Onana langoni tena kwa Galatasaray

Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amesema anaamini kuwa kipa wake, Andre Onana atarudi katika kiwango chake wakati kikosi chake kikirudi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Onana ambaye alikuwa lawamani wakati Man United ikilala kwa mabao 4-3 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, leo anatarajiwa kuanza langoni dhidi ya Galatasaray.
Akizungumzia kuhusu nafasi ya kipa wake, Ten Hag alisema anaamini kuwa Onana bado ni kipa mzuri na anaendelea kuwa sawa akiwa ndani ya kikosi kipya msimu huu.
"Bado ana muda wa kujifunza na kuzoea, makosa kwenye mchezo ni kawaida ila yanapotokea katika nyakati ngumu inaumiza. Naamini atakuwa na mchezo mzuri kwasababu ana muda wa kujiimarisha.
"Hakuna mashaka juu yake, amajua kuwa anatakiwa kutoa zaidi kwa timu, kuinua kiwango chake, lakini bado hatuoni kama ni tatizo kwake kuendelea kukaa langoni," alisema kocha huyo wa zamani wa Ajax.
Akizungumzia mchezo wa leo, Ten Hag alisema wanatakiwa kupata ushindi ili kurejesha imani katika kundi lake, kwani bado hawajapata ushindi na kutumia uwanja wao wa nyumbani kuwatuliza mashabiki.
"Tunataka kuwatuliza mashabiki, wote tunajua kuwa hatuna mwenendo mzuri. Kila mtu anataka kuona hali inabadilika haraka.," alisema.
Man United imepoteza mechi tano kati ya saba za mashindano yote msimu huu, wakati ikianza vibaya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kipigo cha ugenini, huku ikitoka kuchapwa na Crystal Palace kwa bao 1-0.
Katika michezo mingine, Arsenal itakuwa uwanjani dhidi ya Lens ya Ufaransa, wakati mchezo mwingine wa Kundi D ukizikutanisha PSV Eindhoven dhidi ya Sevilla.
Mabingwa watetezi, Real Madrid wasafiri kuifuata timu iliyo katika kiwango bora msimu huu, Napoli, ukiwa mchezo wa Kundi C, wakati Union Berlin ikicheza na Sporting Braga.
Ligi ya Mabingwa Ulaya
Leo Oktoba 03, 2023
KUNDI A
FC Copenhagen vs Bayern Munich
Man United vs Galatasaray
KUNDI B
Lens vs Arsenal
PSV Eindhoven vs Sevilla
KUNDI C
Union Berlin vs Sporting Braga
Napoli vs Real Madrid
KUNDI D
Salzburg vs Real Sociedad
Inter Milan vs Benfica