Nico Williams anukia Barca, Lamine atajwa
Muktasari:
- Licha ya uwepo wa timu nyingi, Williams ambaye msimu uliopita alifunga mabao 5 katika mechi 29 za michuano yote, tayari ameweka wazi nia yake ya kujiunga na Barcelona kupitia mazungumzo ya faragha na Lamine Yamal na wachezaji wengine wa Barcelona anaocheza nao kikosi cha Hispania.
BARCELONA, HISPANIA: STAA wa Athletic Bilbao, Nico Williams anaonekana kuwa njiani kuondoka katika timu hiyo dirisha lijalo la majira ya kiangazi na timu kibao zinahitaji huduma yake ikiwemo Barcelona.
Licha ya uwepo wa timu nyingi, Williams ambaye msimu uliopita alifunga mabao 5 katika mechi 29 za michuano yote, tayari ameweka wazi nia yake ya kujiunga na Barcelona kupitia mazungumzo ya faragha na Lamine Yamal na wachezaji wengine wa Barcelona anaocheza nao kikosi cha Hispania.
Ripoti kutoka tovuti ya SPORT inadai Williams amedhamiria kujiunga na Barcelona dirisha lijalo, licha ya Bayern Munich na Arsenal kushinikiza kumsaini.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 tayari ametuma ujumbe wa moja kwa moja kwenda kwa mastaa kama Yamal, Pau Cubarsi, Fermin Lopez na Pedri akiwaambia anataka kuungana nao Barca.
Williams anadaiwa kuwa na ndoto ya kucheza pamoja na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Hispania huko Catalunya.
Hivi karibuni ripoti zilieleza mkurugenzi wa michezo wa Barcelona Deco alikutana na wakala wa Williams, Felix Tainta, kujadili uwezekano wa uhamisho kwa dirisha lijalo.
Inaelezwa pia kocha mkuu wa Barca Hansi Flick tayari amefanya mazungumzo ya moja kwa moja na Williams na amemwelezea jinsi atakavyoweza kuendana na mfumo na namna atakavyokuwa anamchezesha.
Flick tayari ameidhinisha usajili wake na anamwona kama mchezaji bora wa kulia atakayeenda kuimarisha zaidi safu yao ya ushambuliaji.
Bilbao imeweka wazi haina shida katika kumuuza Williams lakini timu yoyote inayomhitaji itatakiwa kukubali kulipa Pauni 62 milioni ambayo imewekwa katika kipengele cha kuvunja mkataba wake.