Walipo kwa sasa mastaa wa Leicester City waliofanya maajabu 2016
Muktasari:
- Kocha, Claudio Ranieri aliiongoza timu ambayo ilikuwa imetumia sehemu kubwa ya msimu uliotangulia ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hadi kufikia moja ya ushindi wa ajabu zaidi wa ubingwa katika historia ya soka.
LONDON, ENGLAND: MSIMU wa 2015-16, Leicester City iliushangaza ulimwengu wa michezo kwa kushinda taji la Ligi Kuu England licha ya kuanza msimu ikiwa na uwezekano finyu kabisa na wacheza kamari waliobainisha kuwa ni uwezekano wa 5000/1.
Kocha, Claudio Ranieri aliiongoza timu ambayo ilikuwa imetumia sehemu kubwa ya msimu uliotangulia ikiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hadi kufikia moja ya ushindi wa ajabu zaidi wa ubingwa katika historia ya soka.
Wakati Christian Fuchs hivi karibuni akiteuliwa kuwa kocha mkuu wa Newport County ya League Two, swali lililoibuka ni nini kiliwapata wachezaji wengine wa kikosi hicho cha kipekee cha Leicester City kilichobeba ubingwa kimiujiza?
Kasper Schmeichel
Nafasi: Golikipa
Umri: 39
Msimu wa 2015-16 ulikuwa wa tano kwa Schmeichel akiwa Leicester City na aliendelea kucheza katika Uwanja wa King Power kwa misimu sita zaidi, akifikisha jumla ya mechi 479 katika mashindano yote na kujiimarisha kama gwiji halisi wa klabu hiyo. Alihamia OGC Nice mwaka 2022 na kucheza msimu mmoja katika Ligue 1, kabla ya kuhamia R.S.C. Anderlecht kwa mwaka mmoja katika Ligi Kuu Ubelgiji. Kwa sasa ndiye golikipa namba moja wa Celtic baada ya kujiunga na klabu hiyo ya Glasgow mwaka 2024, akishinda Scottish Premiership na Kombe la Ligi katika msimu wake wa kwanza Celtic Park.
Ritchie De Laet
Nafasi: Beki wa Kulia
Umri: 36
Baada ya kucheza mechi chache katika nusu ya kwanza ya msimu akiwa Leicester City kabla ya kuhamia Middlesbrough, Ritchie de Laet alipata mafanikio ya kipekee katika msimu wa 2015/16, akipata medali ya mshindi wa Ligi Kuu England pamoja na kupanda daraja kutoka Championship katika msimu huo huo.
Aliondoka kwenye timu hiyo majira ya joto yaliyofuata na kujiunga Aston Villa na alicheza mechi nane tu za ligi katika kipindi cha miaka mitatu kabla ya kutumia miaka mitano katika klabu ya kwao ya Royal Antwerp. Alistaafu kucheza mwaka 2024, lakini bado yupo katika klabu hiyo ya Ligi Kuu Ubelgiji kama kocha wa akademi.
Danny Simpson
Nafasi: Beki wa Kulia
Umri: 38
Baada ya kumwondoa Ritchie De Laet katika nafasi ya beki wa kulia, Simpson alithibitisha kuwa chaguo la kuaminika kwa Leicester City kwa misimu kadhaa kabla ya kupoteza nafasi yake kikosini na kucheza kwa vipindi vifupi Huddersfield Town na Bristol City kwenye Championship.
Alifanya kazi kama mchambuzi wa soka kwenye televisheni mwaka 2022, kisha akacheza kwa muda Macclesfield, kabla ya kupambana na YouTuber Danny Aarons katika pambano la ndondi la hisani jijini Dublin mwaka 2024. Hivi karibuni amefungua mgahawa katika mji alikozaliwa wa Salford.
