Prime
Kilicho iponza Simba CAFCC hiki hapa

Muktasari:
- Matokeo hayo yamezima matumaini ya Simba ambayo ilikuwa ikiona ina uwezo wa kubeba ubingwa huo licha ya kwamba mwanzo wa msimu uongozi na Kocha Mkuu, Fadlu Davids kusema wanajenga timu.
SIMBA imepoteza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.
Matokeo hayo yamezima matumaini ya Simba ambayo ilikuwa ikiona ina uwezo wa kubeba ubingwa huo licha ya kwamba mwanzo wa msimu uongozi na Kocha Mkuu, Fadlu Davids kusema wanajenga timu.
Wakati Simba ina deni la mabao 2-0 kutokana na kichapo cha mechi ya kwanza ugenini mjini Berkane Morocco, kisha nyumbani ilianza vizuri kwa kufunga bao dakika ya 17 kupitia Joshua Mutale, lakini dakika ya 90+3, ikaruhusu nyavu kutikiswa mfungaji akiwa Soumaila Sidibe. Mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1 na kufanya matokeo ya jumla Berkane kushinda 3-1.
Matokeo hayo ya kushindwa kutwaa taji kwa mara nyingine baada ya kukwama pia mwaka 1993 ilipopoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, lakini kuna mambo matano yaliyoichangia timu hiyo kukwama katika fainali ya mwaka huu.
Hii ni fainali ya tatu kwa klabu za Tanzania kushindwa kubeba taji la Afrika baada ya Yanga msimu wa 2022-2023 kulikosa kiduchu kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini, kwani matokeo ya jumla dhidi ya USM Alger ya Algeria yalikuwa sare ya 2-2, ikipoteza nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0.
Kupoteza huko kwa juzi kwa Simba kumechangiwa zaidi na mambo matano makubwa ambayo ni siasa, kuhama uwanja wa Benjamin Mkapa, ukubwa wa RS Berkane, mbinu zilizotumika mechi ya kwanza na matukio ya refa wa pambano hilo, Dahane Beida wa Mauritania katika uamuzi wake.

SIASA
Wakati Simba inajiandaa na mchezo wa fainali, zilitoka taarifa kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa haupo tayari, hivyo Simba inatakiwa kutafuta uwanja mwingine.
Katika hilo, yalitoka matamko mengi yakihusisha viongozi wa kisiasa hapa nchini akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa na Naibu Waziri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ambapo kila mmoja alikuwa anasisitiza uwanja upo tayari na mechi itachezwa hapo.
Hali hiyo iliibua matumaini kwa Simba kwamba itamaliza kazi nyumbani uwanjani hapo huku zoezi la uuzaji tiketi likianza kwa kasi hali iliyofanya mashabiki wa timu hiyo kuwa na imani kubwa katika kuisapoti timu kwa wingi.
Viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), walipokuja kufanya ukaguzi, wakasema uwanja haupo tayari na mechi itachezwa New Amaan Complex, Zanzibar.
Tamko la mwisho kutoka CAF, likaharibu kila kitu, uuzaji mpya wa tiketi ukaanza ambapo baadhi ya mashabiki wakashindwa kusafiri kwenda Zanzibar kushuhudia mchezo huo kwenye uwanja wenye uwezo wa kuingiza watamazaji 15,000. Kumbuka Uwanja wa Benjamin Mkapa mashabiki wanaoingia ni 60,000.

KUHAMA UWANJA
Kitendo cha Simba kuhama uwanja kutoka Benjamin Mkapa hadi New Amaan Complex, kwa kiasi fulani iliiondolea timu hiyo hali ya kujiamini baada ya kutengeneza ngome yao imara uwanjani hapo.
Simba inapokuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, imekuwa na matokeo mazuri kwenye michuano ya kimataifa kiasi cha wapinzani kuhofia kucheza hapo.
Hata kitendo cha Berkane kuthibitisha mechi itachezwa Zanzibar, ilionekana kuwa nafuu kwao kiasi cha kufurahia.
“Kisaikolojia tulikuwa tunajua kuwa kwa Tanzania ukicheza kwa Mkapa unapoteza na tunafahamu hilo, lakini tumefurahi kwasababu hatuchezi kwa mkapa,”€ alisema kiungo wa RS Berkane, Mamadou Camara wakati akizungumza na waandishi wa habari siku moja kabla ya mchezo huo.
Hii ilikuwa mara ya pili Simba kucheza New Amaan Complex msi-mu huu baada ya nusu fainali kuichapa hapo Stellenbosch bao 1-0.
Kw-enye Uwanja wa Benjamin Mk-apa, ilicheza mechi tano, ikishinda zote ikiwemo ile ya robo fainali ilipopindua matokeo mbele ya Al Masry ya Misri kufuatia kufungwa 2-0 ugenini na nyumbani kushinda idadi hiyo ya mabao, ikavuka kwa penalti 4-1.

