NYUMA YA PAZIA: Afadhali Paulo na shetani wamefika mwisho wao
ILIKUWA miongoni mwa hadithi mbaya za mapenzi ambazo mwandishi amewahi kuandika. Lakini afadhali mwandishi ametuandikia sentensi ya mwisho katika hadithi hii na sasa tunaweza kwenda kulala. Hadithi ilitwa penzi la Paulo na shetani.
Namaanisha Paul Pogba na Manchester United ambao huwa wanajiita Mashetani Wekundu. Afadhali uhusiano wao umefika mwisho. Mapema wiki hii walipeana talaka baada ya ndoa yao kudumu kwa miaka sita. Subiri kwanza. Hii ilikuwa ndoa yao ya pili. Waliwahi kuoana hapo mwanzo, wakaachana, wakarudiana mwaka 2016 lakini sasa wameachana tena. Naamini hawatarudiana.
Inakera kurudia mara kwa mara hadithi ya Pogba na Manchester United. Nimeandika mara nyingi na sasa sina cha kuandika. Afadhali yangu ni kwamba hii inaweza kuwa mara ya mwisho kuandika kitu kuhusu Manchester United na mchezaji anayeitwa Paul Pogba.
Tutaendelea tulipoishia. Kwamba inakuwa mara ya pili kwa Pogba kuondoka bure Manchester United. Mara yake ya kwanza alimuacha Sir Alex Fergsuon akiwa na hasira dhidi yake na wakala wake, Hayati Mino Raiola. Sir Alex alikaririwa akidai kwamba hakuwahi kuona mtu wa ovyo kama Raiola.
Wakati ule alikuwa anamuandaa Pogba kuchukua mikoba ya Paul mwenzake, Paul Scholes. Hata hivyo Scholes alikuwa hajaisha vizuri. Raiola akamshawishi Pogba waondoke zao. Wakaondoka huku Pogba akiwa kinda. Akaenda kukomaa Juventus.
Safari hii Pogba anaondoka tena bure kwa mara nyingine. Alirudi mwaka 2016 akiwa mchezaji ghali duniani. Kocha alikuwa Jose Mourinho lakini wakala alikuwa yuleyule Raiola. Hata hivyo muda mwingi wa maisha yake Old Trafford ulijaa migogoro.
Afadhali wameachana kwa sababu walishindwa kusaidiana. Pogba aliletwa klabuni akiwa staa kwa ajili ya kuisaidia United kurudi katika njia ya mataji. Kipaji kikubwa kilikuwepo miguuni. Pasi zake za mwisho. Umiliki wake wa mpira. Maono yake uwanjani. Kipaji kilikuwepo.
Tatizo kubwa ali-shindwa kuisaidia United kwa sababu ya mambo mengi. Kwanza nje ya uwanja muda wote wakala wake, Raiola alikuwa akileta migogoro klabuni. Mara watishie kuondoka. Pogba akiwa Japan katika ziara binafsi aliwahi kusema kuwa alikuwa ameichoka United na anataka kuondoka. Wakati huo kocha alikuwa Ole Gunnar Solskjaer.
Nje ya uwanja Pogba alikuwa bize kwelikweli kubadilisha staili za nywele. Ndani ya uwanja Pogba alikuwa na kipaji maridhawa lakini ambacho kilikosa mwendelezo wa ubora.
Alipaswa kufanya zaidi kufikia mambo ambayo kama Kelvin de Bruyne alikuwa anafanya pale Manchester City.
Matokeo yake alijikuta haisaidii sana timu. Lakini pia kumbuka kwamba hata United yenyewe ilikuwa haimsaidii vyema Pogba. Afadhali wameachana. Akiwa na Juventus, Pogba alikuwa amezungukwa na mastaa wakubwa na wenye uwezo.
Anapokuwa na timu ya taifa ya Ufaransa pia Pogba anazungukwa na mastaa wakubwa wenye uwezo. Haishangazi kuona mwaka 2018 pale Moscow, Russia alinyanyua makwapa yake kwa kutwaa Kombe la Dunia. Ufaransa huwa anazungukwa na kina Antoine Griezmann, Kylian Mbappe, N’Golo Kante na wengineo.
