Osimhen aitamani tena Italia, Juventus yatajwa

Muktasari:
- Staa huyu kwa sasa anaichezea kwa mkopo Galatasaray ambako ameendelea kuonyesha kiwango bora, mkataba wake na Napoli unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
MSHAMBULIAJI wa Napoli na timu ya taifa ya Nigeria, Victor Osimhen, 26, ambaye mara kadhaa ametajwa ana mpango wa kwenda England, imefichuka pia angependa kurudi Italia ambako Juventus inahitaji saini yake.
Staa huyu kwa sasa anaichezea kwa mkopo Galatasaray ambako ameendelea kuonyesha kiwango bora, mkataba wake na Napoli unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi timu nyingi zilihitaji kumsajili lakini changamoto kubwa ilikuwa ni kiasi cha zaidi ya Euro 100 milioni kilichohitajika na Napoli ili kumuuza, hali hiyo ikasababisha ajiunge na Galatasaray katika dakika za mwisho.
Tangu kuanza kwa msimu huu, akiwa na Galatasaray, Osimhen amecheza mechi 30 za michuano yote, amefunga mabao 26 na kutoa asisti tano.
Adam Wharton
MANCHESTER City na Manchester United zipo katika vita kali ya kuiwania saini ya kiungo wa Crystal Palace anayeichezea timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 21, Adam Wharton, 21, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Wharton ni mmoja kati ya mastaa wa Palace walioonyesha kiwango bora tangu msimu uliopita na alihitajika na baadhi ya timu lakini alichagua kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Martin Zubimendi
REAL Madrid inataka kuingilia mpango wa Arsenal wa kutaka kumsajili kiungo wa Real Sociedad na timu ya taifa ya Hispania, Martin Zubimendi,26, ambapo itaweka kiasi kikubwa cha pesa zaidi ya kile ambacho washika mitutu hao wamepanga kukitoa. Mpango wa Madrid kumsajili fundi huyu ni katika harakati za kufanya mabadiliko ya kikosi chao kuelekea msimu ujao. Msimu huu ameonyesha kiwango bora licha ya timu yake kutolewa kwenye michuano ya Europa League na Man United.
Kenan Yildiz
MABOSI wa Manchester United wamemwongeza mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Uturuki, Kenan Yildiz, 19, katika orodha ya washambuliaji ambao inahitaji kuwasajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuboresha eneo hilo. Mbali ya Yildiz, Man United pia inataka kumsajili fundi wa RB Leipzig na Uholanzi, Xavi Simons, 21 ambaye anawaniwa pia na Liverpool ya Ligi Kuu England.
Ethan Nwaneri
ARSENAL imepanga kumpa mkataba mpya wa miaka mitano winga wao Ethan Nwaneri, 18, mwisho wa msimu huu baada ya kuona timu kibao zikiwemo Chelsea na Manchester City zimeanza kuinyemelea saini yake. Fundi huyu wa kimataifa wa England ni miongoni mwa wachezaji vijana wa Arsenal waliopandishwa kutoka kwenye akademi yao ambao wamekuwa bora.
Ferran Torres
BARCELONA itakuwa tayari kumuuza mshambuliaji wao raia wa Hispania, Ferran Torres, 25, kwa takriban Pauni 30 milioni dirisha lijalo la majira ya kiangazo. Timu kibao ikiwemo Aston Villa, Liverpool na Manchester United wameonyesha kuvutiwa na mshambuliaji huyu wa zamani wa Manchester City. Mkataba wa staa huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Rayan Ait-Nouri
TOTTENHAM ipo tayari kulipa Pauni 40 milioni kwenda Wolves ili kuipata saini ya beki kisiki wa timu hiyo na Algeria, Rayan Ait-Nouri, 23, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Ili kuipata huduma yake, Spurs itatakiwa kushinda vita dhidi ya vigogo wengine wa England ikiwemo Liverpool, Arsenal na Manchester United ambao pia wanahitaji saini yake.
Antonio Rudiger
BEKI kisiki wa Real Madrid, Antonio Rudiger, 32, amesisitiza hana mpango wa kuondoka timu hiyo licha ya timu kutoka Saudi Arabia ikiwa pamoja na Al-Nassr kuonyesha nia ya kutaka kumsajili mwisho wa msimu huu. Rudier ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani, msimu huu amecheza mechi 41 za michuano yote.