Wes Morgan
Nafasi: Beki wa Kati
Umri: 41
Gwiji mwingine wa “The Foxes”, Morgan alikuwa nahodha wa kikosi hicho cha Leicester pamoja na Kasper Schmeichel walicheza kila dakika ya msimu huo wa kihistoria. Kwa kufanya hivyo, alikua mchezaji wa tatu tu asiyekuwa kipa katika historia ya Ligi Kuu England kucheza kila dakika ya msimu wa ubingwa.
Aliendelea kubaki King Power hadi mwisho wa maisha yake ya soka, akistaafu mwaka 2021 akiwa amecheza jumla ya mechi 323 na kufunga mabao 14 kwa klabu. Alipata shahada ya Uzamili (MSc) ya kuhusu Sports Directorship kupitia UCFB na sasa anafanya kazi kama Skauti wa Akademi ya Taifa kwa klabu yake nyingine ya zamani, Nottingham Forest.
Robert Huth
Nafasi: Beki wa Kati
Umri: 41
Huth alijiunga na Leicester moja kwa moja katika majira ya joto ya 2015 baada ya kufurahia kipindi kizuri cha mkopo katika msimu uliotangulia. The Foxes walikuwa klabu yake ya mwisho kwani alistaafu mwaka 2018 akiwa amecheza zaidi ya mechi 400 katika taaluma yake, zikiwemo 93 akiwa Leicester.
Alipata shahada ya Sports Directorship kutoka Chuo Kikuu cha Salford na akarejea King Power kufanya kazi kama Meneja wa Mikopo ya wachezaji, kabla ya kuondoka mwaka 2024. Tangu hapo ameonekana akicheza katika mechi za mastaa wa zamani wa Stoke City na Chelsea.
Christian Fuchs
Nafasi: Beki wa Kushoto
Umri: 39
Alikuwa usajili mzuri kwa Leicester City. katika majira ya joto ya 2015. Fuchs alifurahia msimu wake wa kwanza bora nchini England na alidumu klabuni hapo kwa jumla ya miaka sita, akicheza zaidi ya mechi 150 kabla ya kuhamia Marekani kujiunga na Charlotte FC mwaka 2021.
Baada ya kumaliza maisha yake ya uchezaji, Fuchs aliendelea kubaki katika klabu hiyo ya Major League Soccer kama kocha msaidizi kabla ya kurejea England kwa mshangao Novemba 2025 kuchukua nafasi yake ya kwanza kama kocha mkuu wa Newport County.
Jeffrey Schlupp
Nafasi: Beki wa Kushoto/Kiungo
Umri: 32
Akiwa amekulia katika akademi ya Leicester, Schlupp alipata nafasi za kucheza mara chache katika msimu wa ubingwa wa 2015-16. Uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali ulikuwa muhimu kwa kocha Claudio Ranieri na alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa klabu mwishoni mwa msimu.
Alijiunga na Crystal Palace mwaka 2017 na alidumu Selhurst Park kwa miaka minane, akicheza mechi 220 za Ligi Kuu England . Baada ya kucheza kwa mkopo Celtic, alijiunga na Norwich City kwa uhamisho wa bure mwaka 2025.
N'Golo Kante
Nafasi: Kiungo wa Kati
Umri: 34
Kante alitumia msimu mmoja tu, lakini wa kipekee, katika Uwanja wa King Power, akicheza mechi 37 za Ligi Kuu England baada ya kujiunga kutoka SM Caen katika majira ya joto ya 2015. Alikuwa mmoja wa wachezaji wanne wa Leicester walioteuliwa katika Kikosi Bora cha Mwaka cha PFA mwishoni mwa msimu.
Alishinda tena taji la Ligi Kuu England msimu uliofuata baada ya kujiunga na Chelsea mwaka 2016, na pia akashinda Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na FIFA Club World Cup katika kipindi cha miaka saba Stamford Bridge. Alijiunga na Al-Ittihad Club mwaka 2023, akishinda Saudi Pro League na Kombe la Mfalme katika msimu wa 2024-25.
