Nathan Ake kutimkia Barcelona, Guardiola atajwa
Muktasari:
- Mustakabali wa Guardiola ndani ya Man City bado haujulikani, huku ripoti kadhaa zikidai kuwa msimu huu huenda ukawa wa mwisho kwake kuinoa klabu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola anaripotiwa kuwa tayari kuisaidia klabu yake ya zamani, Barcelona, kwa kuidhinisha uhamisho wa nyota wa City, Nathan Ake kwenda kwa wababe hao.
Mustakabali wa Guardiola ndani ya Man City bado haujulikani, huku ripoti kadhaa zikidai kuwa msimu huu huenda ukawa wa mwisho kwake kuinoa klabu hiyo.
Majina ya makocha kama Enzo Maresca na Vincent Kompany yanatajwa miongoni mwa wanaoweza kuchukua nafasi ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 iwapo ataamua kuondoka Etihad mwisho wa msimu.
Hata hivyo, Pep anaonekana kutaka kuiacha City katika hali bora zaidi, kutokana na usajili wa mastaa wakubwa anaoendelea kuufanya ikiwamo Tijjani Reijnders, Rayan Cherki na Gianluigi Donnarumma waliosajiliwa katika dirisha la usajili lililopita.
Vilevile, akawaondoa baadhi ya wachezaji walioonekana kuwa umri unawatupa mkono kama Kyle Walker, Ederson na Ilkay Gundogan.
Ake ambaye amecheza mechi 13 tu msimu huu, anaripotiwa kuwa chaguo kwa Barcelona kutokana na changamoto zao katika safu ya ulinzi.
Kikosi cha Hansi Flick kwa sasa hakina beki wa kati baada ya Ronald Araujo, kupewa ruhusa ya mapumziko kutokana na matatizo ya afya ya akili.
Vilevile, beki wa zamani wa Chelsea, Andreas Christensen anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne kutokana na jeraha la sehemu ya ligamenti ya goti, hali inayomwacha kocha Flick na Pau Cubarsi mwenye umri wa miaka 18 kama beki wa kati pekee aliyepo.
Katika mechi za hivi karibuni, beki wa kushoto Gerard Martin ametumika kama beki wa kati na Barca inaamini uzoefu wa Ake aliyeshinda mataji manne ya Ligi Kuu England na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya mmoja akiwa Manchester City utasaidia sana katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Hispania Mundo Deportivo, Ake ni miongoni mwa machaguo manne ya mabeki ambao Barca inawaangalia akiwamo nahodha wa Benfica, Nicolas Otamendi, beki wa Inter, Stefan de Vrij na beki wa Bournemouth, Marcos Senesi.
Ake ana mkataba na Manchester City hadi Juni 2027 na anaripotiwa kutofurahishwa na hali ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza kwa sasa na mtu pekee anayeweza kutoa ruhusa ya kuuzwa kwake ni Guardiola.