Rais Napoli ajitosa dili la Darwin Nunez

Muktasari:
- Nunez alijiunga na Liverpool kwa ada ya uhamisho ya rekodi ya timu hiyo ya Pauni 85 milioni miaka mitatu iliyopita, lakini inaonekana yupo tayari kuondoka baada ya kocha Arne Slot kutompa nafasi ya kutosha.
NAPLES, ITALIA: RAIS wa Napoli, Aurelio De Laurentiis, anaripotiwa kuamua kuvaa gwanda mwenyewe na kuingia katika mazungumzo ya usajili wa straika wa Liverpool, Darwin Nunez ili kumsajili katika dirisha hili.
Nunez alijiunga na Liverpool kwa ada ya uhamisho ya rekodi ya timu hiyo ya Pauni 85 milioni miaka mitatu iliyopita, lakini inaonekana yupo tayari kuondoka baada ya kocha Arne Slot kutompa nafasi ya kutosha.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alifunga mabao matano na kutoa pasi tatu za mabao katika Ligi Kuu England msimu uliopita, lakini alianza mechi nane pekee.
Inaonekana ataondoka Anfield katika dirisha hili, huku Napoli, Atletico Madrid na Al-Hilal zote zikionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay.
Kikosi cha Antonio Conte kinataka kuimarisha safu ya ushambuliaji kwa lengo la kupunguza utegemezi kwa Romelu Lukaku na kupigania taji la pili mfululizo la Serie A pamoja na kufika hatua za juu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kwa mujibu wa tovuti ya Corriere dello Sport, De Laurentiis sasa ameanza kushiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo kwa lengo la kusukuma mbele dili hilo.
Ingawa Nunez anaripotiwa kuwa tayari kujiunga na Napoli, mazungumzo yamesimama katika wiki za hivi karibuni.
Rais huyo wa Napoli ameamua kuchukua usukani, akizungumza moja kwa moja na wakala Fali Ramadani, ambaye anaratibu dili hilo.
Hadi sasa, mabingwa hao wa Serie A hawajakubaliana ada ya uhamisho na Liverpool, huku Liverpool ikisemekana inahitaji Euro 60 milioni.
Hata hivyo, Napoli haiko tayari kutoa zaidi ya Euro 43 milioni, kiasi ambacho ni chini ya nusu ya kile Liverpool ilicholipa kwenda Benfica mwaka 2022.
Iwapo dili hilo litakwama, Lorenzo Lucca wa Udinese ndiye mpango mbadala wa Napoli.
Ikiwa Nunez atakamilisha uhamisho wake kwenda Napoli, ataungana na mastaa kadhaa waliowahi kucheza Ligi Kuu England.
Kiungo wa zamani wa Manchester United, Scott McTominay, alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa Serie A Mei mwaka huu na anacheza pamoja na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Scotland na aliyewahi kuwa Chelsea, Billy Gilmour.
Kevin De Bruyne pia alikamilisha uhamisho wa kujiunga na timu hiyo.