Nyie, hebu msikieni fundi Zubimendi

Muktasari:
- Na staa huyo wa Kihispaniola amewahidi mashabiki wa Arsenal mambo matamu yanakuja.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO Martin Zubimendi amefunguka Arsenal ndiyo timu iliyokuwa kwenye akili yake mara tu alipoamua kufanya uamuzi wa kuachana na Real Sociedad dirisha hili la kiangazi.
Na staa huyo wa Kihispaniola amewahidi mashabiki wa Arsenal mambo matamu yanakuja.
Zubimendi alikuwa kwenye kikosi cha Sociedad kwa miaka 15 kabla ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda kukipiga huko Emirates baada ya dili la Pauni 55 milioni, huku mwaka jana alikatalia Liverpool.
Kwenye kikosi cha Arsenal, Zubimendi, 26, amesaini mkataba wa miaka mitano katika tukio ambalo amelieleza ni kubwa kwenye maisha yake ya soka.
Huo ulikuwa usajili wa pili wa Arsenal kwenye dirisha hili, baada ya kumnasa pia kipa wa Kihispaniola, Kepa Arrizabalaga kutoka Chelsea kwa ada ya Pauni 5 milioni.
Zubimendi atakuwa mchezaji wa pili wa kutoka Real Sociedad kujiunga na Arsenal ndani ya muda mfupi baada ya Mikel Merino kutua Emirates kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.
Na Zubimendi akijiandaa kwenda kuungana na mchezaji mwenzake huyo wa zamani, anaamini safu yao ya kiungo itaweza kufanya kile kinachohitajika kwenye kubeba mataji.
Zubimendi alishawahi kucheza pamoja na Merino na nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard, alisema:
“Nina furaha kuwa hapa pamoja nao.”