Paris na Ufaransa inavyotawala Afcon

Makala ya 34 ya mashindano ya soka ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mataifa  Afrika, Afcon 2023, yamehitimika huko Ivory Coast na wenyeji ‘Tembo’ kulibakisha kombe nyumbani.
Tofauti na mabara mengine, Afcon imetawaliwa sana na ushindani wa kitamaduni wa kurithi kutoka kwa wakoloni miongoni mwa timu shiriki.

Mataifa mengi yanayoshiriki michuano hiyo yaliyotawaliwa aidha na Uingereza au Ufaransa na hata ushindani wake umegawanyika hivyohivyo.
Hata mashindano yenyewe yana majina mawili rasmi kutokana na lugha zao.
Kwa yale mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza, mashindano haya yanaitwa Afcon, lakini kwa waliotawaliwa na Ufaransa, yanaitwa Can.

Kama uliyafuatilia vizuri mashindano ya mwaka huu, utakuwa ulimuona Didier Drogba wa Ivory Coast akiwa na fulana yale iliyoandikwa Can 2023… hiyo ni sawa na kusema Afcon 2023.
Hata fainali ya mwaka huu iliangukia huko huko, Waingereza (Nigeria) dhidi ya Wafaransa (Ivory Coast).

Kwa hiyo ushindi wa 2-1 wa Ivory Coast haukuwa tu ushindi wao bali ushindi wa Wafaransa wa Afrika dhidi ya Waingereza wa Afrika.

Kombe la Ivory Coast likawa la 16 kwa mataifa ya Kifaransa ya Afrika dhidi ya mataifa ya Kiingereza ya Afrika.
Zaidi ya hapo likawa kombe la tano mfululizo kwa Wafaransa wa Afrika.

Mgawanyo wa makombe ya Afcon
Waingereza - 17
Wafaransa - 16
Wareno - 0
*Wengineo - 1
Wahispaniola - 0
*Ethiopia haikuwahi kutawaliwa

Ukiangalia takwimu utaona Waingereza wanaongoza kwa kutwaa makombe mengi, lakini wanafaidika na kuchelewa kwa Wafaransa kuanza kushiriki.

Wakati mashindano haya yanaanza, 1957, yalishirikisha mataifa ambayo yameshapata uhuru tu na ndiyo maana yaliitwa mataifa huru ya Afrika.

Nchi za Kifaransa zilichelewa sana kupata uhuru. Mfaransa wa kwanza kushiriki alikuwa Tunisia, 1963 katika makala ya nne.
Kabla ya hapo walishiriki Waingereza na Ethiopia pekee.

Lakini ukianza kuhesabu makombe tangu Wafaransa waanze kushiriki, wanaongoza.

KWANINI
Mataifa ya Kifaransa yanafaidika sana na ukaribu wao na mkoloni wao.
Wakati wa ukoloni kulikuwa na sera ambayo Ufaransa iliitumia katika makoloni yake.
Sera hii iliitwa ASSIMILER, neno la Kifaransa ambalo kwa Kiswahili linatafsirika kama kufanana.
Ufaransa ilitaka kuwabadili watu wote waliokuwa kwenye makoloni yao wajione wanafanana na Wafaransa kiutamaduni na mienendo yote ya maisha.

Kupitia sera hii, Ufaransa ilitaka kufuta kila kitu cha wenyeji na kupandikiza kila kitu chao lugha, imani (dini) na kila kitu.
Hii ilikuwa tofauti na wakoloni wengine kama Waingereza.Japo haikufanikiwa moja kwa moja, lakini sera hii ilichangia sana kuwafanya Wakoloni waione Ufaransa kama nyumbani kwao na Paris kama jiji lao.

Watu wengi kutoka makoloni ya Ufaransa walihamia huko na kuwa raia, wakazaa watoto ambao wengine waliangukia kwenye mpira na baadhi yao kuchagua kuyatumikia mataifa ya asili ya wazazi wao.

Hapo ndipo balaa linapokuja kwenye Afcon, timu nyingi za Kifaransa zimejaza wachezaji ambao walizaliwa Ufaransa hususani jiji la Paris.

Kwenye Afcon ya mwaka huu ilikuwa na wachezaji 200 waliozaliwa nje ya mataifa yao ya asili, 107 kati yao walizaliwa Ufaransa na 54 ni jiji la Paris. Hii imekuwa hivyo tangu Wafaransa wa Afrika walipoanza kushiriki Afcon.