Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cheza nao mbali, wamefunga mabao 100 ndani ya umri mdogo

HUKO Ulaya kwa sasa kila kona ni Erling Haaland.

Straika huyo wa kimataifa wa Norway amewatesa makipa ile mbaya na Jumamosi iliyopita, alifunga mara mbili ndani ya dakika 10 dhidi ya Bayern Munich katika mechi ambayo timu yake ya Borussia Dortmund ilichapwa 4-2 kwenye mikikimikiki ya Bundesliga.

Bao lake la pili kwenye mechi hiyo, lilimshuhudia Haaland akifikisha mabao 100 tangu alipoanza soka la kulipwa. Kwenye kikosi cha Dortmund, Haaland amefunga mabao 45 katika mechi 46, wakati alipokuwa RB Salzburg alifunga mabao 29 katika mechi 27. Kabla ya hapo, alikuwa Molde, ambako alifunga mabao 20 katika mechi 50 na amefunga mabao sita katika mechi saba za kimataifa.

Kinachovutia zaidi amefikisha idadi hiyo ya mabao 100 akiwa na umri wa miaka 20 na siku 228. Staa Haaland amefikisha mabao 100 katika mechi chache ukilinganisha na walivyofanya mastaa Kylian Mbappe, Lionel Messi, Zlatan Ibrahimvovic na Cristiano Ronaldo.

Lakini, je ni mchezaji gani aliyefikisha idadi hiyo ya mabao akiwa na umri mdogo zaidi?

Kwa mujibu wa The National News, hii hapa orodha ya mastaa waliofikisha idadi ya mabao 100 wakiwa na umri mdogo, huku Haaland akishika nafasi ya pili.

Neymar alifikisha idadi ya mabao 100 katika siku ya kuzaliwa kwake, alipokuwa anatimiza miaka 20, huku mabao yake hayo alifunga alipokuwa Brazil kwenye kikosi cha Santos.

1) Neymar- miaka 20

Supastaa wa Paris Saint-Germain, Neymar ndiye mchezaji aliyefikisha idadi ya mabao 100 kwenye maisha yake ya mpira akiwa na umri mdogo zaidi. Neymar alifanya hivyo kwenye siku yake ya kuzaliwa alipotimiza umri wa miaka 20, kipindi hicho akitamba na klabu ya Santos ya Brazil. Lakini, kwa upande wa mabao ya klabu, Neymar alifikisha mabao 100 baada ya kucheza mechi 177.

2) Erling Haaland-

miaka 20, siku 228

Haaland ni gumzo la dunia kwa sasa. Straika huyo kinda amekuwa akifunga mabao kama anavyotaka jambo linalomfanya awe kivutio kikubwa kwa timu mbalimbali na kufukuzia saini yake. Haaland anashika namba mbili kwa sasa kwa wachezaji waliofikisha idadi ya mabao 100 wakiwa na umri mdogo baada ya mkali huyo wa zamani wa Molde na RB Salzburg kufunga akiwa na umri wa miaka 20 na siku 228.

3) Kylian Mbappe -

miaka 20, siku 356

Staa, Kylian Mbappe tayari ana medali ya ubingwa wa Kombe la Dunia alilobeba akiwa na kikosi cha Ufaransa mwaka 2018 huko Russia. Fowadi huyo hakika ni moto wa kuotea mbali na makipa wanayekabiliana naye wamekuwa wakiteseka sana. Huduma yake ya klabu kwa sasa anaitoa kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain. Mbappe ni mmoja wa mastaa waliofikisha mabao 100 akiwa na umri mdogo, alifanya hivyo akiwa na miaka 20 na siku 356.

