Polisi Thailand avaa jezi ya Liverpool amkamate muhalifu

Muktasari:
- Jambo hilo lilidaiwa kama tukio la kulipa kisasi baada ya Liverpool kuchapwa 2-1 na Newcastle United kwenye fainali ya Kombe la Ligi iliyofanyika uwanjani Wembeley wiki iliyopita.
KRABI,THAILAND: WANASEMA tembea uyaone. Ndiyo hivyo, polisi wa upepelezi Thailand walivaa jezi za Liverpool kwa ajili ya tukio la kumkamata shabiki wa Newcastle United aliyedaiwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Jambo hilo lilidaiwa kama tukio la kulipa kisasi baada ya Liverpool kuchapwa 2-1 na Newcastle United kwenye fainali ya Kombe la Ligi iliyofanyika uwanjani Wembeley wiki iliyopita.
Polisi watatu waliokuwa wametinga jezi za Liverpool walikwenda kwenye kioski cha mtu huyo anayedaiwa ni shabiki wa Newcastle, ambaye anauzwa bagia za nyama kila moja Pauni 200, lakini kumbe ndani yake kuna kitu kingine, vidonge 200 vya dawa aina ya methamphetamine.
Alitiwa nguvuni na kisha kupiga picha na polisi hao huko mjini Krabi, Thailand, ambayo ilionekana kama mashabiki wa Liverpool wakiwa na shabiki wa Newcastle.
Mtuhumiwa, Aphichat Nayaw, 33, anakabiliwa na adhabu ya kifo au kifungo cha muda mrefu jela endapo kama atakutwa na hatia na wingi wa dawa alizokamatwa nazo.
Liverpool ni klabu ya Ligi Kuu England yenye mashabiki wengi Thailand na inapokuwa na mechi, mashabiki kibao wamekuwa wakijazana kwenye baa kutazama mechi za timu hiyo, ikiwamo maofisa wa polisi.
Mkuu wa polisi wa wilaya, Preecha Saingthong, ambaye aliongoza tukio hilo alisema: “Mimi na polisi wenzangu ni mashabiki wa Liverpool. Nilitazama ile mechi ya fainali ya Kombe la Ligi, nisingeweza kukosa. Hatukushinda, lakini sikuhuzunika kwa sababu Liverpool tumeshashinda mara 10 na Newcastle ilikuwa haijashinda kombe kwa miaka 70.
““Na mwisho wa msimu, nina uhakika tutashangilia Liverpool itakapobeba ligi. Tuna klabu ya mashabiki wa Liverpool hapa, tunajiandaa na kusherehekea, hakuna shida hapo.”