PSG rasmi kwa Pogba, wachezaji walia

MANCHESTER, ENGLAND. RASMI sasa wawakilishi wa Paris Saint-Germain wameripotiwa kuingia kwenye mazungumzo na wawakilishi wa Paul Pogba ili kuangalia uwezekano wa kukamilisha dili lake katika dirisha hili.

Hata hivyo, taarifa kutoka The Sun zimefichua kwamba kundi kubwa la wachezaji wa Manchester United likiongozwa na Marcus Rashford limekuwa kwenye kazi ya ziada ya kumuomba kiungo huyo asiondoke.

Pogba ambaye amebakisha miezi 12 kwenye mkataba wake wa sasa, mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kusalia kwenye viunga vya Old Trafford yamekwama.

Hadi sasa PSG imeshasajili wachezaji watano katika dirisha hili ambao ni golikipa wa Italia, Gianluigi Donnarumma, Sergio Ramos, Achraf Hakimi, Georginio Wijnaldum na Danilo Pereira na wanatazamia kumsajili Pogba kwa Pauni 43 milioni kama usajili wao wa sita.

Man United imekuwa ikihofia kumpoteza bure Pogba ambaye ilitumia Pauni 89 milioni kumnunua katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2016 kwa sababu mkataba wake unamalizika mwakani.

Kiungo huyu aliyeonyesha kiwango bora kwenye michuano ya Euro kwa sasa anakula bata huko Florida kabla ya kurejea England kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Pogba mwenyewe alipoulizwa kuhusiana na tetesi hizi mwezi uliopita alisema: “Bado nina mwaka mmoja kwenye mkataba wangu, kila mtu analifahamu hilo na hakuna mazungumzo yoyote ya kuurefusha, hivyo itoshe kusema bado nipo Manchester.”

Wachezaji wa Man United wameonekana kuwa kwenye hofu kubwa juu ya taarifa ya mwamba huyo kuondoka na katika kuzuia suala hilo baadhi yao wamehusika kwenye kumshawishi na kumuomba asichukue uamuzi huo.

Chanzo cha kuaminika kutoka Man United kiliiambia tovuti ya The Sun kwamba: “Rashford na wachezaji wengine wamekuwa wakifanya kila kitu ili kuhakikisha Pogba anaendelea kusalia kwenye timu. Wanaamini kwamba timu itakuwa imepoteza mchezaji muhimu na mwenye kipaji, vilevile kiongozi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.”

Inasemekana wiki hii Pogba alikataa ofa ya Pauni 50 milioni kutoka kwa Man United ikiwa ni ishara moja wapo kwamba fundi huyo huenda asiwe sehemu ya kikosi cha mashetani wekundu kwa msimu ujao.

Man United imekuwa ikihofia sana kumpoteza Pogba kwa sababu hakuna mchezaji anayeweza kusimama badala yake ana akaonyesha kiwango kama chake.

Ilijaribu kumsajili Donny van de Beek kutoka Ajax kwa Pauni 40 milioni katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi ili akawe mbadala wa kiungo huyo iwapo ataondoka lakini bado hajaonyesha kama anaweza kuvaa viatu vya fundi huyo wa Ufaransa.

Vilevile kumekuwa na orodha ndefu ya viungo kutoka timu mbali mbali barani Ulaya wanaotajwa kwamba huenda wakasajiliwa na wababe hao ili kuziba nafasi ya Pogba.

Man United inahusishwa kuwa kwenye mpango wa kumsajili kiungo mmoja kati ya staa Declan Rice wa West Ham, Saul Niguez wa Atletico Madrid au kiungo wa Rennes na Ufaransa, Eduardo Camavinga.

Katika siku chache zijazo Man United inatarajiwa kuthibitisha rasmi usajili wa beki wa kati kutoka Real Madrid, Raphael Varane anayetarajiwa kuwa atasaini mkataba wa miaka minne utakaokuwa na kipengele cha kuurefusha kwa mwaka mmoja zaidi.

Dili hilo linatarajiwa kukamilika katika siku chache zijazo baada ya Man United yenyewe kuthibitisha kwamba wameshafanya makubaliano ya awali na Real Madrid.