Danny Drinkwater
Nafasi: Kiungo wa Kati
Umri: 35
Mwaka mmoja baada ya N'Golo Kante kuhamia Stamford Bridge kujiunga na Chelsea, alifuatiwa na mwenzake wa zamani wa Leicester City, Danny Drinkwater. Hata hivyo, wawili hao hawakuweza kurudia ushirikiano wao bora waliouonyesha katika Uwanja wa King Power, kwani nafasi za kikosi cha kwanza zilikuwa chache kwa mhitimu huyo wa akademi ya Manchester United.
Drinkwater alicheza mechi 12 pekee katika kipindi cha miaka mitano Stamford Bridge, akitolewa kwa mkopo katika klabu za Burnley, Aston Villa, Kasimpasa S.K. na Reading kabla ya kustaafu mwaka 2022. Kwa sasa anajishughulisha na biashara ya maendeleo ya majengo.
Andy King
Nafasi: Kiungo wa Kati
Umri: 37
Mchezaji mwingine aliyekaa muda mrefu Leicester, King alikuwa tayari ametumikia klabu hiyo kwa miaka 10 wakati iliponyanyua taji la Ligi Kuu England mwaka 2016 na aliendelea kubaki hapo kwa miaka minne zaidi, ingawa kipindi hicho kilijumuisha mikopo katika timu za Swansea City, Derby County, Rangers na Huddersfield Town.
Baada ya kucheza mechi 55 katika Championship akiwa na Bristol City, King alistaafu mwaka 2021 na tangu hapo amerejea katika klabu aliyotambulika nayo zaidi wakati wa uchezaji wake. Kwa sasa anafanya kazi kama kocha wa kikosi cha kwanza Leicester chini ya kocha mkuu Marti Cifuentes.
Marc Albrighton
Nafasi: Winga
Umri: 36
Baada ya kujiunga na Leicester City kutoka klabu jirani ya Midlands, Aston Villa, mwaka mmoja tu kabla ya msimu wa ubingwa, Albrighton alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi kilichoshinda taji hilo na alibaki na The Foxes kwa miaka minane zaidi kabla ya kustaafu mwaka 2024.
Kama ilivyokuwa kwa mwenzake wa zamani, Wes Morgan, Albrighton amerejea katika mizizi yake na kuchukua jukumu la ukocha katika akademi ya klabu yake ya kwanza, Aston Villa. Pia alicheza kwa timu ya Wrexham katika mashindano ya TST ya wachezaji saba kwa kila upande yaliyofanyika North Carolina majira ya joto mwaka 2025.
Riyad Mahrez
Nafasi: Winga
Umri: 34
Nguvu ya ubunifu nyuma ya kikosi hiki cha Leicester City, Mahrez alifunga mabao 18 na kutoa asisti 10 katika msimu huo wa kukumbukwa. Kiwango chake kilimfanya ashinde tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika ya BBC na kumaliza katika nafasi ya saba kwenye tuzo ya Ballon d'Or.
Alibaki Leicester kwa misimu miwili zaidi kabla ya kujiunga na Manchester City, ambako alishinda mataji manne zaidi ya Ligi Kuu England katika misimu mitano, pamoja na taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja, Kombe la FA mara mbili na Kombe la Ligi mara tatu. Kwa sasa yuko katika msimu wake wa tatu na klabu ya Ligi Kuu Saudia, Al-Ahli, ambako alishinda AFC Champions League msimu 2024-25.
Demarai Gray
Nafasi: Winga
Umri: 29
Mchezaji pekee aliyesajiliwa mwezi Januari ambaye alipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika msimu wa 2015-16, Gray mwenye umri wa miaka 20 wakati huo alikuwa chaguo muhimu la benchi katika hatua za mwisho za kampeni kabla ya kujithibitisha kama mchezaji wa kikosi cha kwanza katika misimu iliyofuata.
