Morata achafua hali ya hewa

Muktasari:

  • Morata, ambaye anaiongoza Hispania katika michuano ya Euro inayoendelea Ujerumani, amesema ni  rahisi kwake kuhama nchi kutokana na dharau na jinsi anavyochukuliwa hali inayoathiri familia yake, ikiwa ni pamoja na mke wake na watoto wanne wadogo.

MADRID, HISPANIA: ALVARO Morata amechafua hali ya hewa katika kambi ya timu ya taifa ya Hispania baada ya kuweka wazi anafikiria hata kuachana na timu hiyo ya taifa na kuondoka Hispania kutokana na dharau anazoonyeshwa.

Morata, ambaye anaiongoza Hispania katika michuano ya Euro inayoendelea Ujerumani, amesema ni  rahisi kwake kuhama nchi kutokana na dharau na jinsi anavyochukuliwa hali inayoathiri familia yake, ikiwa ni pamoja na mke wake na watoto wanne wadogo.

Kabla ya mechi yake ijayo dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali ya kwanza kesho, mahojiano na El Mundo yamezua taharuki katika nchi yake.

“Inaweza kuwa michuano yangu ya mwisho na Hispania,” alisema Morata ambaye amewahi kupita Real Madrid, Juventus na Chelsea.

Inaelezwa mashabiki wengi wa Hispania hawamkubali staa huyu na waliwahi kumzomea katika mchuano ya Euro 2020, pia alidhihakiwa alipokuwa uwanja wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Hispania na Brazil, Machi mwaka huu.

“Nikiwa Hispania ni ngumu kwangu kuwa na furaha,” bila shaka huwa napata furaha zaidi nje ya nchi hii. Nimesema mara nyingi hili na ni kwa sababu watu hawaniheshimu, yaani hamna heshima hata kidogo,” alisema Morata.

“Juzi, watu walisema nilikuwa nalia uwanjani, kwa sababu nilikuwa nimepewa kadi ya njano, huu ni upuuzi, mimi nilikuwa nalia kwa sababu ya nchi yangu, nikiwa nahodha, niliguswa kwa kuingia nusu fainali.”

“Ingekuwa mimi nisingeweza ukumkosoa mtu yeyote ambaye angekuwa analia kwa sababu hiyo, lakini nilikosolewa, najaribu kufurahia mashindano haya, ambayo yanaweza yakawa ya mwisho nikiwa na timu ya taifa, inawezekana siku moja wakanikumbuka, nafurahi kuona kila siku muda wa kuhudumu timu ya taifa unapungua.”

Morata anaeleza hali hii pia inaathiri familia yake ambayo pia inashuhudia haya yanayoendelea na ndiyo maana anafikiria hata kuondoka Atletico dirisha hili na atafanya uamuzi zaidi baada ya kumaliza michuano ya Euro.

Haya ya Morata yaliibuka juzi ikiwa ni siku moja kabla ya mchezo wa nusu fainali kati Hispania na Ufaransa uliopigwa jana kati yao na Ufaransa.