Mshahara wa kipa wa kipa bora Afcon 2023 wafunika

Kipa wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Ronwen Williams aliyeokoa penalti nne kwenye mchezo wa robo fainali za Afcon 2023, dhidi ya Cape Verde ni mmoja wa makipa wanaolipwa pesa nyingi Afrika.

Kwa mujibu wa mtandao wa Briefly wa nchini humo, Ronwen ni mchezaji wa pili kulipwa pesa nyingi kwenye kikosi cha Mamelodi Sundowns (Rand 500,000) kwa mwezi sawa na Sh66,747,000.

Ronwen ambaye amejiunga na Mamelodi akitokea SuperSport United mwaka 2022, kwa ada ya uhamisho ya Euro 880,0000 (Sh2 bilioni), mkataba wake na timu hiyo unamalizika mwaka 2027.

Kwa sasa ndiye kipa namba moja kwenye kikosi hicho msimu huu na amecheza mechi 26 za michuano yote, ameruhusu mabao saba na mechi 20 ametoka bila ya nyavu zake kuguswa.

Ronwen ameisaidia Afrika kusini kutinga nusu fainali ya Afcon na itacheza dhidi ya Nigeria, Februari 07 katika dimba la Boukae, saa 2:00 usiku.

Kwa sasa kipa wa Al Ahly, Mohamed El Shenaw anatajwa ndiye analipwa zaidi barani Afrika kwa makipa wanaocheza ndani na anaingiza Sh181,787,760.