Baada ya Simba kukosa ubingwa CAF, Manula atoa kauli nzito

Muktasari:
- Simba imelikosa taji hilo baada ya kupoteza mchezo wa fainali kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane, kufuatia kuanza kufungwa ugenini 2-0, kisha sare ya 1-1 nyumbani timu hizo ziliporudiana Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
SIKU chache baada ya Simba SC kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, golikipa wa timu hiyo, Aishi Manula, ameibuka na kutoa kauli nzito kuhusu kilichotokea.
Simba imelikosa taji hilo baada ya kupoteza mchezo wa fainali kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane, kufuatia kuanza kufungwa ugenini 2-0, kisha sare ya 1-1 nyumbani timu hizo ziliporudiana Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Manula ambaye msimu huu hajacheza mechi yoyote ya kimashindano ndani ya kikosi cha Simba, amesema katika safari ndefu ya kuwania ubingwa huo, mwisho wa siku wameshindwa kufikia malengo huku akiamini wakati ujao utakuwa bora zaidi.
"Ndio ilikuwa ni safari ndefu. Safari ambayo wanajeshi tuliweza kupigana pamoja kwa hali na mali kuhakikisha tunafikia malengo, lakini kwa bahati mbaya hatukufikia malengo yale ambayo tulikuwa tumeyapata baada ya kufika fainali," amesema Manula ambaye mechi ya mwisho kucheza ndani ya Simba ilikuwa ya kirafiki dhidi ya Al Hilal iliyochezwa Agosti 31, 2024 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo alitumika dakika 45 za kwanza, akampisha Hussein Abel.
Ukiweka kando mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal, upande wa mashindano mara ya mwisho Manula alidaka katika Ligi Kuu Bara Machi 6, 2024 wakati Simba ikipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu ilikuwa safari ndefu na siku kadhaa tulikuwa na matumaini makubwa ya kuhakikisha tunapata medali ya CAF ya ubingwa, lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu atatujalia zaidi tuweze kufika pakubwa," amesema Manula kupitia video aliyoposti leo Mei 27, 2025 kwenye akaunti yake ya Instagram.
Manula ambaye anamaliza mkataba mwishoni wa msimu huu, mustakabali wake ndani ya kikosi cha Simba bado umebaki kuwa kitendawili huku ripoti zikibainisha kwamba anaondoka akihusishwa kutua Yanga au Azam.
Kipa huyo aliyejiunga na Simba msimu wa 2017-2018 akitokea Azam, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa, Ayoub Lakred kutokea FAR Rabat ya Morocco msimu uliopita, huku ujio wa Moussa Camara kutoka AC Horoya ya Guinea msimu huu umeongeza balaa zaidi kwake kufuatia Camara kucheza mechi zote 14 za Kombe la Shirikisho Afrika na 24 za Ligi Kuu Bara kati ya 26 akimuachia Ally Salim akidaka mbili.