Ole amshika shingo Klopp

Ole amshika shingo Klopp

Muktasari:

KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemtaka mwenzake wa Liverpool, Jurgen Klopp kuacha kutafuta huruma ya marefa akitumia mbinu ya kuituhumu timu yake kuwa inabebwa.

MANCHESTER ENGLAND. KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amemtaka mwenzake wa Liverpool, Jurgen Klopp kuacha kutafuta huruma ya marefa akitumia mbinu ya kuituhumu timu yake kuwa inabebwa.

Juzi, Klopp aliwashutumu waamuzi kwa kuipa penalti za mara kwa mara Man United akidai wanaibeba katika mbio za ubingwa, kauli ambayo imemshangaza Solksjaer ambaye ameitafsiri kuwa inalenga kuwapa presha marefa waibebe Liverpool.

“Huo ndio ukweli na ndio litakuwa jibu langu. Ni kweli kwamba tumepata penalti nyingi kuliko yeye,” alisema Solksjaer.

“Sijui penalti ngapi wamepata. Sihesabu penalti zao, hivyo kama wanatumia muda wao kuhofia penalti zetu pale tunapofanyiwa faulo, mimi siwezi kupoteza muda wangu kujadili zao.”

Nyota huyo wa zamani wa timu hiyo anaamini kauli ya Klopp inalenga kutengeneza mazingira ya kuwafanya marefa watoe uamuzi wenye kuidhoofisha Man United na kuinufaisha Liverpool kwenye mbio za ubingwa.

Solskjaer alitolea mfano wa msimu uliopita ambapo waamuzi waliikandamiza timu yake ilipokutana na Chelsea ikiwa ni muda mfupi baada ya kocha Frank Lampard kutoa kauli inayoelekea kufanana na ya Klopp.

“Siwezi kuwasemea makocha wengi, lakini mbona wao wanalisema hili. Nadhani ilifanya kazi msimu uliopita kwenye nusu Fainali ya Kombe la FA ambapo Frank Lampard alizungumza kuhusu hilo,” alisema.

“Tulikuwa na fursa ya kupata penalti ya wazi ambayo tulistahili na hatukupewa, hivyo naamini hiyo ni njia ya kushawishi marefa. Sijui, lakini pia siwezi kuwa na hofu kwa hilo. Wakiwafanyia faulo wachezaji wangu ni penalti ikiwa ni ndani ya eneo la hatari,” alisema Solskjaer.

Msimu uliopita, Manchester United walipata penalti 22 ambazo ni idadi kubwa zaidi ya zilizotolewa kwa timu moja kwenye ligi kubwa tano barani Ulaya.

Muda mfupi baada ya Liverpool kuchapwa bao 1-0 na Southampton, Klopp aliwalalamikia waamuzi kuwa wamekuwa hawaitendei haki timu yake kwa kuinyima penalti ambazo imekuwa ikistahili kuzipata ingawa wamekuwa wepesi kuizawadia Man United.

“Nimesikia kuwa Manchester United sasa hivi wana penalti nyingi ndani ya miaka miwili kuliko ambazo mimi nimepata ndani ya miaka mitano na nusu. Ilionekana ni penalti ya wazi na nilimgeukia refa wa nne na kusema tutaiangalia? Akanijibu kuwa imeshaangaliwa tayari hakuna penati,” alisema Klopp alipozungumzia tukio la mshambuliaji wake, Sadio Mane kuangushwa ndani ya eneo la hatari la Southampton na Walker-Peters ingawa Liverpool haikuzawadiwa pigo la penalti.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Klopp imeonekana kuwashangaza wengi kwani takwimu zinaonyesha tofauti na kile alichokisema kuwa United chini ya Solskjaer imepata penati nyingi kulinganisha na penati ambazo Liverpool imepata chini ya uongozi wa Klopp katika kipindi cha miaka mitano na nusu aliyoinoa.;

Wakati United ikipata penalti 27 chini ya Solksjaer, Liverpool yenyewe chini ya Klopp imepata jumla ya penati 30.

Liverpool na Manchester United zinakabana koo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya England zikiwa na pointi 33 kila moja lakini Liverpool wanaongoza kwa kuwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa kuizidi United.

Hata hivyo Liverpool imecheza idadi kubwa ya michezo kulinganisha na wenzao kwani wao wamecheza mechi 17 wakati Manchester United wamecheza mechi 16.