Morocco haishikiki, Diarra atinga mtoano
Muktasari:
- Simba wa Atlas, ambao wameizidi pointi nne timu inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi, Mali baada ya kuzoa pointi nne katika mechi zao mbili za kwanza, ilianza kwa kasi katika mchezo huo wa Rabat dhidi ya Zambia, ambapo Ayoub El Kaabi alifunga kwa kichwa katika dakika ya tisa tu na kufunga baada ya kona.
RABAT, MOROCCO: WENYEJI wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025), Morocco wameibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Zambia na kumaliza vinara kwenye Kundi A huku ikimkaribisha mchezoni nahodha wao Achraf Hakimi, aliyekuwa majeruhi.
Simba wa Atlas, ambao wameizidi pointi nne timu inayoshika nafasi ya pili kwenye kundi, Mali baada ya kuzoa pointi nne katika mechi zao mbili za kwanza, ilianza kwa kasi katika mchezo huo wa Rabat dhidi ya Zambia, ambapo Ayoub El Kaabi alifunga kwa kichwa katika dakika ya tisa tu na kufunga baada ya kona.
Brahim Diaz alifanya ubao wa matokeo kusomeka 2-0, akimalizia vyema kazi ya Abde Ezzalzouli na hivyo kufunga bao lake la tatu katika mashindano hayo ya Afcon 2025.
El Kaabi alifunga kwa tick-tack matata kabisa dakika ya tano baada ya kipindi cha pili kuanza kufanya matokeo kusomeka 3-0, ambapo bao hilo lilikubaliwa baada ya VAR kulipitisha kwamba hakukuwa na tukio la kuotea.
Morocco, inafukuzia taji lake la kwanza la Afrika tangu 1976, ilitumia mchezo huo wa mwisho wa hatua ya makundi kumkaribisha beki wa kuia wa Paris St-Germain, Hakimi, ambaye amekuwa nje ya uwanja kwa karibu miezi miwili kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya enka.
Hakimi nusura afunge bao katika dakika tisa za mwisho, lakini jaribio lake liliokolewa na kipa wa Chipolopolo, Willard Mwanza.
Kikosi hicho cha kocha Walid Regragui sasa kitasubiri timu ya tatu bora kutoka Kundi C, D au E ili kukabiliana nayo kwenye mechi ya mtoano hatua ya 16 bora. Kwa matokeo ya mechi za Kundi A na Kundi B hiyo ina maana Benin, Sudan na Msumbiji zimejihakikishia nafasi kwenye hatua ya 16 bora.
Zambia, kwa upande wao wametupwa nje ya mashindano, huku ikicheza mechi ya 13 kwenye Afcon bila ushindi rekodi yao inayoanzia tangu kwenye ushindi wa nusu fainali dhidi ya Ghana kabla ya ubingwa wao wa Afcon ya nchini Gabon 2012.
Katika mchezo mwingine wa Kundi A, Comoro na Mali zimetoka sare ya bila kufungana na hivyo kufanya msimamo wa kundi hilo kuzibakiza Comoro na Zambia zikiwa na pointi mbili kila moja huku Mali ya kipa Djigui Diarra ikikusanya pointi tatu na Morocco pointi saba.