Newcastle Utd, Nottingham Forest zajitosa kwa Nunez

Muktasari:
- Licha ya timu hizo za England kuonyesha nia ya kumsajili, uwezekano wa Liverpool kukubali kumuuzia ni mdogo kwa sababu ina mpango wa kumuuza kwa timu za Saudi Arabia ambazo zinataka kuweka zaidi ya Euro 80 milioni mezani ili kumpata wakati Newcastle na Nottingham zinadaiwa kutaka kutuma ofa ya kumsajili kwa mkopo.
NOTTINGHAM Forest na Newcastle United zote zinapigana vikumbo kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez, 25, ambaye anadaiwa kuwekwa sokoni kuelekea dirisha lijalo. Inaelezwa Liverpool ipo tayari kumwachia Nunez kwa sababu kocha wa timu hiyo, Arne Slot haridhishwi naye tangu kuanza kwa msimu huu licha ya mchango aliouonyesha.
Licha ya timu hizo za England kuonyesha nia ya kumsajili, uwezekano wa Liverpool kukubali kumuuzia ni mdogo kwa sababu ina mpango wa kumuuza kwa timu za Saudi Arabia ambazo zinataka kuweka zaidi ya Euro 80 milioni mezani ili kumpata wakati Newcastle na Nottingham zinadaiwa kutaka kutuma ofa ya kumsajili kwa mkopo.
Mkataba wa Nunez unatarajiwa kumalizika 2028 na msimu huu amecheza mechi 40 za michuano yote, amefunga mabao saba na asisti saba.
Alexander Isak
MCHAKATO wa Liverpool kutaka kumsajili mshambuliaji wa Newcastle United na timu ya taifa ya Sweden, Alexander Isak, mwenye umri wa miaka 25, unaendelea kupamba moto na kocha Arne Slot anamuona staa huyo kama mbadala sahihi wa Mohamed Salah ambaye anatarajiwa kuondoka mwisho wa msimu mara baada ya mkataba wake kumalizika 2028. Isak amekuwa moto katika kikosi cha Newcastle.
Bart Verbruggen
BAYERN Munich inajiandaa kuwasilisha ofa ya Pauni 60 milioni kwenda Brighton kwa ajili ya kuipata saini ya kipa wa timu hiyo na timu ya taifa ya Uholanzi, Bart Verbruggen, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Bart ambaye ni kipa namba moja wa Brighton anahitajika na Bayern kuchukua mikoba ya Manuel Neuer ambaye umri umeshamtupa mkono na amekuwa akisumbuliwa na majeraha kila mara.
Francisco Trincao
KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim amewaomba mabosi wa timu hiyo wahakikishe wanamsajili winga wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Ureno, Francisco Trincao, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Trincao ni miongoni mwa mastaa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Sporting na msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote.
Joan Garcia
MANCHESTER United, Arsenal, Paris St-Germain, Bayer Leverkusen, Real Madrid na Atletico Madrid zote zinapambana ili kumsajili kipa wa Espanyol, Joan Garcia, 23 dirisha lijalo la usajili huko Ulaya. Garcia ambaye aliwahi kuchezea timu ya taifa ya vijana ya Hispania chini ya miaka 21, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.
Noni Madueke
ASTON Villa inaongoza kuiwania saini ya mshambuliaji wa Chelsea na England, Noni Madueke mwenye umri wa miaka 23, ambaye alitaka kuondoka tangu dirisha lililopita kwa ajili ya kujiunga na timu ambayo itampa nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Madueke ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2030.
Xavi Simons
NYOTA wa RB Leipzig ambaye msimu uliopita alizikataa timu kibao na kukubali kusaini mkataba wa kuendelea kusalia timu hiyo aliyoichezea kwa mkopo, Xavi Simons, 21, yupo katika rada za Manchester United inayohitaji kumsajili dirisha lijalo. Kiungo huyo wa PSG mkataba wake unamalizika 2027.
Benjamin Sesko
ARSENAL, Manchester United, AC Milan na Bayern Munich zote zipo katika vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa RB Leipzig na timu ya taifa ya Slovenia, Benjamin Sesko, 21, katika dirisha lijalo. Licha ya ofa nzuri zilizotolewa na timu zote, Sesko anatamani zaidi kutua England kucheza EPL badala ya sehemu nyingine kwa sababu ni ndoto yake.