Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ronaldinho, Kaka kukipiga Zanzibar

Muktasari:

  • Tukio hili la kihistoria linakuja kama sehemu ya maadhimisho ya ‘Brazil Week’, wiki nzima ya sherehe na burudani ambazo zitasherehekea utamaduni wa Kibrazil kwa namna tofauti, huku zikitumika kama jukwaa la kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.

MASHABIKI wa soka Zanzibar na Afrika kwa ujumla, wakae tayari kushuhudia tukio la Kihistoria litakalofanyika Julai 27, 2025, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kupitia “The Match of the Legends” inayowaleta mastaa wakongwe wa Brazil wakiongozwa na Ronaldinho Gaúcho, Kaká na Julio Cesar.

Tukio hili la kihistoria linakuja kama sehemu ya maadhimisho ya ‘Brazil Week’, wiki nzima ya sherehe na burudani ambazo zitasherehekea utamaduni wa Kibrazil kwa namna tofauti, huku zikitumika kama jukwaa la kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.

Kwa mujibu wa waandaaji wa tukio hilo, mastaa hao wa Brazil wataambatana na vyombo vya habari vya kimataifa kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii Zanzibar, kama vile Fukwe za Nungwi, Mji Mkongwe na maeneo ya urithi wa kitamaduni ili kuonyesha uzuri wa visiwa hivyo kwa dunia nzima.

“Mbali na mechi yenyewe (dhidi ya mastaa wa Zanzibar), kutakuwa na matembezi ya utalii kwa mastaa hao wa soka na wageni wengine, jambo litakalosaidia kutangaza vivutio vya Zanzibar kwa hadhira ya kimataifa,” ilisomeka sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari.

Kwa upande mwingine, Mnazi Mmoja Grounds itageuka kuwa jukwaa la burudani na utamaduni ambapo kutakuwa na tamasha la ‘Brazilian Carnival’, ladha ya vyakula vya Kibrazil, pamoja na BBQ ya kuvunja mbavu kwa wakazi na watalii.

Aidha, kutakuwa na ‘Fan Village’ karibu na Uwanja wa New Amaan Complex, ambapo bidhaa za kienyeji na za kimataifa zitaonyeshwa, ikiwemo kazi za mikono za Zanzibar, chakula cha asili na burudani nyingine jambo litakalowapa wageni nafasi ya kuonja utamaduni wa Wazanzibari kwa ukaribu zaidi.

Usiku wa Gala utakaoandaliwa kwa heshima ya mastaa wa Brazil, ukihudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, utaweka alama ya juu ya ukarimu wa Wazanzibari na kuonyesha uwezo wa visiwa hivyo kupokea wageni mashuhuri wa kimataifa.

Mwishoni mwa tukio, kutakuwa na mkutano wa waandishi wa habari wa kuwaaga wageni, sambamba na uzinduzi wa ushirikiano wa kuanzisha akademi kati ya Brazil na Zanzibar jambo litakalokuwa urithi wa kudumu kwa maendeleo ya michezo na utalii.

Wizara ya Utalii na Urithi ya Zanzibar tayari imeridhia rasmi tukio hilo, ikilitambua kama jukwaa mahsusi la kukuza utalii wa michezo, kuimarisha utambulisho wa kitamaduni wa Zanzibar, na kuitangaza visiwa hivyo kama kituo bora cha wageni duniani.