Akiwa Old Trafford Pogba anazungukwa na Fred na Scott McTominay. Unaweza kuona tofauti. Sawa, Pogba alikuwa haisaidii sana Manchester United lakini sidhani kama na United nayo ilikuwa inamsaidia sana Pogba. Ni sawa na ambavyo De Bruyne na mastaa wa Manchester City wanavyosaidiana.
Kama Pogba angekuwa amezungukwa na Paul Scholes, David Beckham, Roy
Keane, Andy Cole, Ryan Giggs na wengineo labda huenda angefanya vizuri zaidi. Lakini kwa United hii unaweza kuona hata Bruno Fernandes ameanza kuchoka. Kwa sasa anaishia kulalamikia waamuzi na wachezaji wenzake.
Afadhali Paul na shetani wake wameachana. Yajayo yasingekuwa mazuri sana. Nadhani uamuzi wake ulikuwa umefikiwa kabla ya kocha mpya, Erik Ten Hag kutua Manchester United.
Lakini ukweli ni kwamba kwa ninavyomuona huyu kocha mpya, hata kama Pogba angekuwa bado na mkataba na Manchester United huenda wasingekuwa na uhusiano mzuri.
Ten Hag kama walivyo makocha wa kisasa wanaopata mafanikio, anahitaji wachezaji ambao hawana majivuno (egoism). Anahitaji wachezaji ambao watajitolea hasa kwa ajili ya timu. Kukaba kwa pamoja na kucheza kwa pamoja.
Pogba sioni sana kama ni mchezaji wa aina hiyo. Ana kipaji kikubwa pale ambapo anakuwa na mpira mguuni. Unaweza kumkumbuka zaidi kwa pasi zake ndefu, lakini hauwezi kumkumbuka sana kwa uchezaji wa pamoja.
Kwa United hii sitashangaa wachezaji wengi wanaojiona mastaa wakihenya na kuondoka Trafford. Ni kama ambavyo rafiki zao Arsenal chini ya Mikel Arteta walianza kuondokana na kina Mesut Ozil na Pierre-Emerick Aubameyang. Nadhani mwanga wameanza kuuona.
Lakini tukimgeukia Paul mwenyewe ni wazi kwamba mwisho wake Manchester United haujawa mzuri kama ambavyo alitaka. Kama angeondoka miaka miwili iliyopita nadhani alikuwa wa moto na angeweza kuzusha gumzo sokoni. Lakini kwa sasa hapana.
Anatajwa kurudi katika klabu yake ya zamani Juventus. Ni wazi kwamba amekubali kukatwa mshahara ili arudi katika klabu yake ya zamani.
Hii ina maana kwamba klabu zenye uwezo wa kulipa mishahara mikubwa zote zimemchomolea.
Pogba ameondoka akiwa hana moto. Ungeweza kudhani Real Madrid wangejitosa kwake, PSG labda wangejitosa kwake, Manchester City labda wangetupa ndoana. Wote wamejiweka kando na wamemuacha apite aendelee na safari yake.Katika umri wa miaka 29 ni ishara tosha kwamba sasa analazimika kujikita zaidi katika soka na kuachana na mambo mengi ya nje ya uwanja.
Lakini katika kuperuzi kwangu nimegundua kwamba mashabiki wengi wa United hawajaumia kwa Pogba kuondoka klabuni hapo. Hii ina maana mchango wake hawajauthamini na hawaoni pengo lake.
Lakini United pia nao wanahitaji kujitathmini. Zamani ilikuwa ni timu yenye mvuto na ambayo wachezaji wengi walitamani kuichezea, lakini sasa hivi wameanza kuwa timu ya kawaida ambayo wachezaji wengi hawaiheshimu.
Pogba ni miongoni mwa wachezaji ambao wameonekana wazi kuichezea thamani ya Manchester United. Mkataba wake wa miaka sita ulijaa kiburi dhidi yao. Haipaswi kuwa hivi.
United warudishe heshima yao uwanjani waone kama mchezaji kama Pogba anaweza kuwachezea kama ambavyo alifanya katika ujio wake wa pili. Alijiona ni mkubwa kuliko timu.