Neville: Waje sita Manchester United

Muktasari:
- Man United inatarajia kufanya usajili mkubwa wa kuboresha kikosi kwenye dirisha lijalo baada ya kuwa na msimu mbaya kwenye Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa zamani, Gary Neville amefichua mastaa sita ambao Manchester United inapaswa kufanya kila inaloliweza kunasa saini zao kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kukifanya kikosi hicho kuwa moto wa kuotea mbali.
Man United inatarajia kufanya usajili mkubwa wa kuboresha kikosi kwenye dirisha lijalo baada ya kuwa na msimu mbaya kwenye Ligi Kuu England.
Staa wa Wolves, Matheus Cunha anatarajia kuwa usajili wa kwanza wa Man United kwenye dirisha hilo baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kuwa tayari kulipa Pauni 62.5 milioni kama ilivyoelezwa kwenye mkataba wake kwamba ndiyo bei anayouzwa mwisho wa msimu.
Hata hivyo, gwiji wa Old Trafford, Neville amewaambia mabosi wa klabu hiyo aliyowahi kuichezea kwamba inahitaji wachezaji wanaoanzia sita ili kukijenga upya kikosi cha Ruben Amorim, aliposema: “Wanapaswa kufanya sasa ni kutengeneza uimara. Kumekuwa hakuna uimara nje ya uwanja kwenye upande wa uongozi na hakuna uimara pia ndani ya uwanja kutokana na mabadiliko ya kocha na mabadiliko ya kikosi. Hivyo vitu vinapaswa kumalizwa. Inahitaji kufanya usajili mkubwa dirisha la kiangazi. Wachezaji watano au sita wanaweza kubadili mwelekeo wa timu na namna kocha anavyotaka timu yake icheze.
“Inahitaji walau mastraika wawili, kiungo wa kati, wing-back wawili na beki mwingine wa kati. Kwa kifupi inahitaji walau wachezaji sita. Ruben amekuwa vizuri kwenye kutambua wachezaji ambao anataka waondoke kwenye klabu. Klabu ya klabu ya sasa ni kupata wabadala anaowataka na kuwahitaji kwenye timu yake.”€
Man United imeshinda mechi sita tu kati ya 26 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England chini ya kocha Amorim, lakini ilikuwa haijapoteza mechi yoyote ya Europa League, ambapo usiku wa Jumatano dhidi ya Tottenham Hotspur huko Bilbao, Hispania.
Staa mwingine wa zamani wa Man United, David Beckham anaamini kocha Amorim anahitaji kusapotiwa kwa kuletewa wachezaji makini kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kuliko kufunguliwa mlango wa kutokea.
Beckham alisema: “Ruben anapaswa kupewa sapoti kama kocha ili kuwa na uwezo wa kuingiza falsafa zake. Anajaribu kufanya hivyo, lakini naamini atakapopata wachezaji wake basi kitaonekana kitu tofauti.”