Prime
Rekodi tatu mwamuzi Dabi ya Kariakoo

MCHEZO wa Dabi ya Kariakoo umeingia kwenye historia mpya baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuwashusha waamuzi kutoka Misri na Somalia, huku rekodi za mwamuzi wa kati zikiwa tishio.
Taarifa iliyotolewa na TPLB jana ni, mchezo huo utaamuliwa na Amin Omar atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Mahmoud El Regal, Samir Mohamed, huku mwamuzi wa nne mezani akiwa Ahmed Elghandour wote kutoka Misri.
Kwa upande wa mtathimini waamuzi ni Alli Mohamed kutoka Somalia, huku kamishna wa mechi ni Salim Omary Sindano kutoka Tanga, Tanzania.
Hii inakuwa mara ya kwanza kihistoria kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara kuamuliwa na waamuzi kutoka nje ya Tanzania na Dabi ya Kariakoo imeingia kwenye rekodi hiyo.
Omar sio mwamuzi rahisi akiwa uwanjani na ana rerkodi ya kumwaga kadi nyingi za njano na nyekundu na suala la kuamua penalti sio gumu kwake.
Rekodi zinaonyesha katika mechi 239 ambazo mwamuzi huyo amechezesha za michuano tofauti, ameonyesha kadi za njano 823 huku nyekundu zikiwa 20 na mikwaju ya penalti 85.
Uteuzi wa waamuzi hao umekuja baada ya Dabi ya Kariakoo kuahirishwa mara mbili, kutoka Machi 8, 2025 kisha Juni 15, 2025 na sasa Juni 25, 2025 na waamuzi wa awali waliopangwa ni Ahmed Arajiga aliyekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Mohammed Mkono na Kassim Mpanga, huku mwamuzi wa nne ni Amina Kyando.
REKODI ZAKE KWA TIMU ZA TANZANIA
Katika mechi 239, rekodi zinaonesha Omar amewahi kusimamia mechi tatu zinazohusu timu za Tanzania na ni Taifa Stars, Yanga na Simba.
Mechi ya kwanza ilikuwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2022-2023 iliyofanyika Februari 11, 2023 nchini Guinea na wenyeji Horoya AC ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Baada ya hapo, akawa mwamuzi wa katika katika mchezo wa Kundi F kwenye michuano ya Afcon 2023 uliochezwa Januari 24, 2024 nchini Ivory Coast na ulizikutanisha Tanzania dhidi ya DR Congo na kumalizika kwa matokeo ya 0-0.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/24 hatua ya robo fainali, mwamuzi huyo alichezesha mechi ya Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns iliyomalizika kwa matokeo ya 0-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar. Ilikuwa Machi 30, 2024.
KAULI YA MWENYEKITI WA WAAMUZI
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Nassor Hamduni, alisema ujio wa waamuzi kutoka Misri kuchezesha Dabi ya Kariakoo ni suala la ushirikiano tu, hamna tatizo lolote.
Pia amefunguka, wamefanya hivyo kutokana na waamuzi waliopangwa kuchezesha mchezo huo kutokuwepo nchini na hawakuwa na namna nyingine ya kuwaandaa wengine.
“Kushirikiana katika michezo si jambo baya na huo ni mwanzo tu waamuzi kutoka ndani watatoka na kwenda huko na sisi tutawaleta wengine kuja kuchezesha huku, pia ni fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzetu,” alisema na kuongeza.
“Huwezi kuwaandaa waamuzi kwa uharaka wachezeshe mechi ya dabi ambayo inatazamwa na watu wengi duniani, ni mechi kubwa, hivyo tunaamini ujio wa waamuzi hao ni sehemu sahihi kwani hata wetu wamekuwa wakipata fursa ya kutoka kwenda kuchezesha mechi kubwa kwa nini sisi tusifanye hivyo.”
KANUNI ZINASEMAJE?
Kanuni za Ligi Kuu Tanzania toleo la 2024, Kanuni ya 39 imeainisha masuala kuhusu waamuzi kupitia vifungu mbalimbali.
Kanuni hiyo inaeleza hivi: “(1) Kutakuwa na waamuzi TEULE (select referees) ishirini na nne (24) na waamuzi wasaidizi arobaini (40) watakaoteuliwa na Kamati ya Waamuzi ya TFF mwanzoni mwa kila msimu maalum kwenye Orodha ya Waamuzi watakaopangwa kuchezesha michezo ya Ligi Kuu. Waamuzi TEULE hawa wanawajibika kuwa waaminifu, waadilifu na wenye nidhamu na tabia njema zisizotiliwa mashaka.
“(2) Katika Orodha ya Waamuzi Teule wa Ligi Kuu kutakuwepo waamuzi wachache wa akiba kwa Ligi Kuu wanaoweza kujumuishwa kuchezesha michezo ya Ligi Kuu katika mazingira ya dharura au uwepo wa haja ya kufanya hivyo kwa sababu zinazoaminika. Katika Mazingira ya kawaida, Waamuzi wa Akiba katika Orodha ya Waamuzi teule wa Ligi Kuu watatumika kuchezesha Ligi ya Championship.
“(3) Mwamuzi TEULE yeyote wa Ligi Kuu anaweza kuondolewa wakati wowote endapo TFF itajiridhisha au kubaini Mapungufu katika uwezo wake, Uadilifu au Uwajibikaji wake kwenye michezo na kuhusiana na Ligi Kuu na michezo mingine aliyopangiwa na wakati wowote TFF inaweza kufanya Uteuzi wa Mwamuzi TEULE wa Ligi Kuu kwa Mazingatio ya Sifa na Vigezo kwa Mujibu wa Kanuni hizi.
(4) Waamuzi TEULE watateuliwa wakijumuisha waamuzi na waamuzi wasaidizi walio na hadhi ya FIFA, pia kutoka miongoni mwa waamuzi wazoefu na vijana wanaofanya vizuri sana kwa kipindi husika walio na Hadhi ya Daraja la Kwanza (Class I).”
Kuhusu upangwaji wa waamuzi hao, kanuni hiyo kipengele cha 7 imeanisha huku pia kipengele cha 8 kikitoa mwongozo wa kufuatwa endapo timu mojawapo haitaridhika na uteuzi huo.
Kanuni hiyo inasema: “(7) Kamati ya Waamuzi ya TFF itapanga Waamuzi kwenye Michezo ya Ligi Kuu na ndiyo pekee yenye mamlaka ya kupanga, kubadilisha na kuondoa mwamuzi kwenye ratiba kwa Utaratibu na Mfumo uliowekwa (kwa kushirikiana na Sekretarieti ya TFF) kwa Mazingatio ya Kanuni hizi.”
“(8) Klabu au yeyote aliye na malalamiko au jambo kuhusu kupangwa au Uchezeshaji wa mwamuzi anawajibika kuwasilisha kwa Maandishi kwa TFF si chini ya siku tatu (3) katika mazingira ya wakati kabla ya Mchezo na/au wakati mwingine wowote baada ya Mchezo husika. Hairuhusiwi kwa klabu/Kiongozi/Kocha/Mchezaji kumkataa mwamuzi yeyote aliyepangwa wala kumjadili au kushutumu kwa namna yoyote au kwenye vyombo vya habari. TFF itachukua hatua katika mazingira ya uvunjifu wa sharti hili.”