Mastaa Real Madrid hatarini kufungiwa

Muktasari:
- Masupastaa wa Real Madrid, washambuliaji Kylian Mbappe na Vinicius Junior, beki wa kati Antonio Rudiger na kiungo Dani Caballos wameingizwa kwenye uchunguzi wa Uefa kutokana na kile walichofanya kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya mahasimu wao wa Madrid derby, Atletico Madrid.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Arsenal inaweza kupata mserereko kwenye mechi yake ijayo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya mastaa wanne wa Real Madrid kuwa kwenye hatari ya kufungiwa kucheza kipute hicho cha robo fainali mwezi ujao.
Masupastaa wa Real Madrid, washambuliaji Kylian Mbappe na Vinicius Junior, beki wa kati Antonio Rudiger na kiungo Dani Caballos wameingizwa kwenye uchunguzi wa Uefa kutokana na kile walichofanya kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya mahasimu wao wa Madrid derby, Atletico Madrid.
Kamati ya nidhamu ya Uefa imeunda tume ya uchanguzi juu ya wachezaji hao wanne baada ya kudaiwa kufanya vitu visivyokuwa vya kiungwana katika mechi hiyo iliyokutanisha mahasimu wakubwa. Mambo hayo yanayochunguzwa yanaripotiwa kutokea kwenye mechi ya marudiano ya hatua hiyo ya 16 bora iliyofanyika Machi 12. Adhabu yao kama watakutwa na hatia bado haijafahamika. Lakini, kama watafungiwa itakuwa faida kubwa kwa Arsenal, ambayo yenyewe pia inakosa mastaa wake muhimu kutokana na kuwa majeruhi. Arsenal itakipiga na Real Madrid uwanjani Emirates, Jumanne, Aprili 8 kabla ya kurudiana kwenye mchezo utakaofanyika Bernabeu, Jumatano ya wiki inayofuatia.
Na Vinicius na Mbappe ndiyo vinara wa mabao wa Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, kila mmoja akifunga mara saba.
Madrid imetinga nusu fainali baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia ushindi wa Atletico wa bao 1-0 nyumbani kwenye mechi ya marudiano baada ya ile ya kwanza Los Blancos kushinda 2-1 Bernabeu na kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2, jambo lililohitajika kupigwa mikwaju ya penalti.
Vinicius alidaiwa kujibizana na mashabiki wa Atletico, wakati Rudiger alionyesha ishara ya kuchinja, huku Ceballos akilalamikiwa juu ya ushangiliaji wake wa ishara ya bastola, wakati Mbappe alishangilia kwa kushika sehemu za siri.
Atletico iliwasilisha malalamiko Uefa, ambayo yameanza kufanyiwa kazi na kinachosubiriwa kama mastaa hao, Rudiger, Ceballos, Vinicius au Mbappe kuna atakayeadhibiwa au kama adhabu itawahusu wote kwa pamoja.