Ishu la Wirtz, Liverpool yakubali yaishe

Muktasari:
- Kiungo huyo raia wa Ujerumani anadaiwa amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano wa kuitumikia Liverpool lakini kinachokwamisha dili hilo ni makubaliano baina ya timu juu ya ada ya uhamisho.
LIVERPOOL, ENGLAND: MABOSI wa Liverpool wanajiandaa kulipa Pauni 126 milioni ili kumnasa kiungo wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz haraka iwezekanavyo.
Kiungo huyo raia wa Ujerumani anadaiwa amekubali kusaini mkataba wa miaka mitano wa kuitumikia Liverpool lakini kinachokwamisha dili hilo ni makubaliano baina ya timu juu ya ada ya uhamisho.
Kumekuwa na panda shuka nyingi katika mazungumzo baina ya timu hizi mbili lakini ripoti zinaeleza kwamba kocha Arne Slot amewaambia mabosi wa Liverpool wafanye kila linalowezekana kuhakikisha saini ya fundi huyo inapatikana.
Kutokana na hilo mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo, Michael Edwards amepewa ruhusa na wamiliki wa timu kwamba amalize dili na kulipa kiasi kinachohitajika.
Ripoti zinaongeza kwamba staa huyo mwenye miaka 22 atasaini mkataba baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa kumalizika Jumapili.
Wirtz alikuwa katika kikosi cha Ujerumani kilichocheza dhidi ya Ureno katika nusu fainali ya michuano ya Nations League.
Alifunga bao kwa kichwa muda mfupi baada ya mapumziko lakini Francisco Conceicao na Cristiano Ronaldo walifunga mabao ndani ya dakika tano na kugeuza matokeo.
Awali, Liverpool iliwasilisha ofa ya Pauni 110 milioni lakini Leverkusen ilikataa na kusisitiza kwamba bei ya staa huyo ni Pauni 126 milioni ambayo inaweza kufikia Pauni 130 milioni pamoja na ada ya ziada zitakazotokana na kiwango chake.
Hadi sasa Liverpool imeshafanya biashara moja na Leverkusen ambapo imemsajili beki Jeremie Frimpong kwa Pauni 29 milioni ili kwenda kuziba pengo la Trent Alexander Arnold.
Ripoti zilidai kuwa Wirtz ambaye huvaa jezi namba 10 akiwa na Liverkusen na namba 17 akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani akisajiliwa Liver anaweza kuvaa jezi namba 10 ambayo kwa sasa inavaliwa na Alexis Mac Allister, lakini mwenyewe alikanusha.
Alisema: “Nani amesema nataka namba 10. Nawaheshimu wachezaji. Msiamini kila kitu kinachoandikwa.”