Matumizi ya pesa yamridhisha Slot
Muktasari:
- Uwekezaji wa Pauni 295 milioni katika dirisha hili imekuwa ni mada kubwa ya mijadala, kwani ni tofauti na Liverpool ilivyozoeleka katika miaka kadhaa iliyopita.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot amesema kuwa pesa nyingi zinazomwagwa na timu hiyo katika dirisha hili ni lazima zitumike ili wasiachwe nyuma.
Uwekezaji wa Pauni 295 milioni katika dirisha hili imekuwa ni mada kubwa ya mijadala, kwani ni tofauti na Liverpool ilivyozoeleka katika miaka kadhaa iliyopita.
Mbali ya wachezaji kama Florian Wirtz na Hugo Ekitike ambao wamesajiliwa kwa pesa nyingi, klabu hii huenda ikasajili wachezaji zaidi kabla ya dirisha kufungwa, kwani Slot anahitaji beki wa katikati na mshambuliaji mmoja.
Katika miezi 12 iliyopita Liverpool imenunua mchezaji mmoja tu ambaye ni Federico Chiesa na Slot anaamini kusingefanyika usajili katika dirisha hili ingezidisha hatari ya timu kufanya vibaya kwani kuna uwezekano wapinzani wao kuwatabiri kirahisi.
Katika mahojiano aliyofanya na moja ya televisheni huko England Slot alisema:
“Tumeongeza ubunifu kwa kumsajili Florian, kasi kupitia Jeremie Frimpong, Hugo na Milos Kerkez. Kawaida ikiwa hutobadilika, ukibaki kufanya mambo kama kawaida, watu wanaweza kupata jibu la jinsi ya kucheza dhidi yako. Hilo lilitokea nusu ya pili ya msimu uliopita, ingawa kwa kimahesabu tulipata pointi nyingi katika nusu ya pili kama nusu ya kwanza.”
“Niliona tulikumbwa na changamoto zaidi. Niliiona tukipata mabao mengi zaidi kutoka kwenye mpira wa kona katika nusu ya pili ya msimu, tulipata mabao ya aina hiyo dhidi ya West Ham United ugenini. Nottingham Forest ugenini.Leicester City ugenini, ambapo tulishinda kwa bao 1-0.
Hivyo tulilazimika kutegemea zaidi mpira wa kona ambao ingawa ni sehemu ya mpira wa miguu, lakini tulitakiwa kutengeneza nafasi zaidi kuanzia chini, lakini ilishindikana kwa sababu tulipoteza muundo wetu wa safu ya ulinzi na wapinzani wetu walishaanza kujua mbinu za kucheza na sisi.”