Presha imerudi EPL
LONDON, ENGLAND. BAADA ya kupumzika kwa muda kupisha mechi za michuano za kimataifa za kalenda ya FIFA, hatimaye presha imerudi barani Ulaya ambapo leo kwa pale England timu tano kati ya sita bora zitashuka dimbani. Huku vigogo wengi wakionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mechi zao kutokana na rekodi na historia zilizopo.
Mashabiki wa Manchester United ndio wanaonekana kuwa na wakati mgumu zaidi kwani kwa sasa timu yao imekuwa ikipitia changamoto lukuki ndani na nje ya uwanja na mpinzani wanayekwenda kukutana naye ameanza vizuri ligi zaidi yao.
Man United ambayo itakuwa nyumbani kuikaribisha Brighton kwenye mechi itakayoanza saa 11:00 jioni inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa mwisho kabla ya mapumziko ya michuano ya kimataifa dhidi ya Arsenal.
Vilevile itakuwa inakosa huduma za mastaa wao Jadon Sancho na Antony ambao wanasumbulia na matatizo ya nje ya uwanja ambapo kwa upande wa Sancho ametibuana na kocha wake wakati Antony amesimamishwa ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili za unyanyasaji wa kijinsi kwa mchumba wake wa zamani.
Brighton ya Roberto de Zerbi inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na alama tisa na kushika nafasi ya sita huku ikiwa imetoka kuifunga Newcastle United mabao 3-1.
Man United ina kazi ya kujitetea kwa sababu ndani ya mechi nne za ligi ilizocheza imeshinda mbili na imepoteza mbili huku ikiwa nafasi ya 11.
Hata hivyo, kumekuwa na rekodi nzuri zaidi kwenye mechi ambazo Man United imecheza na Brighton ndani ya Septemba kwani kwenye michezo mitatu, Man United imeshinda miwili na kutoa sare moja.
Liverpool ambayo imeshinda mechi tatu kati ya nne ilizocheza hadi sasa ikiwa inashika nafasi ya tatu ndio itakuwa ya kwanza kufungua dimba kwa kuumana na Wolves yenye alama tatu pekee ikiwa imeshinda mechi moja kati ya nne ilizocheza na kushika nafasi ya 15. Mechi hii itapigwa saa 8:30 mchana.
Vijana kutoka London, Tottenham nao watakuwa nyumbani kuvaana na Sheffield United saa 11:00 jioni, Spurs inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na matumaini makubwa baada ya kufanya vizuri kwenye mechi zake nne za kwanza ambazo imekusanya alama 10 ikishinda mechi tatu na sare moja na hadi sasa ikiwa inashika nafasi ya pili.
Wakati huo wapinzani wake Sheffield imeambulia pointi moja tu kwenye mechi nne ilizocheza hadi sasa na inashikilia nafasi ya 17.
Vinara wa ligi hii Manchester City ambao ndio timu pekee iliyoshinda mechi zote nne za mwanzo wakikusanya alama 12, wenyewe watakuwa na kibarua dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano ya Uefa Europa Conference League, West Ham ambao hawajapoteza mechi yoyote kati ya nne walizocheza huku wakiwa wanashika nafasi ya nne kwa pointi zao 10, mechi hii itapigwa saa 11:00 jioni pia.
Vibonde Luton Town ambao wamepanda daraja msimu huu hadi sasa wakiwa hawana pointi hata moja watakuwa ugenini kuvaana na Fulham ambayo imekusanya pointi 4 kwenye mechi tatu.
Aston Villa iliyo nafasi ya 10 itaikaribisha Crystal Palace ambayo imeanza na moto licha ya kuondokewa na mshambuliaji wao tegemeo Wilfred Zaha. Palace wapo nafasi ya saba wakiwa na alama saba ilizokusanya kwenye mechi nne. Mechi hizi zote zitachezwa saa 11:00 jioni.
Newcastle United ambayo ilifanya vizuri msimu uliopita ikifanikiwa kufuzu hadi michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu huu imeanza vibaya ikiwa imepata alama tatu pekee kwenye mechi nne.
Watakuwa nyumbani kuikaribisha Brentford ambayo inashika nafasi ya sita ikiwa na alama sita baada ya mechi nne.
Inaonekana kuwa ni kipimo kigumu pia kwa Newcastle ambayo hadi sasa inashika nafasi ya 14 na mchezo wao wa mwisho walichapika na Brighton. Mchezo huu utaanza saa 1:30 usiku.