UKUBWA WA BERKANE
Mbali na yote, daraja walilonalo Berkane na Simba ni vitu viwili tofauti. Wamorocco hao wametumia ukubwa walionao kubeba ubingwa na kuikosesha Simba nafasi ya kuandika rekodi.
Tukizichambua dakika 180 za fainali kwa maana ya mechi ya kwanza na ya pili, RS Berkane ilikuwa na takwimu bora dhidi ya Simba.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa nchini Morocco, RS Berkane iliongoza katika maeneo yote muhimu ikiwemo dhidi ya Simba iliyopiga mashuti tisa pekee huku kukiwa hakuna hata moja lililolenga lango wakati wapinzani wao wakipiga 14, sita yakilenga lango yaliyozaa mabao mawili.
Pia umiliki wa mpira Simba ilikuwa na asilimia 47 dhidi ya 53 za Berkane wakati pasi za Simba zikiwa 358, Berkane ikipiga 381. Kitu pekee ambacho Simba iliongoza kwenye kuotea ikifanya hivyo mara mbili, Berkane ni moja, lakini upande wa kona, Berkane ilipiga saba huku moja ikiitumia kufunga bao la kwanza. Simba ilipiga mbili.
Mechi ya pili, kulikuwa na mabadiliko kidogo lakini bado Simba ilizidiwa eneo la kushambulia, licha ya kupiga mashuti saba, lakini ni moja pekee lililenga lango la wapinzani na kuwa bao.
Berkane iliyopiga mashuti tisa, sita yalilenga lango huku moja likiwa bao, katika ushambuliaji ilionekana kuwa hatari zaidi ya wenyeji wao huku ikiwa na uwezekano wa kufunga zaidi ya bao moja.
Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 60 dhidi ya 40 za Berkane, huku ikipiga pasi 433 wakati Berkane ikiwa nazo 297.
Kona Simba ilipiga sita na Berkane tatu, wakati faulo za Simba ni 20 na Berkane 13, huku Simba ikiwa na kadi moja nyekundu za njano mbili. Berkane kadi za njano nne, haikuwa na nyekundu.
Ukija kimafanikio, Berkane kabla ya mchezo huo ilikuwa na mataji mawili ya Kombe la Shirikisho iliyoshinda 2019-20 na 2021-22, huku msimu uliopita ikipoteza fainali ya michuano hiyo mbele ya Zamalek. Pia ina taji la CAF Super Cup ililoshinda mwaka 2022.

MWAMUZI
Malalamiko makubwa yamekwenda kwa mwamuzi wa kati, Dahane Beida raia wa Mauritania ambapo inadaiwa uamuzi wake katika matukio mengi ilikuwa ni dhidi ya Simba huku akiifaidisha Berkane.
Mwamuzi huyo amekuwa na rekodi mbaya mbele ya timu za Tanzania kwani msimu wa 2022-2023 alikataa bao la Stephane Aziz Ki wakati Yanga ilipocheza dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mwamuzi huyo anakumbukwa kwa tukio hilo la Aprili 5, 2024 lililozua gumzo baada ya shuti la Aziz Ki alilopiga dakika ya 58 dhidi ya Mamelodi Sundowns katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali uliochezwa Afrika Kusini, licha ya mpira kuonekana kudundia ndani baada ya kugonga mwamba wa juu, lakini Beida alikataa sio bao baada ya kwenda kujiridhisha kwenye VAR. Mchezo huo ulimalizika kwa matokeo ya 0-0, Yanga ikapoteza kwa penalti 3-2.
Kabla ya hapo, mwamuzi huyo aliichezesha Simba mechi ya African Football League dhidi ya Al Ahly iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2, Oktoba 20, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, huku akiichezesha Yanga fainali ya mkondo wa pili Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger iliyochezwa Juni 3, 2023 nchini Algeria na Yanga kushinda 1-0.
Katika mchezo wa juzi, mwamuzi huyo alimtoa kiungo wa Simba, Yusuf Kagoma kwa kadi nyekundu baada ya kumuonyesha mbili za njano kwenye matukio tofauti.
Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema: “Mwamuzi ametuumiza sana, mchezo ulikuwa wazi, hii ni fainali na uona kabisa kuna kadi imetoka iliyotufanya tuwe nyuma, kwa hiyo mwamuzi ameharibu fainali, lakini kwa upande wetu tulijiandaa vizuri na mechi tulishaikamata, tulikuwa tunaamini tunaweza kusawazisha na kupata ushindi.”

MBINU ZA KOCHA
Matokeo ya mchezo wa kwanza yalichangia kwa kiasi kikubwa Simba kushindwa kubeba ubingwa kufuatia kufungwa mabao 2-0 ndani ya dakika 15 tangu kuanza kwa mchezo.
Simba ilikwenda katika mchezo huo ikitambua kwamba wapinzani wao ni hatari zaidi kipindi cha kwanza, hivyo iliweka mbinu za kuwazuia, lakini ilijikuta ndani ya kipindi hicho tena dakika 15 za kwanza, ikiruhusu mabao mawili ambayo yalidumu hadi mwisho.
Mbinu alizoanza nazo Kocha wa Simba, Fadlu Davids kwa kiasi kikubwa zilichangia kupoteza mchezo wa kwanza kwani timu haikuwa inajilinda, iliamua kucheza kwa kupishana na wapinzani kosa ambalo liliwagharimu, kabla ya kushtuka kipindi cha pili ambacho kilimalizika bila bao.
Fadlu alikuwa anatambua ubora wa Berkane kwani kabla ya mchezo huo wa kwanza, alinukuliwa akisema: “Kocha wa Berkane (Moine Chabaan) amefanya kazi kubwa tangu alipojiunga nayo kutokea Raja. Ni timu yenye uwezo kimbinu wa kuukabili mchezo na jambo la muhimu kwetu ni namna gani ya kupunguza makali yao.
“Uwanja wao una eneo zuri la kuchezea. Tunajua watakuja na kasi na nguvu kubwa katika dakika 45 za kwanza. Msimu huu timu yangu imeonyesha utayari wa kucheza katika viwanja vyenye ubora tofauti wa eneo la kuchezea.”€
Lakini mbinu za mchezo wa pili kwa kiasi fulani zilimlipa kwani Simba ilihitaji mabao ya mapema, ikaingia kwa kushambulia na kufunga bao moja kipindi cha kwanza ingawa halikutosha huku ikiruhusu dakika za mwisho na matokeo kuwa 1-1.