Mwisho wa Jurgen Klopp wenye taswira ya Hitler

INASADIKIKA mwaka 1945, ndipo kiongozi wa Chama cha Nazi Party cha Ujerumani, dikteta hatari zaidi kuwahi kutokea duniani, Adolf Hitler alipoteza maisha ikiwa ni saa chache baada ya kufunga ndoa na Mwanamama Eva Braun.
Hadi sasa hakuna taarifa kamili juu ya kifo chake, wengine wanasema alijiua kwa kujipiga risasi yeye na mkewe na wengine wanasema alijiua kwa sumu, wengine wanadai alifariki dunia kutokana na maradhi.
Hata hivyo, alifikia ukomo huu baada ya kuponda maisha kwa zaidi ya miaka 12, akiwa dikteta aliyezisumbua nchi zote Ulaya. Kuanzia vita ya kwanza na ya pili ambayo ndio ilimshinda na kifo chake kikaripotiwa.
Kuna muda aliiteka Dunia ndani ya saa sita na kuamrisha ifanye alichohitaji na ikatii. Naona kuna uhusiano kati ya Wajerumani na tabia hii ya kufeli baada ya mafanikio.
Ninapotazama pale jijini Liverpool, kuna mzee wa Kijerumani, kilio kimekua sehemu kubwa ya maisha yake.
Huyu ni Jurgen Klopp, kocha anayepitia magumu sana msimu huu baada ya kufanya vizuri misimu mitatu iliyopita.
Msimamo wa Ligi Kuu England timu yake inashika nafasi ya nane kwa alama 43, tofauti kabisa na ilivyokua msimu uliopita na aliweka rekodi ya kuifanya Liverpool ishinde taji la Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
Hata hivyo, nini kimemkuta msimu huu? Hakuna mashaka juu ya safu ya ushambuliaji wachezaji tegemeo karibia wote wamekuwa wakicheza eneo hilo kwenye mechi nyingi msimu huu.
Kuna matatizo mengi lakini naomba nianze na hili la Roberto Firminho. Huyu sio mshambualiaji wa kukupa mabao zaidi ya 10 kwa msimu, lakini anafanya timu ipate zaidi ya mabao 10.
Ki vipi? Muda mwingi hucheza katikati ya mabeki wa kati na nyuma ya kiungo namba sita, eneo hilo huwa ni ngumu sana kukabika kwa sababu kiungo anahofia akitoka atakuwa anaruhusu wachezaji wa Liverpool wasogee zaidi na hawa mabeki wa kati watakua wanahofia kumfuata kwa sababu watakuwa wanawapa Salah na Mane nafasi ya kuingia kwenye lango lao.
Kimsingi yeye ndio kiini cha mashambulizi ya Liverpool, mpira unapotoka kwa kipa mtu wa kwanza huwa ni beki wa pembeni ama kati.
Ikiwa wa pembeni mfano Trent huwa anatakiwa kusogea juu zaidi, muda huu beki wa kushoto naye atatakiwa kwenda sawa naye.
Kitendo cha hawa mabeki wa pembeni kusogea juu zaidi husababisha Salah na Mane kuingia ndani na kucheza katikati ya mabeki wa kati na pembeni wa timu pinzani, hii itawafanya mabeki wa pembeni wa Liver wale waliopanda kucheza kwa uhuru kwani mabeki wote wa timu pinzani hawatasogea kwa kuwahofia wao.
Baada ya Trent kupanda na mpira hutakiwa kuangalia alipo Firminho na baada ya mpira kumkuta, Trent na beki mwingine wa pembeni hutakiwa kusogelea zaidi lango la timu pinzani na kufanya idadi yao kuwa ni watano dhidi ya wanne wa timu pinzani. Kazi ya Firminho hapa huwa rahisi nayo ni kupiga pasi mpenyezo (Penetration Pass), katikati ya mabeki wa kati na pembeni wa timu pinzani mahali Salah na Mane wanacheza, wakati huo ukumbuke Trent na beki mwingine wa kushoto Robertson wamesogea juu.
Sasa hawa mabeki wa pembeni wa timu pinzani watakuwa na kazi ya kuwazuia Trent na mwenzake, wakati huo Salah na Mane wataachwa na mabeki wa kati jambo lililowafanya wawe wanapiga au kukokota mpira na kufunga.
Msimu huu Firminho amecheza mechi 27 tu za Ligi Kuu England na nyingi aliingia akitokea benchi na kwa mahesabu hajacheza zaidi ya dakika 400 na ukigawanya unapata jumla amecheza kila mechi kwa dakika 14, jambo ni tofauti na msimu uliopita Liver ilipochukua ubingwa, jamaa alicheza karibia mechi 30 tena kwa dakika zote.
Hivyo kumkosa Firminho kumechangia kushuka kwa kiwango cha Salah na Mane na mwisho mabao yamekua adimu.