Mpigambizi aangua kilio mbele ya baba’ke Olimpiki

Muktasari:
- Mrembo huyo na patna wake, Lois Toulson walipiga mbizi kwa mitindo matata kabisa na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu.
PARIS, UFARANSA: MPIGA mbizi, Andrea Spendolini-Sirieix ameangua kilio baada ya kumfurahisha baba yake kwa kushinda medali ya shaba kwenye Olimpiki.
Mrembo huyo na patna wake, Lois Toulson walipiga mbizi kwa mitindo matata kabisa na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu.
Wawili hao walishika nafasi ya pili kwenye raundi ya pili, lakini walimaliza nafasi ya tatu kwenye raundi ya mwisho na hivyo kushinda medali ya shaba.
Wakitokea kwenye nafasi ya tano katika raundi ya mwisho katika mashindano yaliyofanyika Aquatics Centre karibu na Stade de France huo ulionekana ni ushindi mkubwa kwao, ambapo walikuwa kwenye vita kali na Canada, iliyowakilishwa na wakali Caeli McKay na Kate Miller.
Warembo wa China, Chen Yuzi na Quan Hongchan ndio waliobuka washindi kwa kukusanya pointi 359.10, wakati wenzao wa Korea Kaskazini, Kim Mi-rae na Jo Jin-mi walishika namba mbili na pointi zao 315.90.
Timu ya China imekuwa ikifanikiwa kwenye mchezo huo tangu ulipotambulishwa kwenye Olimpiki mwaka 2000, hiyo ina maana imeshinda medali za dhahabu mara saba mfululizo.
Fred Sirieix alikuwapo jukwaani kwenye mchezo huo kumshuhudia binti yake akifanya mambo makubwa na kusababisha aangue kilio baada ya kuwa miongoni mwa walionyakua medali.