Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbwa amponza beki Real Madrid

Muktasari:

  • Mbali na kifungo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa pia anaweza kutozwa faini mbalimbali kufuatia tukio hilo, ambalo liliwaacha mbwa wawili wa watu wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Mmoja wao baadaye alilazimika kuuawa kwa njia ya kitabibu kutokana na majeraha makubwa aliyopata.

MADRID, Hispania: BEKI wa Real Madrid, Ferland Mendy anakabiliwa na uwezekano wa kufungwa jela baada ya mbwa wake kudaiwa kumjeruhi kijana katika tukio la mashambulizi ya kung'ata watu.

Mbali na kifungo, mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa pia anaweza kutozwa faini mbalimbali kufuatia tukio hilo, ambalo liliwaacha mbwa wawili wa watu wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Mmoja wao baadaye alilazimika kuuawa kwa njia ya kitabibu kutokana na majeraha makubwa aliyopata.

Mendy, ambaye ameichezea Real Madrid tangu aliposajiliwa kutoka Lyon mwaka 2019, amesaidia klabu hiyo kutwaa mataji matatu ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 sasa atakabiliwa na mchakato wa kisheria nchini Hispania kufuatia tukio lililotokea Januari 2023 katika kitongoji cha Alcobendas, jijini Madrid.

Kijana aliyekuwa na umri wa miaka 17 wakati wa tukio anadai kuwa mmoja wa mbwa wa Mendy alimng'ata mguu wake wa kushoto. Mawakili wake wameiomba mahakama kumhukumu Mendy kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kusababisha majeraha kutokana na uzembe mkubwa.

Waendesha mashtaka, kwa upande wao, wamependekeza mchezaji huyo atozewe faini zinazoweza kufikia euro 25,000.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa katika Mahakama Namba 26 ya Madrid, ingawa tarehe rasmi ya kusikilizwa bado haijatangazwa.

Inadaiwa kuwa mbwa wanne wa Mendy walitoroka kutoka nyumbani kwake baada ya lango kuachwa wazi.

Mmoja wa mbwa hao anadaiwa kumshambulia mbwa aina ya dachshund wa mwanamke mmoja, ambaye baadaye alilazimika kuuawa kutokana na majeraha makubwa aliyopata.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17, ambaye pia alikuwa akimtembeza mbwa wake, alijeruhiwa kwa kung'atwa alipokuwa akijaribu kumsaidia mwanamke huyo.

Mbwa wake pia alidaiwa kushambuliwa, hali iliyosababisha gharama kubwa za matibabu ya mifugo.

Ofisi ya Waendesha Mashtaka ya Madrid ilisema kuwa Mendy hakuchukua tahadhari zinazotakiwa katika kuwadhibiti mbwa wake.

"Tendo hilo lilisababisha hatari kubwa kwa watu na wanyama wengine," ilisema taarifa hiyo.

Mendy ameichezea Ufaransa mara 10, mechi yake ya mwisho ikiwa mwaka 2024.

Msimu uliopita alicheza mechi tisa pekee akiwa na Real Madrid, huku ripoti zikieleza kuwa mustakabali wake katika Uwanja wa Santiago Bernabeu unaweza kuwa wa mashaka chini ya kocha mpya, Jose Mourinho.