Mastaa kibao kukosa Arsenal na Chelsea
Muktasari:
- The Gunners wanatarajia kuendeleza ushindi wao wa mabao 4-1 iliyoupata dhidi ya Tottenham Hotspur katika dabi ya kaskazini mwa London Jumapili iliyopita, kwa kupata ushindi mwingine muhimu katika harakati zao za kutwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada miaka 22.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL na Chelsea zinakutana kwa mara ya nne ndani ya miezi mitatu, ambapo kikosi cha Mikel Arteta kikiwakaribisha The Blues katika Uwanja wa Emirates kwa ajili ya kipute cha Ligi Kuu England, Jumapili.
The Gunners wanatarajia kuendeleza ushindi wao wa mabao 4-1 iliyoupata dhidi ya Tottenham Hotspur katika dabi ya kaskazini mwa London Jumapili iliyopita, kwa kupata ushindi mwingine muhimu katika harakati zao za kutwaa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England baada miaka 22.
Lakini, Chelsea itakuwa na hamasa ya kurejea katika njia ya ushindi baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Burnley, Jumamosi iliyopita na kuimarisha matumaini yao ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, wachezaji kadhaa watakosekana katika mchezo wa Jumapili kaskazini mwa London. Arsenal itamkosa Mikel Merino anayeendelea kupona baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu. Kai Havertz, Ben White na Bukayo Saka wako kwenye mbio za kurejea uwanjani, huku Arteta akithibitisha Ijumaa kuwa watasubiri hadi Jumamosi kuamua upatikanaji wao.
Max Dowman alirejea kuichezea Arsenal ya chini ya miaka 21 dhidi ya Ipswich Town, Ijumaa, baada ya kukaa nje kwa miezi mitatu kutokana na tatizo la kifundo cha mguu. Mchezo wa Jumapili dhidi ya Chelsea huenda ukawa wa mapema mno kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16 kucheza. Kwa upande wa Chelsea, ina orodha ndefu zaidi ya majeruhi au wanaotumikia adhabu ya marufuku kwa mechi hiyo.
Levi Colwill ni miongoni mwa waliokaa nje kwa muda mrefu, hajacheza kutokana na jeraha la goti. Jamie Bynoe-Gittens na Estevao kwa sababu ya majeraha ya paja, huku Wesley Fofana akifungiwa kufuatia kadi nyekundu katika sare dhidi ya Burnley.
Dario Essugo pia ni majeruhi wa muda mrefu na hatarajiwi kurejea adi hapo baadaye mwezi huu. Estevao anaendelea kuuguza jeraha. Bado hajaichezea tangu alipojiunga kwa Pauni 18.5 milioni akitokea Sporting CP majira ya joto yaliyopita.
Marc Cucurella pia hatapatikana baada ya kupata jeraha la msuli wa nyuma wa paja katika sare dhidi ya Leeds United mapema mwezi huu, ingawa Rosenior ana matumaini kuwa atarejea hivi karibuni. Mykhailo Mudryk ndiye mchezaji mwingine wa Chelsea ambaye hakika atakosa safari ya kwenda Emirates. Filip Jorgensen, kwa upande mwingine, anaweza kurejea kikosini kuikabili Arsenal, ingawa atafanyiwa tathmini ya mwisho ya utimamu wa mwili na huenda asianze katika kikosi cha kwanza.
Ukiweka kando kipute hicho cha dabi ya London kati ya Arsenal na Chelsea, mechi nyingine za Ligi Kuu England zitakazopigwa Jumapili, Brighton itacheza na Nottingham Forest, wakati Fulham itakuwa nyumbani kukabiliana na Tottenham Hotspur, huku Manchester United ikijimwaga uwanjani Old Trafford kukabiliana na Crystal Palace, mechi ambayo ushindi kwa vijana wa Michael Carrick utawafanya kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.