Timu vigogo Ulaya zazidi kumiminika kwa Leao

Muktasari:
- Leao ambaye mara kadhaa alidaiwa kuwa katika rada za Real Madrid, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizima 2028. Katika msimu uliopita alicheza mechi 50 za michuano yote na kufunga mabao 12.
CHELSEA, Bayern Munich na Manchester United zimeonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa AC Milan na timu ya taifa ya Ureno, Rafael Leao, 25, dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Leao ambaye mara kadhaa alidaiwa kuwa katika rada za Real Madrid, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizima 2028. Katika msimu uliopita alicheza mechi 50 za michuano yote na kufunga mabao 12.
Mshambuliaji huyo yupo tayari kuondoka ingawa hadi sasa bado hajafanya makubaliano na timu yoyote kati ya zile zinazomtaka.
Mojawapo kati ya kikwazo kikubwa kinachosababisha dili hili lisikamilike kwa haraka ni kiasi cha pesa ambacho AC Milan ambacho ni Pauni 70 milioni inahitaji kama ada ya uhamisho kuwa ni kikubwa, hivyo timu zimeendelea kuzungumza akubali kupunguza.
Tijjani Reijnders
MANCHESTER City imefikia hatua nzuri kwenye harakati za kuwania saini ya kiungo wa AC Milan na Uholanzi, Tijjani Reijnders, 26, kuelekea dirisha lijalo la majira ya kiangazi. AC Milan ipo tayari kumuuza supastaa huyo mwenye umri wa miaka 26, lakini kwa timu itakayokuwa tayari kutoa zaidi ya Pauni 55 milioni kama ada ya uhamisho.
Bryan Mbeumo
MANCHESTER United inaendelea kufanya mazungumzo na wawakilishi wa straika wa Brentford na timu ya taifa ya Cameroon, Bryan Mbeumo, 25, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la kiangazi. Brentford ipo tayari kumuuza ikihitaji kiasi cha Pauni 50 milioni kama ada ya uhamisho. Mkataba wa sasa wa Mbeumo unatarajiwa kumalizika 2026.
Hugo Ekitike
CHELSEA inajaribu kuzungumza na Eintracht Frankfurt ili kuona ikiwa inaweza kuipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo na Ufaransa, Hugo Ekitike, 22, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mbali ya Ekitike, Chelsea pia inahitaji saini ya mshambuliaji wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Sweden, Viktor Gyokeres, 26.
Liam Delap
NEWCASTLE United imekutana na wakala wa mshambuliaji wa Ipswich Town na timu ya taifa ya England, Liam Delap, 22, kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mabosi wa Newcastle wanajaribu kumshawishi Delap kujiunga nao badala ya Chelsea, Manchester United na Everton ambazo pia zinamtaka.
Idrissa Gueye
PARIS FC ambayo imepanada Ligi Kuu Ufaransa msimu ujao, imepanga kumsajili kiungo wa Everton, Idrissa Gueye katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Staa huyo mwenye umri wa miaka 35, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na tayari ameshaonyesha nia ya kutaka kuondoka. Mbali ya ofa ya Paris FC pia nyota huyo wa kimataifa wa Senegal amepokea ofa kutoka Saudi Arabia.
Nelson Semedo
MANCHESTER United inataka kumsajili beki wa kulia wa Wolves na timu ya taifa Ureno, Nelson Semedo, 31, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi ambapo mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika. Semedo ameonyesha nia ya kutaka kuondoka na kujiunga na Mashetani Wekundu kwani licha ya kupewa ofa ya kusaini mkataba, hadi sasa bado hajaikubali.
Jobe Bellingham
MDOGO wake Jude Bellingham aitwaye Jobe Bellingham ambaye anaichezea Sunderland yupo kwenye mazungumzo na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani inayohitaji katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Mbali ha Frankfurt, Jobe pia anawindwa na Borussia Dortmund na RB Leipzig ambazo pia zinahitaji kumsajili katika dirisha lijalo.