Namba moja NBA yenye kazi nzito

Muktasari:
- Kwa wachezaji ambao wanacheza ligi na waliwahi kuchaguliwa kama namba moja kwenye drafti ni LeBron, Kyrie Irving na Anthony Davis walio tayari na taji, lakini wapo ambao wanaliona tu kwa wenzao na orodha inawatazama zaidi wale ambao wana kazi kubwa ya kufanya ili kulibeba.
WAKATI supastaa LeBron James akiwa kinara wa mafanikio katika orodha ya wachezaji waliowahi kuchaguliwa kama namba moja kwenye drafti za Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) kwa wanaocheza hivi sasa, lakini wapo wachezaji ambao bado wana kazi ya kufanya ili kutwaa taji la NBA.
Kwa wachezaji ambao wanacheza ligi na waliwahi kuchaguliwa kama namba moja kwenye drafti ni LeBron, Kyrie Irving na Anthony Davis walio tayari na taji, lakini wapo ambao wanaliona tu kwa wenzao na orodha inawatazama zaidi wale ambao wana kazi kubwa ya kufanya ili kulibeba.
BEN SIMMONS
Mwamba yupo kwenye wakati mgumu zaidi wa hata kucheza katika timu aliyopo kwa sasa ya Brooklyn Nets ambaye alikuwa chaguo namba moja kwenye drafti la 2016.
Simmons ambaye mambo hayamwendei vizuri kwenye NBA kiasi cha wengi kushangaa aliwezaje kuwa namba moja kwa kutokuwa na mwendelezo wowote wa ubora kwenye ligi.
Ajabu ni kwamba 2016 Simmons alichaguliwa namba moja na Philadelphia 7ers na hana wakati mzuri kwenye ligi tofauti na aliochaguliwa nao siku hiyo kama Jaylen Brown (Celtics) aliyekuwa namba mbili na Jamal Murray (Nuggets) aliyekuwa chaguo namba saba na tayari wameshabeba taji.
DEANDRE AYTON
Mwaka 2018, miaka miwili baada ya Simmons kuchaguliwa na Sixers ilikuwa ni zamu ya nyota DeAndre Ayton kuwa kinara katika drafti la mwaka huo akichaguliwa na Phoenix Suns alipokwenda kutengeneza timu ya ushindani kutoka kuwa timu ya kawaida hadi kucheza fainali 2021.
Ayton kama ilivyo kwa Simmons naye hajawahi kubeba ubingwa, lakini haonekani kuwa kwenye ubora wa kutisha kwa misimu ijayo kutokana na kupoteana akiwa Suns na sasa ana kazi ya kufanya ili kurejesha makali aliyowekewa kwa kuwa namba moja kwenye drafti 2018.
ZION WILLIAMSON
Katika orodha ya wachezaji waliowahi kuchaguliwa namba moja kwenye drafti, moja ya jina kubwa lililotikisa na kuwa gumzo ni la Zion Williamson aliyechaguliwa na New Orleans Pelicans na kiasi kikubwa ametumika kuirudishia makali baada ya kuondokewa na supastaa Anthony Davis aliyehamia Los Angeles Lakers.
Williamson tangu aanze kucheza NBA 2019, ameshindwa kuwa na mwendelezo mzuri kutokana na kukumbwa na majeraha ya mara kwa mara ambayo yametibua jitihada zake za kutisha NBA na kubaki kuwa mchezaji asiye tishio hadi sasa tofauti na kama angekuwa anacheza msimu mzima akiwa bora.
ANTHONY EDWARDS
Hili ni jina lingine kubwa NBA ambalo linadaiwa mafanikio baada ya kuingia kwenye ligi 2020 kama chaguo namba moja akichaguliwa na Minnesota Timberwolves.
Ni ukweli usiojificha kwamba, uwepo wake ndani ya timu hiyo uliongeza sababu za Timberwolves kuwa na makali msimu uliopita kiasi cha kuwavua taji Denver Nuggets, lakini bado haitoshi hadi aiongoze timu hiyo kubeba ubingwa msimu ujao.
VICTOR WEMBANYAMA
Mchezaji huyo amekuwa na msimu wa kwanza bora kwake binafsi, lakini haukuwa bora kwa timu nzima ya San Antonio Spurs ambayo ilishindwa kucheza hatua ya mtoano (playoffs) achilia mbali mechi za mchujo (play-in). Wembanyama ambaye pia aliupiga mwingi kwenye michuano ya Olimpiki akiwa na Taifa mwenyeji, Ufaransa, ana kazi ya kufanya msimu ujao ili kuthibitisha ubora wake.