Mipango ya Barca kurudi Nou Camp yavurugika
Muktasari:
- Barca haijacheza kwenye uwanja huo maarufu tangu Machi 2023, na badala yake imekuwa ikicheza Estadi Olimpic Lluis Companys wakati kazi kubwa za ukarabati zikifanyika pale Uwanja Camp Nou.
BARCELONA, HISPANIA: MABINGWA watetezi wa La Liga, Barcelona wako tayari kufuta mpango wao wa kurudi kwenye Uwanja wa Spotify Camp Nou kwa ajili ya mechi ya Joan Gamper Trophy dhidi ya Como mwezi ujao kutokana na kutokamilika kwa matengenezo.
Barca haijacheza kwenye uwanja huo maarufu tangu Machi 2023, na badala yake imekuwa ikicheza Estadi Olimpic Lluis Companys wakati kazi kubwa za ukarabati zikifanyika pale Uwanja Camp Nou.
Mwezi uliopita Barcelona ilitangaza nia ya kurudi Spotify Camp Nou kwa ajili ya Joan Gamper Trophy Agosti 10, lakini ripoti zinaeleza kuwa mpango huo utalazimika kufutwa kwa sababu Halmashauri ya Jiji haitaki kutoa leseni kwani inaona kuna maeneo hayapo sawa na inaweza kuleta shida kwa mashabiki.
Ripoti inaongeza kuwa Idara ya Mipango ya Miji ya Halmashauri ya Jiji tayari imesema wazi kuwa maeneo ya viti yanahitaji kukamilika kikamilifu kabla ya kutoa idhini ya kuruhusu umma kuingia uwanjani.
Barcelona sasa inapanga kutumia siku ya Septemba 14, kwa ajili ya ufunguzi mkubwa wa uwanja huo ambapo itakuwa inacheza dhidi ya Valencia katika La Liga.
Hata hivyo, hakuna uhakika kama hilo litatimia, kwani kuna uwezekano pia hadi kufikia wakati huo wakawa hawajapata kibali.
Vijana hawa wa Hansi Flick wamepangwa kusafiri hadi Japan na Korea Kusini kwa ajili ya mazoezi ya maandalizi ya msimu.
Mechi yao ya mwisho ya kirafiki itakuwa ni dhidi ya Como ya Italia ambayo itakuwa ya kikombe cha Joan Gamper mwezi ujao na baada ya mchezo huo itaanza rasmi La Liga kwa kucheza dhidi ya Mallorca Agosti 16.