mafanikio hayo? Ni vipi inaweza kuwekeza kwa vijana hadi wafikie kuwa tishio katika soka la Afrika?
Shirikisho la Soka la Senegal linapata wapi rasilimali za kuwekeza katika soka kama nchi yenyewe haina utajiri huo? Au ni fedha za miradi ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa)?
La hasha! Ni jitihada mchanganyiko za watu binafsi kuwekeza katika soka kwa kuanzisha shule za soka za watoto ambazo sasa ndizo zinazozalisha sehemu kubwa ya wachezaji wanaounda timu za taifa za kuanzia vijana hadi hiyo iliyotwaa taji la AFCON Morocco.
Senegal imetwaa ubingwa wa soka la ufukweni Afrika mara saba kati ya mashindano tisa yaliyochezwa hadi sasa. Simba hao wa Teranga walitwaa taji la Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwaka 2023, wakati timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 walitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2023.
Pia timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 ilitwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2022 na 2023.
Haikuwa ajabu kwa nchi hiyo kutawala tuzo za ubora Afrika mwaka 2022, wakati Sadio Mane alipotangazwa kwa Mwanasoka Bora wa Mwaka, huku Pape Ousmane Sakho akatwaa tuzo ya Goli Bora, huku PapeMatar Sarr akatangazwa kuwa Mwanasoka Bora Kijana na kocha wao Aliou Cisse kuwa Kocha Bora na Senegal ikitangazwa kuwa Timu Bora ya Mwaka.
Kwa mwaka huo, Senegal ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na wachezaji wengi (wachezaji 51) katika ligi tano kubwa Ulaya.
Mafanikio yote hayo hayakupatikana kwa bahati au kufurukuta, bali jitihada binafsi tofauti, zikiwemo za shule za soka kama Generation Foot, iliyomzalisha Mane, Ismaila SarrSaliou Ciss, Irissa Gueye, Diambars Academy iliyoanzishwa na Saer Seck kwa kushirikiana na kocha wa zamani wa Crystal Palace na kiungo wa Arsenal, Patrick Vieira.
Shule hizo mbili zilizalisha wachezaji nane kati ya 27 walioitwa na Cisse kwa ajili ya fainali za mwaka 2021’
Shule nyingine ni Etoille de Lusitana ambayo si maarufu sana lakini inatoa mchango mkubwa kwa kuandaa wachezaji wanaosajiliwa na klabu za ligi ya juu nchini Senegal na sasa ikom shule nyingine iliyoanzishwa na mchezaji wa zamani wa Senegal na Liverpool, Salif Diao.
Mbali na kusaidia vijana kisoka, lengo la Diao kuanzisha shule hiyo ya mpira wa miguu ni kutaka wafanye vitu viwili pamoja, yaani wapate mafunzo ya mpira wa miguu na elimu itakayowawezesha kuendesha maisha iwapo hawatapata mafanikio uwanjani.
Diao mwenyewe hakusoma na aliachana na shule ya soka Metz akiwa na umri wa miaka 13 ili kwenda kutafuta nafasi kwa shida hadi akaibukia Liverpool. Na sasa hataki vijana wapitie shida hizo ndio maana mchezaji anayesajiliwa na shule yake inayoendeshwa na Salif Diao Foundation, ni lazima awe na uthibitisho anahudhuria masomo shuleni. Kila siku wanapofika mazoezini, husali na baadaye kukaguliwa na kocha au ofisa elimu kabla ya kuanza mazoezi.
Imekuwa rahisi kwa shule za soka za Senegal kupata wanafunzi kutokana na mapenzi waliyonayo watoto na vijana kwa mchezo huo. Kwa mujibu wa Moor Sport, fukwe za nchi hiyo hutawaliwa na vijana wengi wanaosakata soka hadi giza linapoingia.
Kwa hiyo haiwezi kuwa ajabu kwa nchi hiyo kutwaa taji la soka la ufukweni mara saba kati ya tisa.
Ukichunguza shuoe hizo utaona zimeanzishwa na ama wadau wa soka ama wachezaji wa zamani walio na uhusiano mkubwa na wachezaji wenzao wa zamani wa barani Ulaya au wenye uwezo wa kutengeneza mahusiano mazuri na klabu kubwa za Ulaya.
Hayo huwezesha shule hizo za soka kupata misaada ya vifaa na fedha kwa ajili ya kujiendesha.
Kwa hiyo, kunapokosekana jitida au kunapokuwepo na jitihada rasmi za mamlaka zinazosimamia mpira wa miguu, watu binafsi wanaweza kuongeza nguvu kama hizo za kuanzisha shule za soka za watoto na kuchangia kuzalisha wachezaji ambao baadaye watalibeba taifa.
Hatuhitaji miujiza ili kupata mafanikio Afrika na duniani bali jitihadaza pamoja kati ya mamlaka za soka na watu wengine kama ambavyo Senegal wamefanya.