Mourinho: mi’ nilimpa ukweli salah

Muktasari:
- Juzi mashabiki wa soka walitokwa povu wakimwandama kocha huyo huku wakimshutumu kuwa alihusika kumuuza straika huyo ambaye kwa sasa ndiye habari ya ‘mujini’ dunia nzima.
LILE picha la kocha wa Manchester United, Jose Mourinho na ishu nzima ya kumuuza Mohamed Salah akiwa Chelsea linaendelea, na safari hii kocha huyo amekuja na ishu nyingine kabisa.
Juzi mashabiki wa soka walitokwa povu wakimwandama kocha huyo huku wakimshutumu kuwa alihusika kumuuza straika huyo ambaye kwa sasa ndiye habari ya ‘mujini’ dunia nzima.
Salah ambaye hakuchukua muda mrefu Stamford Bridge, wiki iliyopita alituzwa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kulipwa England (PFA) akiwa na Liverpool ambayo mpaka sasa ameshafumania nyavu mara 43 kwa mashindano yote.
Salah, 25, kwa sasa ndiyo nguzo ya mabao ya kikosi cha Jurgen Klopp na mashabiki wa Chelsea wanahoji imekuwakuwaje hadi wakamwachia Salah kuondoka kirahisi klabuni.
Mourinho wakati huo ndiye alikuwa kocha wa Chelsea kipindi ambacho alimwachia mchezaji huyo kwenda Fiorentina Februari 2015 na ilikuwa suala la kawaida.
‘Wanaposema mimi nimemuuza, wanaongopa. Si kweli kabisa. Mimi ndiye niliyemnunua. Mimi ndiye niliyekubali pia kumuuza kwa mkopo, nilidhani lilikuwa jambo la maana,’ Mourinho aliiambia ESPN Brasil. ‘Lakini ifahamike kuwa suala lake kuuzwa, pamoja na mimi kukubali, lakini halikuwa la mtu mmoja. Tulishirikiana kwa pamoja.”
Kwa mechi za Chelsea msimu wa 2013-14, Salah hakuwa katika kiwango ambacho Mourinho alikuwa anakitaka. Chelsea ilitoka suluhu na Norwich City na Salah alicheza kipindi kimoja kwa dakika 45 kabla ya kutoka.
Akiwa mwenye hasira, Mourinho inaelezwa kuwa alimwambia Salah ahakikishe anajifua kwa kiwango cha juu ili aje kuwa mwanasoka wa maana,”
Salah hakukaa Chelsea akachezeshwa mechi tatu tu chini Mourinho na akaamua kusepa zake Fiorentina.
Hiyo ilikuwa Julai 2015 na Mourinho hakuwa ameonyesha kumuhitaji tena Salah na wala kumtengenezea mazingira ya baadaye kurudi Chelsea.
Ndani ya miezi mitatu sasa akiwa Fiorentina, alionyesha soka ya kiwango lakini Mourinho akasema kuwa walimtoa Chelsea kwa uwazi kabisa.
‘Angalia, nilikuwa na mawinga watano, nikaona nimtoe, kumpoteza mchezaji mmoja si kitu, nikakubali apelekwe kwa mkopo Fiorentina,’ alisema Mourinho. ‘[Lakini Salah,] nikaona anaendelea vizuri.
Kocha huyo mwenye maneno mengi, anasema kumuuza mchezaji kwa ofa au kwa mkopo haijalishi sana, kama una wachezaji wengi huna sababu ya kubakia na wengine.
“Salah baadaye alijiunga na Roma kwa mkopo lakini klabu hiyo ya Serie A ilimtaka jumla wakaleta mzigo wa Pauni15mil tukamwachia.”