No Tuchel, no Ancelotti Man United!
Muktasari:
- Unajua kwanini? Kwa sasa, yeye ndiye kocha wa Manchester United, akiinoa timu hiyo kwa muda hadi mwisho wa msimu.
LONDON, ENGLAND: UNAWEZA kusema dua za Michael Carrick zinapokelewa kimyakimya kutokana na kuongezeka kwa makocha wanaohusishwa na kibarua chake anachofanya kwa sasa kusaini mikataba kwingineko.
Unajua kwanini? Kwa sasa, yeye ndiye kocha wa Manchester United, akiinoa timu hiyo kwa muda hadi mwisho wa msimu.
Lakini, baada ya kuanza vizuri katika mechi zake tano za kwanza, akishinda nne mfululizo na kutoka sare moja, jina lake likaanza kuingizwa kwenye mjadala wa kuonekana kama mtu anayefaa kukabidhiwa mikoba ya jumla ya kuwa kocha wa kudumu Man United.
Nje ya hapo, kuna makocha wengine wenye majina makubwa wamekuwa wakihusishwa na klabu hiyo ya Old Trafford, akiwamo Thomas Tuchel, Carlo Ancelotti na Luis Enrique. Ukubwa wa majina ya makocha hao, umemfanya Carrick aonekane kutokuwa na nguvu katika kupewa kibarua cha kudumu cha kuinoa miamba hiyo ya Old Trafford.
Hata hivyo, Alhamisi iliyopita, Carrick alipokea habari njema kuhusu Tuchel, kwamba amekubali kuongeza miaka miwili ya kuendelea kuinoa timu ya taifa ya England, jambo ambalo limepunguza wapinzani wake katika kuwania kiti hicho cha ukocha wa kudumu.
Na kufumba na kufumbua, kocha mwingine tena, Ancelotti naye aliripotiwa kuwa wa na mpango wa kusaini nyongeza ya mkataba wa miaka minne hadi mwaka 2030 katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil.
Hii itamfanya Mbrazili huyo kuendelea kuinoa Brazil hadi baada ya Kombe la Dunia 2030, hivyo kumtoa kwenye orodha ya makocha wanaoweza kujiunga na Man United, ambao wamekuwa wakimvutia kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa The Athletic, taratibu za mwisho za makubaliano hayo bado hazijakamilika. Hata hivyo, kuna matarajio makubwa kuwa kocha huyo mwenye mafanikio makubwa ataendelea kubaki katika wadhifa wake wa sasa.
Ancelotti alijiunga na Brazil, Mei 2025 ikiwa ni uzoefu wake wa kwanza kama kocha mkuu wa timu ya taifa, ingawa aliwahi kuwa msaidizi wa Arrigo Sacchi katika Kombe la Dunia 1994 akiwa na Italia.
Alimrithi Dorival Junior baada ya kuondoka Real Madrid. Kocha huyo wa Italia alishinda mataji mawili ya LaLiga na mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika vipindi viwili tofauti akiwa na Los Blancos. Ancelotti alitangaza kikosi chake cha kwanza Mei 26 mwaka jana kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Ecuador na Paraguay. Aliwajumuisha wachezaji aliowahi kufanya nao kazi kama Casemiro, Vinicius Junior na Richarlison. Sare ya bila kufungana dhidi ya Ecuador na ushindi wa 1-0 dhidi ya Paraguay, Juni uliihakikishia Brazil kufuzu Kombe la Dunia 2026, fainali zitazofanyika katika nchi za Marekani, Canada na Mexico majira yajayo ya kiangazi.
Baada ya kufuzu, Brazil ilicheza mechi nne za kirafiki, ushindi wa 5-0 dhidi ya Korea Kusini, kichapo cha 3-2 kutoka Japan, ushindi wa 2-0 dhidi ya mabingwa wa AFCON Senegal na sare ya 1-1 dhidi ya Tunisia.
Mkataba mpya wa Ancelotti ni pigo jingine kwa Man United, ambao bado hawajamteua mrithi wa kudumu wa Ruben Amorim. Lakini, ni furaha kwa Carrick, ambaye anaomba watu makini wapungue huko sokoni ili afikiriwe nafasi hiyo mwishoni mwa msimu.
Mashetani Wekundu wamekuwa wakimtamani Ancelotti kwa muda mrefu, lakini sasa inaonekana hatakuwa chaguo lao kwa muda wowote wa hivi karibu. Hata hivyo, kocha wa muda Carrick hajapoteza katika mechi zake tano za kwanza za Ligi Kuu England hadi sasa.
Brazil si wao pekee wanaochukua hatua za muda mrefu katika benchi la ufundi. Alhamisi, Chama cha Soka cha England, kilitangaza kuwa kocha wa England, Tuchel amesaini nyongeza ya mkataba wa miaka miwili na timu ya taifa.
Kwa nyongeza hiyo, kocha huyo raia wa Ujerumani sasa ataiongoza England hadi mwisho wa mashindano ya UEFA Euro 2028, ambayo yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yatafanyika katika ardhi ya nyumbani kote Uingereza na Ireland.