Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pengo la Dorgu litakavyozibwa Man United

DORGU Pict

MANCHESTER, ENGLAND: MICHAEL Carrick amekumbana na changamoto ya kwanza kubwa kama kocha wa muda wa Manchester United baada ya kuthibitishwa kuwa Patrick Dorgu atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 10 kutokana na jeraha la paja.

Dorgu amekuwa mchezaji bora zaidi tangu Carrick achukue nafasi ya Ruben Amorim, akifunga mabao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Manchester City na ushindi wa 3-2 ugenini dhidi ya Arsenal. Akiwa amebadilishwa kutoka nafasi ya beki wa kushoto wa pembeni (left wing-back) katika mfumo wa 3-4-2-1 wa Amorim hadi winga wa kushoto katika mfumo wa 4-2-3-1 wa Carrick, amekuwa kwenye kiwango bora.

Gary Neville amefafanua mabadiliko hayo kwenye Sky Sports akisema: “Patrick Dorgu alionekana wa kawaida sana alipokuwa kama wing-back chini ya Ruben Amorim. Lakini, sasa akiwa winga, anaonekana kama mchezaji tofauti kabisa.”

Manchester United sasa itakosa huduma yake kwa takribani wiki 10 baada ya jitihada zake dhidi ya Arsenal kusababisha jeraha hilo kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Denmark. Inatarajiwa atakosa mechi nane za Ligi Kuu England, huku akitarajiwa kurejea dhidi ya Leeds United, Aprili 11.

Carrick aliwachezesha wachezaji wale wale 11 wa mwanzo katika mechi zake mbili za kwanza, lakini sasa atalazimika kubadilika. Swali ni: atafanya nini? Haya hapa machaguo aliyonayo Carrick katika kuziba pengo la Dorgu.

DO 01

1. Mason Mount; Carrick hana nafasi ya kumtumia Jadon Sancho au Marcus Rashford, ambao wote wako kwa mkopo Aston Villa na Barcelona mtawalia, wala Alejandro Garnacho ambaye aliuzwa Chelsea kwa Pauni 40 milioni kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kutofautiana na kocha Amorim.

Hivyo, chaguo la wazi zaidi kuchukua nafasi ya Dorgu ni Mason Mount. Kiungo huyo wa Man United amekuwa akicheza upande wa kushoto kama mmoja wa viungo wa kushambulia chini ya Amorim na yuko vizuri kukata kuelekea ndani kwa mguu wake wa kulia ulio imara zaidi.

Mount aliishia kukaa tu benchini kwenye mechi ya Arsenal wakati ile ya Man City alitokea nje kuchukua nafasi ya Bruno Fernandes. Sasa anaweza kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

DO 02

2. Matheus Cunha; Chaguo jingine kubwa ni kubadilisha mpangilio wa safu ya ushambuliaji. Carrick amemtumia Bryan Mbeumo kama mshambuliaji pekee katika mechi zake zote mbili hadi sasa, na mchezaji huyo wa Cameroon amefunga dhidi ya Man City na Arsenal.

Hata hivyo, mchango wa Matheus Cunha akitokea benchini hauwezi kupuuzwa na Mbrazili huyo mwenyewe amekiri ana kiu ya kuanza.

Cunha alifunga bao la ushindi la kuvutia dhidi ya Arsenal baada ya kuingia uwanjani dakika ya 69 akimchukua Mbeumo, akishirikiana na Kobbie Mainoo kabla ya kupiga shuti lililotinga kona ya chini ya lango kutoka nje ya boksi.

Anafanya vizuri zaidi katikati ya uwanja, hasa akicheza nyuma ya mshambuliaji mwingine, lakini pia ana uwezo wa kuanza upande wa kushoto na kukata kuelekea ndani kwa mguu wake wa kulia hatari.

DO 03

3. Amad Diallo; Man United pia ina mchezaji mwenye mguu wa kushoto katika kikosi cha kwanza, Amad.

Mchezaji huyo wa Ivory Coast hupendelea kucheza upande wa kulia na kukata kuelekea ndani, lakini anaweza kuhamishiwa upande wa kushoto ili kucheza kama winga wa asili.

Iwapo hilo litafanyika, Mbeumo anaweza kurejeshwa upande wa kulia, alipokuwa akicheza chini ya Amorim, huku Cunha akiwa mshambuliaji wa kati na Bruno Fernandes akicheza kama namba 10.

Amad ameonyesha uwezo wa kucheza nafasi tofauti, hata kucheza kama wing-back wa kulia chini ya Amorim.

Hata hivyo, Carrick huenda hataki kuwachezesha wachezaji wengi nje ya nafasi zao halisi, hasa kwa kuwa mafanikio yake ya awali Man United yamejengwa juu ya kurahisisha mambo na kuwaweka wachezaji kwenye nafasi wanazozimudu zaidi.

DO 04

4. Shea Lacey; Carrick amekuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu imani yake kwa akademi ya Man United, ambayo ilikosolewa sana wakati wa enzi ya Amorim.

Kiungo huyo wa zamani wa Man United ana uhusiano mzuri na wachezaji vijana wa klabu na anafahamu vyema kipaji cha Shea Lacey.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 18 amecheza mechi mbili kama mchezaji wa akiba katika Ligi Kuu msimu huu, ingawa alionyeshwa kadi nyekundu katika kipigo cha 2-1 cha Kombe la FA dhidi ya Brighton mapema mwezi huu.

Kama ilivyo kwa Amad, Lacey anapendelea kucheza upande wa kulia akikatiza kuelekea ndani kwa mguu wake wa kushoto, lakini anaweza kupewa nafasi zaidi katika wiki zijazo.