Panga kubwa lapita Arsenal

Muktasari:
- Jorginho na Kieran Tierney ni miongoni mwa waliotemwa na klabu baada ya mikataba yao kumalizika.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imetoa orodha ya wachezaji wanaobaki na wanaoondoka ambayo inaonyesha kuna panga kubwa limewapitia mastaa 17.
Jorginho na Kieran Tierney ni miongoni mwa waliotemwa na klabu baada ya mikataba yao kumalizika.
Wakati huo huo, Thomas Partey yuko kwenye mazungumzo kuhusu mkataba mpya.
Kiungo huyo, mwenye umri wa miaka 31, amehusishwa na kuondoka Emirates huku mkataba wake ukimalizika mwezi huu na timu kama Barcelona, Atletico Madrid na Juventus zote zinatamani huduma yake.
Timu za Saudi Arabia pia zinafuatilia hali yake licha ya ukweli kwamba yeye mwenyewe anataka kubaki katika jijini la London.
Tovuti ya The Sun inaeleza kuwa mazungumzo ya kuongeza mkataba yanaendelea huku Mikel Arteta na mkurugenzi wa michezo Andrea Berta wakiwa na hamu kubwa ya kuendelea kuipata huduma yake.
Taarifa ya klabu kuhusu Partey ilisema: “Majadiliano yanaendelea, na pindi yatakapokamilika baina ya pande zote, tutatoa taarifa.”
Kwa upande mwingine, Jorginho yuko karibu kujiunga na Flamengo kama mchezaji huru wakati beki wa kushoto Tierney anatarajiwa kurejea Celtic mwezi ujao.
Nyota waliokuwa kwa mkopo Pedro Neto na Raheem Sterling wote wamethibitishwa kurejea kwenye timu zao na hawatapewa mikataba ya kudumu.
Sterling bado hajui hatima yake huko Stamford Bridge, licha ya kubakisha miaka miwili kwenye mkataba wake na benchi la ufundi halijaonyesha kumzingatia sana kutokana na kiwango kibovu alichoonyesha akiwa Arsenal ambako alianza katika mechi 13 katika michuano yote na kufunga bao moja.
Mazungumzo kati ya Sterling na Chelsea yatafanyika mwezi huu, lakini hatashiriki Kombe la Dunia la Klabu nchini Marekani.
Waliotemwa wengine wengi ni makinda na wengine wa kutoka katika timu ya wanawake.