4) Romelu Lukaku -

miaka 22, siku 138

Kwenye Ligi Kuu England, straika Romelu Lukaku amezichezea Chelsea, West Brom, Everton na Manchester United. Kwa sasa mkali huyo wa Kibelgiji anakipiga katika kikosi cha Inter Milan na amekuwa moto kwelikweli kwenye kutupia mipira nyavuni. Staa Lukaku ameanza kuonyesha makali ya kufunga tangu alipokuwa na umri mdogo, ambapo mabao 100 alifikisha akiwa na umri wa miaka 22 na siku 138.

5) Sergio Aguero -

miaka 22, siku 147

Kwa kuzingatia mabao ya ngazi ya klabu pekee, straika wa Kiargentina, Sergio Aguero alifikisha mabao 100 baada ya kucheza mechi 158. Lakini, kwa mabao yote ya tangu alipoanza soka la kulipwa, Aguero alifikisha idadi ya mabao 100 akiwa na umri mdogo sana, miaka 22 na siku 147 na hivyo kuwa kwenye orodha ya wakali walionyesha maajabu ya kutesa makipa wa timu pinzani tangu alipokuwa mdogo. Mkataba wake Man City utakwisha mwaka huu.

6) Lionel Messi -

miaka 22, siku 206

Supastaa, Lionel Messi tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa ametamba kwenye timu moja tu, Barcelona. Mkataba wake kwenye timu hiyo utamalizika mwisho wa msimu na kumekuwa na wasiwasi kwamba huenda akaachana na timu hiyo mwisho wa msimu huku Manchester City na PSG zikifukuzia saini yake. Kuhusu kufunga Messi hajawahi kuwa na shida, ambapo mabao 100 alifikisha akiwa na umri wa miaka 22 na siku 206.

7) Wayne Rooney -

miaka 23, siku 37

Staa wa England, Wayne Rooney tangu akiwa na umri mdogo alikuwa akipiga mabao makali tu huko Everton kabla ya Manchester United kutumia mkwanja mrefu kunasa huduma yake. Mkali huyo, ambaye kwa sasa ni kocha wa Derby, alikwenda Old Trafford na kuendeleza moto wake wa kufunga mabao na hivyo kumfanya afikisha mabao 100 akiwa na umri mdogo sana, alipofanya hivyo alipokuwa na umri wa miaka 23 na siku 37.

8) Michael Owen -

miaka 23, siku 133

Kama si majeruhi, Michael Owen angekuwa hatari sana kwenye soka la dunia. Kipindi hicho akiwa Liverpool fowadi huyo Mwingereza alikuwa moto wa kuotea mbali kwenye kutikisa nyavu na kumfanya afikishe idadi ya mabao 100 akiwa na umri mdogo sana, miaka 23 na siku 133. Kwa soka la klabu pekee, Owen, aliyewahi kuichezea pia Real Madrid na Manchester United, alifikisha idadi ya mabao 100 baada ya kucheza mechi 182.

9) Harry Kane -

miaka 23, siku 213

Tegemeo la Tottenham Hotspur kwenye kufunga mabao kwa sasa. Harry Kane amekuwa straika matata sana kwenye kupasia nyavu na hilo amekuwa akilifanya tangu akiwa mdogo, ambapo mabao yake 100 ya mwanzo kwenye maisha yake ya soka, alifikisha akiwa na umri wa miaka 23 na siku 213. Lakini, kwa upande wa mabao 100 ya ngazi ya klabu, Kane alifikisha idadi hiyo baada ya kucheza mechi 169. Timu kibao kwa sasa zinamtaka ikiwamo Man United.

10) Cristiano Ronaldo -

miaka 23, siku 255

Supastaa wa dunia, Cristiano Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji walionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao tangu walipokuwa na umri mdogo. Staa huyo, anayekipiga kwenye kikosi cha Juventus kwa sasa, alikohamia akitokea Real Madrid huku akiwahi pia kuichezea Manchester United, alifikisha idadi ya mabao yake 100 ya kwanza akiwa na umri wa miaka 23 na siku 255. Kwenye ngazi ya klabu peke yake, mabao 100 alifikisha baada ya mechi 105.