Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkataba wa Saka una mengi na Mzize anahusika

PAZIA Pict


TUMETOKA mbali. Nitakusimulia kitu. Vita bado ni ngumu na dalili ya kuishinda ni ndogo, lakini tunaweza kushinda tu. Jumanne usiku Vinicius Junior aliondoka mshindi pale Santiago Bernabeu. Kama kweli alibaguliwa na Gianluca Pestrianni bado linabakia fumbo. Siyo fumbo la imani lakini ni fumbo.


Vinicius alifunga tena na kumwondoa Pestrianni na timu yake ya Benfica katika michuano ya Ulaya. Kama alibaguliwa tena katika mechi ya kwanza basi Vinicius ameibuka mshindi. Bao la Ureno na bao la Madrid yamemwondoa Pestrianni katika michuano ya Ulaya. Ni ushindi tosha kwa rangi nyeusi.

PAZ 01

Lakini kulikuwa na ushindi mwingine siku chache kabla ya huu. Bukayo Saka alisaini mkataba mpya na Arsenal. Mkataba ambao umemfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi Arsenal huku akiwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika katika ligi kuu England. Ameondoka na mkataba wa Pauni 300,000 kwa wiki. Pesa ambazo zinamfanya apokee kiasi cha Pauni 20 milioni kwa mwaka.

Mkataba wa Saka umenitafakarisha mambo manne. Jambo la kwanza. Wazungu huwa wanaishi kwa weledi uliopitiliza hasa katika zama hizi. Kwanza kabisa Saka wamemlea wenyewe. Tangu akiwa na umri wa miaka sita alipojiunga na Arsenal wazungu wamemlea hadi leo. Hata hivyo linapokuja suala la mazungumzo ya mkataba jambo hilo huwa linawekwa kando. Wanazungumzia masuala ya masilahi kwa mchezaji na klabu. Kila upande unajitetea.

Saka anakuwa na kambi yake na klabu yake ina kambi yao. Wanakutana mezani na kujadiliana. Habari ya kuleana huwa inawekwa kando. Haijaanzia kwa Saka tu. Kina Steven Gerrard ilikuwa hivyo hivyo. Kina Ryan Giggs ilikuwa hivyo hivyo. Mchezaji analelewa klabuni lakini wakati wa mazungumzo ya mkataba mpya jambo la kulelewa klabuni huwa linawekwa kando.

PAZ 02

Unashangaa kuona mchezaji aliyekulia klabuni kama Saka mazungumzo ya mkataba wake yanakwenda mpaka miezi sita. Kila upande unatetea masilahi yake bila ya kujali sana masuala ya kuleana. Nilianza kushangaa tangu enzi za kina Gerrard, kisha kina Marcus Rashford lakini na leo naendelea kushangaa zama hizi za kina Saka. Hakuna uswahili. Ni suala la kisheria na maelewano ya pande zote mbili mpaka kila mmoja atakaporidhika.

Huku kwetu mchezaji aliyekulia klabuni huwa nadra sana kufanywa mchezaji anayelipwa zaidi klabuni. Utasikia tu wazee wa timu wakisema "Huyu mtoto tumemlea wenyewe hapa hapa klabuni halafu leo anatusumbua". Na kama baba yako ni shabiki wa hiyo timu viongozi wanaweza kwenda kupitia kwa baba yako ili usaini mkataba mpya. Imewahi kutokea mara kadhaa. Na inaweza kuendelea kutokea.

Mashabiki na viongozi wanataka kuona mchezaji anakuwa shabiki. Wanataka kuona mchezaji anakuwa mwanachama. Wanasahau anachofanya ni kazi yake na katika kazi ambazo zina maisha mafupi mojawapo ni soka. Ukifikisha umri wa miaka 31 tu unaanza kuitwa mzee. Tangu lini kijana wa umri wa miaka 31 akaitwa Mzee? Katika mpira huwa tunakuita mzee.

PAZ 03

Siku hizi kidogo viongozi wetu wameanza kuzinduka usingizini. Naona Yanga wamefanya vyema kwa Clement Mzize. Sawa wamemlea kutoka katika timu ya vijana lakini wamembakisha kwa pesa nyingi na wanamlipa mshahara mkubwa hata kama sio ule anaolipwa Pacome Zouzoua. Azam pia wamefanya vizuri kwa Pascal Msindo. Wamemlipa pesa nzuri katika mkataba wake mpya licha ya kumlea katika timu ya vijana.

