Yamal, Raphinha wameishika dunia

Muktasari:
- Staa huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 17, rekodi alizoweka zimezipiku zile ambazo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo waliwahi kuziweka kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA ilitoa sare ya mabao 3-3 juzi kwenye uwanja wao wa nyumbani ilipokutana na Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya hali iliyoweka ugumu kuelekea mchezo wa marudiano, lakini mastaa wake Lamine Yamal na Raphinha walikuwa na kitu kingine cha kufurahia.
Yamal alikuwa katika ubora wake wa hali ya juu, akifunga bao moja lililoisaidia Barca kurudi mchezoni ambalo kwake lilikuwa ni la 22 tangu aanze kuichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 15, miezi tisa na siku 16. Ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, na hakuwa na mpinzani aliyeweza kumdhibiti kwa muda wote wa mchezo dhidi ya Inter.
Lamine hapo alikuwa akitimiza mechi yake ya 100 akiwa na Barca ambapo kiujumla mbali ya mabao 22, pia ametoa asisti 33.
Staa huyu ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 17, rekodi alizoweka zimezipiku zile ambazo Lionel Messi na Cristiano Ronaldo waliwahi kuziweka kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Messi, gwiji wa Argentina, alicheza mechi tisa tu na kufunga bao moja kwa Barca kabla ya kutimiza miaka 18.
Hakufikia kiwango cha kuwa mchezaji wa kutegemewa sana hata mara baada ya kufikisha miaka 18 na alianza kung'ara zaidi alipokuwa na miaka 19.
Kwa upande wa Ronaldo akiwa na miaka 17, alikuwa bado anapambana kuingia kikosi cha kwanza cha Sporting Lisbon na alikuwa amecheza mechi 19 tu, akifunga mabao matano na kutoa pasi nne za mabao.
Alihamia Manchester United mwaka mmoja baadaye akiwa na miaka 18 baada ya kumvutia Sir Alex Ferguson katika mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya.
Akiwa na umri huo wa miaka 17, Yamal pia ameisaidia Hispania kutwaa ubingwa wa Euro 2024 na sasa yuko mbioni kumaliza msimu huu kwa mataji matatu akiwa na Barcelona.
Raphinha, kwa upande wake alitoa pasi ya bao katika mchezo huo ambayo ilikuwa imekamilisha kuhusika kwake katika mabao 20 ya Ligi ya Mabingwa msimu huu akiipuiku rekodi ya Messi ya mwaka 2021 ambapo aliwahi kuhusika katika mabao 19 kiujumla katika msimu mmoja wa michuano hiyo.
Ni Cristiano Ronaldo pekee aliyewahi kuhusika kwenye mabao mengi zaidi (21) katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo yanaweza kufikiwa na Raphinha kwani bado anaendelea kucheza na anatarajiwa kuanza katika kikosi kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ugenini Italia.
Kwa ujumla, nyota huyo wa zamani wa Ligi Kuu England amehusika katika mabao 51 katika mechi 51 za michuano yote alizochezea Barca msimu huu, akifunga mabao 30 na kutoa asisti 21 za mabao.
Amechangia kwa kiwango kikubwa kwenye mbio za ubingwa za Barca.