Misri yawashtika waamuzi kwa FIFA
Muktasari:
- Misri ilitolewa kwa kichapo cha mabao 3-2 baada ya Argentina kufanya mgeuko wa ajabu katika dakika za mwisho za mchezo uliopigwa jijini Atlanta.
CAIRO, Misri: SHIRIKISHO la Soka la Misri (EFA) limewasilisha malalamiko rasmi kwa FIFA likitaka waamuzi waliosimamia mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Argentina waondolewe katika Kombe la Dunia, likidai walifanya makosa makubwa yaliyoigharimu timu hiyo nafasi ya kusonga mbele.
Misri ilitolewa kwa kichapo cha mabao 3-2 baada ya Argentina kufanya mgeuko wa ajabu katika dakika za mwisho za mchezo uliopigwa jijini Atlanta.
Katika taarifa yake rasmi, EFA ilisema rais wa shirikisho hilo, Hany Abou Rida, amewasilisha malalamiko kwa FIFA akiomba kufunguliwa uchunguzi dhidi ya mwamuzi wa Ufaransa, Francois Letexier, pamoja na timu nzima ya waamuzi kwa kile ilichokiita matumizi ya viwango tofauti vya maamuzi.
"Rais wa Shirikisho la Soka la Misri, Hany Abou Rida, amewasilisha malalamiko kwa FIFA akitaka uchunguzi ufanyike dhidi ya mwamuzi Mfaransa Francois Letexier kufuatia makosa makubwa ya uamuzi yaliyofanywa na waamuzi pamoja na matumizi ya viwango tofauti vya maamuzi, jambo lililosababisha Misri kupoteza mchezo na kuondolewa kwenye Kombe la Dunia," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Moja ya matukio yaliyolalamikiwa zaidi ni pale VAR ilipofuta bao la Mostafa Zico wakati Misri ikiwa inaongoza 1-0 katika kipindi cha pili.
Bao hilo lilibatilishwa baada ya waamuzi wa VAR kubaini kuwa kiungo Marwan Attia alimkanyaga kidogo Lisandro Martinez mwanzoni mwa shambulizi lililozaa bao hilo.
Mbali na tukio hilo, Misri pia ilidai kuwa Mohamed Salah alichezewa faulo ndani ya eneo la penalti la Argentina sekunde chache kabla ya mabingwa hao watetezi kuanzisha shambulizi lililozaa bao la ushindi katika muda wa nyongeza.
EFA imeitaka FIFA kufanya uchunguzi dhidi ya waamuzi wa uwanjani na wa chumba cha VAR, ikidai kulikuwa na "makosa ya wazi" pamoja na "kukataa kwa makusudi kupitia baadhi ya matukio muhimu ya mchezo."
Shirikisho hilo pia limetaka mwamuzi mkuu pamoja na waamuzi wote waliokuwa wakisimamia mchezo huo waondolewe kwenye mashindano baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, EFA ilidai kuwa kilichotokea kilikuwa ni "kitendo cha ubaguzi dhidi ya timu ya taifa ya Misri."
Misri ilikaribia kuandika historia ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, lakini ilishindwa kulinda uongozi wake wa mabao 2-0 baada ya Argentina kurejea kwa nguvu.
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi, alitoa pasi iliyozaa bao la kwanza la timu yake dakika ya 79 kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao la kusawazisha dakika ya 83.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Misri Hossam Hassan alisema timu yake "haikutendewa haki" na "imedhulumiwa."
"Huenda walitaka mabingwa wa dunia waendelee kwenye mashindano. Huenda walitaka Messi aendelee kubaki kwenye mashindano," alisema Hassan.
Mfungaji wa Misri, Mostafa Zico, naye alitoa tuhuma nzito dhidi ya waamuzi.
"Mwamuzi hakuwa wa haki kabisa. Dhuluma ilikuwa wazi tangu mwanzo wa mchezo."
Aliongeza:"Ni wazi kabisa kwamba mashindano haya yamepangwa."
Wakati Misri ikisubiri majibu ya malalamiko yake kutoka FIFA, Argentina sasa imeelekeza nguvu katika robo fainali ambapo itavaana na Uswisi mjini Kansas City, huku ikisaka tiketi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia.