Mkwanja waongezwa Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti, timu itakayofika fainali itapata zawadi ya takribani Pauni 39 milioni ikiwa ni ongezeko kubwa tofauti na ilivyokuwa katika Kombe la Dunia lililopita.
NEW YORK, MAREKANI: SHIRIKISHO la Soka la England pamoja na mashirikisho mengine yatakayoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwakani huko Marekani, Canada na Mexico sasa meno yote nje kutokana na kiasi kikubwa cha pesa ambacho wanatarajiwa kukiingiza.
Kwa mujibu wa ripoti, timu itakayofika fainali itapata zawadi ya takribani Pauni 39 milioni ikiwa ni ongezeko kubwa tofauti na ilivyokuwa katika Kombe la Dunia lililopita.
FIFA imetangaza ongezeko la asilimia 50 ya fedha zitakazogawanywa kwa timu shiriki za Kombe la Dunia lijalo ambazo ni nyingi ikilinganishwa na Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.
Zawadi kwa mshindi wa fainali ya Julai 19 itakayochezwa kwenye Uwanja wa MetLife itaongezeka hadi Pauni 37.5 milioni, kutoka Pauni 31.5 milioni iliyotolewa Qatar.
Mbali ya zawadi hiyo ya fainali, kabla ya kuanza kwa mashindano, timu zote 48 zilizofuzu zitapewa Pauni 1.1 milioni kila moja kwa ajili ya kugharamia maandalizi.
Vilevile ikiwa timu itaishia makundi inaweza kupata takribani Pauni 7.9 milioni na ikiishia robo fainali itaweza kupata Pauni 14.2 milioni ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na Pauni 12.7 milioni ambayo timu zilizoishia robo fainali katika mashindano ya Qatar zilikuwa zikipewa.
Kuongezwa kwa idadi ya timu hadi kufikia 48 kutoka 32 za awali ni moja ya sababu kubwa za kuongezeka kwa pesa za jumla za zawadi ambazo sasa ni Pauni 491 milioni kutoka Pauni 330 milioni za Kombe la Dunia la 2022.
Ongezeko kubwa zaidi, la Pauni 6 milioni ni kwa mabingwa wa mashindano, huku timu itakayopoteza fainali ikipata Pauni 24.7 milioni ikilinganishwa na Pauni 22.5 milioni ilizolipwa Ufaransa baada ya kupoteza mbele ya Argentina.
Baraza la Utawala la FIFA, lilipitisha uamuzi wa bajeti mpya katika kikao chake kilichofanyika Doha, kabla ya fainali Kombe la Mabara kati ya PSG na Flamengo ya Brazil.
Hata hivyo, Fifa imekumbana na ukosoaji mkubwa duniani kuhusu bei za tiketi za mechi za Kombe la Dunia ambapo karibu tiketi zote za fainali isipokuwa 1,000 tu zitauzwa kwa bei ya kuanzia pauni 3,119.
FIFA imesisitiza kuwa kutakuwa na mapato ya kifedha ya kihistoria yatakayofikia Pauni 546 milioni.