Baada ya kufunga mabao 10 katika mechi 133 za Ligi Kuu England, Gray alihamia Bayer Leverkusen na baadaye kucheza kwa vipindi Everton na Al-Ettifaq. Akiwa bado na umri wa miaka 29, alirejea katika klabu yake ya utotoni, Birmingham City mwaka 2025. Pia ameichezea timu ya taifa ya Jamaica mara 29 tangu 2023, akifunga mabao saba.
Nathan Dyer
Nafasi: Winga
Umri: 37
Dyer alisaini kwa mkopo wa msimu mmoja kujiunga na Leicester katika kampeni hiyo na alicheza mechi 12 baada ya kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza kwa misimu sita iliyotangulia akiwa na Swansea City.
Alifunga bao moja tu kwa The Foxes, lakini lilikuwa muhimu sana, bao la ushindi katika dakika za mwisho katika ushindi dhidi ya Aston Villa. Alikamilisha misimu minne zaidi na Swansea kabla ya kutangaza kustaafu mwaka 2021. Sasa anafanya kazi kama wakala wa michezo katika kampuni ya ICM Stellar Sports, ambako anawasaidia wachezaji chipukizi kukabiliana na shinikizo la soka la kisasa.
Jamie Vardy
Nafasi: Mshambuliaji
Umri: 38
Uso wa hadithi ya miujiza ya Leicester City. Miaka minne tu kabla ya Leicester kunyanyua taji la Ligi Kuu England, Vardy alikuwa akicheza soka mchangani katika klabu ya Fleetwood Town. Alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika michezo 11 mfululizo za Ligi Kuu England na alimaliza msimu huo akiwa na mabao 24 katika mechi 36.
Baadaye alifikisha jumla ya mabao 200 katika mechi 500 alizoichezea klabu hiyo katika mashindano yote, kabla ya kujiunga na klabu ya Serie A, US Cremonese, kwa msimu wa 2025-26 na alifunga mabao dhidi ya timu kama Atalanta BC na Juventus FC katika ligi ya Serie A.
Shinji Okazaki
Nafasi: Mshambuliaji
Umri: 39
Ingawa hakuwa na mabao mengi kama Mahrez na Vardy, Okazaki alijijengea nafasi muhimu katika kikosi kilichoshinda taji baada ya kujiunga kutoka FSV Mainz 05 katika majira ya joto ya mwaka 2015.
Alidumu Leicester hadi 2019 kabla ya kwenda kucheza Hispania katika kikosi cha SD Huesca pamoja na FC Cartagena na kumalizia soka lake Ubelgiji akiwa na Sint-Truiden VV. Ni gwiji wa timu ya taifa ya Japan, akiwa amefunga mabao 50 katika mechi 119 kwa Samurai Blue.
Okazaki alichukua nafasi ya kuwa kocha wa Basara Mainz mwaka 2024. Basara ni klabu ya daraja la sita nchini Ujerumani ambayo yeye mwenyewe alisaidia kuianzisha mwaka 2014 alipokuwa akicheza Mainz.
Leonardo Ulloa
Nafasi: Mshambuliaji
Umri: 39
Ulloa alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Leicester katika msimu wa 2014-15, akifunga mabao 11, lakini katika msimu wa 2015-16 alitumika zaidi kama mchezaji wa akiba. Hata hivyo, alichangia mabao sita muhimu na aliichezea klabu hiyo mara 20 zaidi katika misimu miwili iliyofuata.
Mshambuliaji huyo kutoka Argentina alihamia CF Pachuca mwaka 2018 kabla ya kumalizia soka lake na Rayo Vallecano mwaka 2021. Huenda ana maisha ya kipekee zaidi baada ya soka miongoni mwa kikosi hiki, kwani sasa anafanya kazi katika kampuni ya pipi yenye makao yake Madrid iitwayo Sweet Monkey, sambamba na kufanya kazi ya uwakilishi wa wachezaji.