Na sasa Saka analipwa mshahara mkubwa mbele ya wazungu akina Martin Odegaard, Declan Rice,  Kai Havert na wengineo. Tumetoka mbali. Inadaiwa wazungu wa zamani wasingemlipa John Barnes pesa hizi kwa sababu ya rangi. Asingepewa umuhimu mkubwa mbele ya wazungu. Wakati ule ndio kwanza kina Barnes walikuwa wanarushiwa ndizi uwanjani wakifananishwa na nyani.

Mkataba wa Saka pia unaweza kunusuru pesa zetu. Pesa za mtu mweusi. Kaka zetu weusi walio na umaarufu kule Ulaya na Marekani huwa wapo bize zaidi na Warembo wazungu. Haijulikani kwa nini. Wengine wanadai warembo weusi huwa ni wakorofi zaidi kuliko kina dada wa kizungu. Hata hivyo, mwisho wa siku Warembo wa kizungu ndio huwa wanakuja kuwakamua pesa nyingi hawa kaka zetu.

PAZ 04

Kina Tiger Woods, Emmanuel Eboue,  Michael Jordan na wengineo wengi wameishia kukamuliwa pesa nyingi na wazungu. Na mpaka sasa huwa hawakomi. Kina Kylian Mbappe,  Vinicius Junior na mastaa kibao weusi wanatoka na  warembo wa kizungu. Saka yeye mpaka sasa yupo katika mikono ya mrembo mweusi, Tolami Benson ambaye ana asili ya kwao Nigeria.

Walau pesa zake zinaweza kuwa salama hadi sasa. Akinichanganya kidogo kupeleka pesa kwa wazungu anaweza kujikuta na kesi ngumu za kubaka kama ambazo zinamkabili kaka yake, Thomas Partey. Huu ni ukweli mchungu ambao umewakabili wanasoka wengi weusi Ulaya. Sijui kama huwa ni watundu au vinginevyo lakini kesi hizi ni chache kwa wanasoka wazungu.

Ushindi mwingine katika mkataba wa Saka ni ukweli Ulaya imeendelea kuwabakisha wachezaji wake mahiri ambao wamekuwa wakitamaniwa na soka la Saudi Arabia. Nina mashaka mradi wa Saudi Arabia umeanza kupoteza makali kwa sababu kuna wachezaji kibao walikimbilia noti za waarabu lakini wameanza kurudi Ulaya kwa kasi. Kina John Duran, Ngolo Kante na wengineo.

PAZ 05

Pia naona kuna wanasoka wengi mahiri wa Ulaya wamegoma kwenda Saudi Arabia. Ndio hawa kina Saka ambao wameendelea kusaini mikataba mipya katika klabu zao. Ndio kama vile Vinicius Junior na Mbappe ambao waliahidiwa mikataba kufuru kucheza Saudi Arabia lakini walisaini mikataba ya Ulaya. Usidhani Waarabu walikuwa hawamwangalii Saka. Walikuwa wanamtazama na kummezea mate kama wanavyofanya kwa Bruno Fernandes kila kukicha.

Ushindi mwingine upo kwa Arsenal wenyewe. Labda kwa sababu sasa hivi wanashindana lakini mitaa ya hapo kati wameonewa vya kutosha na Manchester City pamoja na timu za Hispania. Hapo katikati waliwapoteza mastaa wao akina Thierry Henry, Emmanuel Adebayor, Samir Nasri, Gael Clichy, Bacary Sagna, Alexandre Hleb waliotimkia City na timu za Hispania. Hata Van Persie pia alitimkia Manchester United.

Kumbakisha Saka ni kuendelea kuonyesha hawataki tena kuwa wauzaji. Lakini inaonyesha pia wachezaji wana imani na timu yao. Kwamba inapambana kuwania mataji tofauti na zama zile za Arsene Wenger wakati alipoishiwa mbinu. Wakati mwingine pesa sio kila kitu. Na kuna wachezaji wakifikia hadhi fulani wanaweza kupata vyote. Wanaweza kupata fedha na mataji kama akina Nasri walivyofanya walipoondoka Arsenal.