Prime
Ahadi ya Camara Simba CAF

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Camara amekiri pia kwamba upendo wa mashabiki umempa deni kubwa, hivyo ahadi yake kubwa kwa mashabiki wa Simba ni kuona wanapata furaha kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Berkane na mechi zote muhimu zinazokuja mbele yao.
KIPA namba moja wa Simba, Mousa Camara amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo jambo moja kuelekea mechi ya fainali ya Shirikisho dhidi ya RS Berkane.
Akizungumza na Mwanaspoti, Camara amekiri pia kwamba upendo wa mashabiki umempa deni kubwa, hivyo ahadi yake kubwa kwa mashabiki wa Simba ni kuona wanapata furaha kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Berkane na mechi zote muhimu zinazokuja mbele yao.
Amesema kila akiwaza anaiona Simba inakwenda kuchukua ubingwa wa Shirikisho licha ya kukutana na timu ngumu na yenye uzoefu.
“Mechi ya ugenini ndio ngumu kwetu, lakini kwa hesabu za kocha tunaamini tutacheza salama na kuja kumaliza kazi hapa nyumbani, kuhusu ishu ya ‘clean sheets’ sio suala ninalozingatia sana. Ninachopambana ni kutimiza majumu yangu ili timu isipoteze,” alisema.
Camara maarufu kama Spider ameingia kwenye dhidi ya kipa wa kikosi cha RS Berkane watakaokutana nao katika mechi ya fainali ya michuano hiyo itakayopigwa kati ya Mei 17 na 25 ili kusaka bingwa mpya kwa msimu huu wa 2024-2025.
Kipa huyo aliyetua Simba msimu huu akitokea AC Horoya ya Guinea anakotokea, amekuwa nguzo imara kwa timu hiyo iliyoandika historia ya kucheza fainali hizo za Shirikisho kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipoasisiwa 2004. Hizo ni fainali za pili Simba kwani ilishatinga zile za Kombe la CAF 1993, michuano iliyokuja kuunganishwa na Kombe la Washindi Afrika na kuzaliwa Shirikisho.

Tangu atue kuchukua nafasi ya Mmorocco Ayoub Lakred aliyeumia, Camara amekuwa nguzo akiwafunika makipa aliowakuta akiwamo Aishi Manula, Hussein Abel na Ally Salim akiwa kinara wa clean sheet katika Ligi Kuu Bara anazo 15 mbele ya Djigui Diarra wa Yanga mwenye 14 na Patrick Munthari wa Mashujaa akiwa na 12.
Kuingia kwake kikosi cha kwanza na kucheza mechi 20 mfululizo za Ligi Kuu kabla ya kuumia, huku kimataifa akifunika imemfanya Camara kuwa tegemo la Simba inayowania taji la kwanza la Afrika tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo 1936.
Kitendo cha kupangua mkwaju mmoja wa penalti kwenye mechi ya makundi iliyopigwa Novemba 27, mwaka jana dhidi ya Bravos ya Angola, kisha kuokoa mbili katika robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri, imeonyesha uwezo mkubwa wa kipa huyo na sasa ana vita dhidi ya kipa wa Berkane, Munir Mohamedi anayeenda kukutana naye katika mechi hizo mbili za fainali.
Makipa hao ndio wanaoongoza kwa clean sheet katika michuano ya Shirikisho, Camara akiwa nafasi ya pili kwa kuwa na sita wakati mpinzani wake akiwa nazo saba na yeyote atakayeibeba timu atafunika zaidi msimu huu.
Rekodi zinaonyesha Camara mbali na clean sheet sita za hatua ya makundi hadi nusu fainali za CAF, pia katika mechi 10 akitumia dakika 900 amefanya sevu 22 za hatari akiokoa penalti mbili na kufungwa mabao saba.

Kwa upande wa Munir ni kinara wa clean sheet akiwa nazo saba kupitia mechi tisa akiruhusu mabao mawili katika dakika 810 akiokoa michomo kadhaa ya hatari.
Hivyo, Camara kwa sasa ana dakika 180 za mechi mbili za fainali ili kumfunika Munir kwa kuipa timu anayoitumikia ubingwa na kuwa Kipa Bora wa michuano ya msimu huu.
Simba itaanza karata ya kuwania ubingwa Mei 17 kwa kucheza na Berkane, huko Morocco kabla ya kurudiana nao huku kombe likiwa uwanjani kama ilivyokuwa katika michuano ya CAF 1993 siku ya Mei 25 na mshindi wa jumla atabeba taji lililotemwa na Zamalek ya Misri iliyotolewa raobo fainali.
Kifupi Camara anaingia kwenye vita ya kuwania kipa bora dhidi ya Mohamedi na hilo litaamuliwa kwenye mechi hiyo ya mwisho wa fainali inayotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
REKODI LIGI KUU
Ukiwa msimu wake wa kwanza kuitumikia Simba, Camara ameonyesha ukomavu mkubwa na kuisaidia Simba kwenye mechi mbalimbali za Ligi Kuu akiruhusu mabao nane kwenye mechi 20 alizocheza.
Kipa huyo amedaka mechi 20 akiwa na clean sheet 15, karuhusu mabao katika michezo mitano dhidi ya Coastal Union (mabao 2-2, Oktoba 4, 2024), dhidi ya Yanga (bao moja Oktoba 19,2024), Fountain Gate (bao 1-1, Februari 6, 2025), dhidi ya Azam (mabao 2-2 Februari 24,2024) na dhidi ya Kagera Sugar na Simba ikishinda 5-2, mchezo huo uliopigwa Desemba 21, 2024.

Camara amecheza dakika 1,800 na kwa ufupi ndiye kipa aliyecheza mechi nyingi Simba.
Ubora alioonyesha umefanya makipa kikosini hapo kama Ali Salim kudaka mechi mbili za ligi baada ya Camara kuumia, huku Hussein Abel akidaka Kombe la Shirikisho FA wakati Manula akiendelea kusugua benchi.