Prime
Ngannou! wewe unatafuta Pesa, yeye pesa zinamtafuta
LAS VEGAS, MAREKANI. KUNA watu wanatafuta pesa na wengine pesa zinawatafuta. Ndivyo ilivyo kwa Francis Ngannou ambaye amepata umaarufu baada ya pambano lake na Tyson Furry lililofanyika Saudi Arabia.
Nyota huyu aliyeanzia kupigana mapambano ya mchanganyiko wa ngumi na mateke Mixed Martial Arts, kwa sasa ana pesa za kutosha kutokana pia na madili mengine.
ANAPIGAJE PESA
Chanzo chake cha kwanza cha mapato jamaa ni ngumi na ana uwezo wa kucheza michezo tofauti huku akikadiriwa kuwa na utajiri wa kufikia Dola 15 milioni.
Wakati yupo chini ya UFC kila pambano moja alilopigana alikuwa akipata chini ya Dola 1 milioni lakini baada ya kujiunga na MMA pambano lake la kwanza kucheza kwa upande wa ndondi jamaa amekunja kiasi kisichopungua Dola 10 milioni na alipigana na Furry.
Mbali na masumbwi jamaa anajipatia pesa kupitia uwekezaji mkubwa alioufanya ikiwamo mkataba wake na MMA Professional Fighters League ambao umemhakikishia kuwa na hisa kwenye mapambano ya Kanda ya Afrika na kila pambano halitokuwa chini ya milioni na atakuwa anapewa mgao kwenye faida iliyopatikana katika mapambano yake.
Pia amepewa haki ya kucheza mapambano mengine nje ya Martial Arts.
Jamaa pia anahisa kwenye kampuni ya PeaTos, na ni balozi wa The Fight Game, Cryo Pain Relief, CBD Research Labs, na Gym King Fight Division.
NDINGA
Ngannou anatajwa ni mmoja wa mastaa wanaopendelea sana kuendesha gari aina ya Rolls-Royce, anamiliki Rolls-Royce Phantom VII, yenye thamani ya Dola 450,000.
Pia anamiliki olls-Royce Ghost yenye thamani ya Dola 300,000.
Mbali ya Rolls-Royce pia anamiliki gari aina nyingine kama Mercedes-Benz G63 AMG, yenye thamani ya Dola 145,000.
MJENGO
Licha ya kwamba haijajulikana ametumia kiasi gani kuinunua lakini taarifa zinadai jamaa anamiliki mjengo huko Las Vegas, Marekani anakoishi kwa sasa.
MSAADA KWA JAMII
Ngannou anamiliki taasisi yake mwenyewe iitwayo ‘The Francis Ngannou Foundation’ ambayo huwa inasaidia vijana Cameroon katika nyanja mbalimbali, pia taasisi hiyo imeanzisha Gym mbalimbali Cameroon ambazo ni maalumu kwa ajili ya kuwafua vijana kuwa wapambanaji. Vile vile imekuwa ikitoa misaada kwa vijana kuwawezesha wawe wajasiriamali.
MAISHA BINAFSI
Taarifa zilizopo kwa sasa ni Ngannou yupo kwenye uhusiano wa kimapenzi na Miesha Tate, lakini hakuna taarifa yoyote ikiwa wawili hawa wamevalishana pete au laa.
Baada ya tetesi za muda wawili hao wapo kwenye mahusiano Tate ambaye ana watoto wawili aliozaa na mpenzi wake wa zamani Johnny Nunez, alithibitisha rasmi tetesi baada ya kuweka picha kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akiwa na Ngannou na watoto wake kisha akaandika Ngannou amekuwa mmoja kati ya wanaume wazuri kwa watoto wake.