Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldo: Sichezi kwa ajili ya pesa

Muktasari:

  • Ronaldo, ambaye ametengeneza historia kubwa katika soka la klabu na timu ya Taifa ya Ureno, amesema zawadi kubwa kwake si utajiri alioupata kutokana na soka, bali ni nafasi ya kuendelea kucheza, kufunga mabao na kuiwakilisha nchi yake katika kiwango cha juu.

MIAMI, Marekani: KWA zaidi ya miongo miwili akiwa katika kilele cha soka la dunia, Cristiano Ronaldo amesema mafanikio yake hayajawahi kuongozwa na tamaa ya fedha pekee, bali mapenzi makubwa kwa mchezo huo ambao umebadilisha maisha yake.

Ronaldo, ambaye ametengeneza historia kubwa katika soka la klabu na timu ya Taifa ya Ureno, amesema zawadi kubwa kwake si utajiri alioupata kutokana na soka, bali ni nafasi ya kuendelea kucheza, kufunga mabao na kuiwakilisha nchi yake katika kiwango cha juu.

“Fedha siyo sababu ya kwanza iliyonifanya niendelee kucheza. Kitu kinachonisukuma ni upendo wangu kwa mpira wa miguu, furaha ninayopata ninapokuwa uwanjani na heshima ya kuichezea klabu yangu pamoja na taifa langu,” amesema Ronaldo.

Kauli hiyo imekuja baada ya timu yake ya Ureno kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia 2026 kwa kufungwa bao 1-0 na Hispania ndani ya dakika 90 za mvhezo.

Pia, kauli hiyo imekuja wakati dunia ya soka ikiendelea kushuhudia sura ya mwisho ya safari ya mchezaji huyo ambaye kwa miaka mingi amekuwa miongoni mwa majina makubwa zaidi katika historia ya mchezo huo.

SAFARI YA MTOTO WA MADEIRA HADI MFALME WA SOKA

Ronaldo alizaliwa Februari 5, 1985, katika mji wa Funchal, kisiwa cha Madeira nchini Ureno.

Alikulia katika familia ya kawaida, akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wanne wa Jose Dinis Aveiro na Maria Dolores dos Santos Aveiro.

Tangu akiwa mdogo, Ronaldo alionyesha kipaji kikubwa cha soka.

Alianza kucheza katika akademi ya klabu ya eneo lao, Andorinha, kabla ya kuhamia Nacional.

Akiwa na umri wa miaka 12, kipaji chake kilivuka mipaka ya Madeira na alijiunga na akademi ya klabu kubwa ya Ureno, Sporting CP, jijini Lisbon.

Huko ndipo alipoanza kuonekana kama mchezaji mwenye uwezo wa pekee kutokana na kasi yake, uwezo wa kupiga mashuti na nidhamu yake ya mazoezi.

Mwaka 2003, akiwa na umri wa miaka 18, alisajiliwa na Manchester United chini ya kocha Alex Ferguson, hatua iliyompa nafasi ya kuingia kwenye jukwaa kubwa la soka la dunia.


MFALME WA REKODI NA MAFANIKIO

Akiwa Manchester United, Ronaldo alibadilika kutoka winga mwenye kipaji hadi kuwa mfungaji hatari zaidi duniani.

Alishinda mataji ya Ligi Kuu England, Kombe la Ligi, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mwaka 2008 alitwaa tuzo yake ya kwanza ya Ballon d'Or.

Mwaka 2009 alihamia Real Madrid kwa ada iliyokuwa rekodi wakati huo, na huko ndipo alipoandika ukurasa mkubwa zaidi wa historia yake.

Akiwa Madrid, Ronaldo alifunga  mabao mengi, akishinda mara nne zaidi tuzo ya Ballon d'Or na kusaidia klabu hiyo kutwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Baadaye alichezea Juventus ya Italia, akarudi Manchester United, kabla ya kujiunga na Al Nassr FC ya Saudi Arabia ambako aliendelea kuvunja rekodi za ufungaji.

Katika maisha yake ya soka, Ronaldo amekuwa miongoni mwa wafungaji bora zaidi duniani, akiwa amefunga zaidi ya mabao 900 katika mechi rasmi za klabu na taifa, huku akiwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Ureno.

Ureno na ndoto ya mwisho ya Kombe la Dunia 2026

Katika upande wa kimataifa, Ronaldo amekuwa nembo ya kizazi cha dhahabu cha Ureno.

Alianza kuchezea timu hiyo mwaka 2003 na baadaye kuwa nahodha, akiwaongoza wenzake kushinda taji la UEFA Euro 2016 na UEFA Nations League 2019.

Hata hivyo, taji la Kombe la Dunia la FIFA  limeendelea kuwa pengo kubwa katika kabati lake la mafanikio.


SIRI YA MAISHA MAREFU KWENYE SOKA NI NIDHAMU

Wakati wachezaji wengi wa kizazi chake tayari wamestaafu, Ronaldo ameendelea kushindana kutokana na mfumo mkali wa maisha unaohusisha mazoezi ya ziada, lishe bora, mapumziko ya kutosha na kujitunza kimwili.

Ameeleza mara nyingi kuwa mafanikio yake yametokana na mchanganyiko wa kipaji, kujituma, imani na kutokubali kushuka kiwango.

Kwa Ronaldo, safari yake haijaishia kwenye rekodi au mataji pekee, bali kwenye urithi anaouacha kwa kizazi kijacho cha wachezaji.

Kutoka mtoto aliyekulia kwenye kisiwa kidogo cha Madeira hadi kuwa mmoja wa mastaa wakubwa zaidi katika historia ya soka, Cristiano Ronaldo anaendelea kuandika hadithi ambayo huenda ikachukua miaka mingi kabla ya kupatikana mwingine mwenye mafanikio yanayokaribia yake.