Refa aliyefungiwa apewa fainali Conference League

Muktasari:
- Refa huyo, Irfan Peljto atakuwa Mbosinia wa kwanza kuchezesha mechi kubwa ya michuano ya Uefa ya ngazi ya klabu wakati fainali hiyo itakapopigwa usiku wa Jumatano.
LONDON, ENGLAND: REFA ambaye alikumbana na adhabu ya kufungiwa mechi sita msimu huu ndiye aliyechaguliwa kuchezesha mechi ya fainali ya Conference League itakayokutanisha Chelsea na Real Betis, Jumatano.
Refa huyo, Irfan Peljto atakuwa Mbosinia wa kwanza kuchezesha mechi kubwa ya michuano ya Uefa ya ngazi ya klabu wakati fainali hiyo itakapopigwa usiku wa Jumatano.
Na Chelsea inajiandaa kuwa timu ya kwanza kushinda michuano yote mitatu mikubwa ya Ulaya endapo kama itafanikiwa kuichapa Real Betis katika mechi hiyo ya kibabe kabisa.
Kwenye kikosi cha Betis kuna wachezaji wengi wenye uzoefu wa Ligi Kuu England kwa maana ya kutambua nguvu ya Chelsea ambao ni Antony, Pablo Fornals na Gio Lo Celso, huku wakinolewa na kocha wa zamani wa Manchester City, Manuel Pellegrini.
Chelsea ya kocha Enzo Maresca itapaswa kuwa kwenye ubora wake mkubwa kwenye mechi hiyo ambayo itachezwa siku chache tangu ilipokamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu England.
Lakini, aliyesimama mbele yao ni refa Peljto, ambaye alichezesha mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Arsenal na Real Madrid, Aprili mwaka huu.
Refa huyo mwenye umri wa miaka 40 anaheshimiwa sana na Uefa akiwahi pia kuchezesha mechi nyingine zisizopungua sita za Ligi ya Mabingwa Ulaya na nne za Europa League.
Hata hivyo, huko kwao Bosnia, Peljto alifungiwa mechi sita baada ya kuboronga kwenye mechi, alipofanya makosa matatu makubwa ikiwamo mawili ya kushindwa kutoa penalti zilizokuwa za wazi kabisa katika mechi ya derby, iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kati ya Zrinjski Mostar na Borac Banja.