Mpo? Msuva kukipiga Ligi moja na Cristiano Ronaldo

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva ambaye anaichezea Al Qadsiah ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia huenda akacheza Ligi moja na supastaa wa Ureno, Cristiano Ronaldo kutokana na kuhusishwa kwake na Al Fateh.

Al Fateh ambayo inashiriki Ligi Kuu Saudi Arabia imeripotiwa kuvutiwa na kiwango cha Msuva ambaye licha ya kwamba huu ni msimu wake wa kwanza, amefunga mabao manane na kuwa na wastani wa kufunga kwenye kila mchezo.

Kwa mujibu wa ripoti inaelezwa Al Fateh wamepanga kuingia sokoni mwishoni mwa msimu huu wa 2022/23 ili kutafuta winga mwenye uwezo wa kufunga na Msuva ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanafuatilia kwa karibu na timu hiyo.

Awali Msuva alikuwa akihusishwa na Al Ahli Saudi inayonolewa na Pitso Mosimane, chama hilo lipo kwenye nafasi ya kupanda Ligi Kuu kutokana na kuongoza msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza ambalo chama la Mtanzania huyo linapambana lisishuke.

Mara kadhaa Msuva amekuwa akieleza vile ambavyo anatamani kucheza Ligi Kuu Saudi Arabia hivyo tetesi hizo, zimeamsha upya matumaini yake.

"Bado hakuna mawasiliano yoyote rasmi ambayo yamefanyika, ni kweli na siwezi kuficha, natamani kucheza Ligi Kuu, nilitamani kuona timu yangu ikipanda daraja lakini hesabu zetu zimeenda tofauti na badala yake tumejikuta tukiwa kwenye hatari ya kushuka daraja."

"Yapo mambo mengi yametufanya kushindwa kufikia malengo, ila ni wajibu wetu wachezaji kupambana na kuibakisha timu," anasema mshambuliaji huyo.

Chama ambalo analichezea Msuva kwenye Ligi Daraja la Kwanza lipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa timu 18 huku wakiwa na pointi 34, "Zimebaki mechi tatu tu kabla ya msimu kumalizika, tunatakiwa kufanya vizuri kwenye kila mchezo ili tusogee nafasi za juu zaidi, itakuwa aibu kwetu tukishuka daraja."

Al Fateh ambayo inahusishwa na Msuva sio timu ya kinyonge, miongoni mwa nyota ambao wapo kwenye kikosi hicho ni pamoja na Cristian Tello ambaye aliwahi kufanya makubwa akiwa na Barcelona ya Ligi Kuu Hispania 'La Liga'.

Akiongelea uvumi huo wa Msuva kuhusishwa na Al Fateh, Omary Hassan ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini humo, anasema,"Hii ni wiki ya pili sasa hizo taarifa kuzisikia, tangu kipindi nilisikia amesaini timu ya Daraja la Kwanza niliamini ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza Ligi Kuu."

"Ligi Kuu Saudi Arabia kwa sasa inafuatiliwa sana kwa sababu ya wachezaji wengi wakubwa ambao wamekuwa wakisajiliwa, bado naamini Msuva ana nafasi ya kuendelea kufanya makubwa, kama ameweza kufanya vizuri Daraja la Kwanza basi huku haiwezi kuwa shida kabisa," anasema Mtanzania huyo.

Mbali na Ronaldo ambaye anaichezea Al-Nassr FC, majina mengine makubwa kwenye ligi hiyo ni pamoja na Anderson Talisca, Odion Ighalo na Abderrazak Hamdallah.


HII NDIO AL FATEH

Al Fateh imecheza katika madaraja ya chini kwa muda mwingi tofauti na wapinzani na majirani zao, Hajer FC ambao walicheza ligi kuu walipopanda daraja katika miaka ya 80, 90 na 2000.