Mastaa Chelsea wamtibua Maresca

Muktasari:
- Wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao hawakuwa kwenye majukumu ya mechi za kimataifa walitakiwa kuwa na mapumziko Alhamisi.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca amefuta mapumziko ya wachezaji wake baada ya kuonyesha kiwango kibovu kwenye mechi ya kimazoezi dhidi ya kikosi cha wachezaji wa U21 wa klabu hiyo.
Wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao hawakuwa kwenye majukumu ya mechi za kimataifa walitakiwa kuwa na mapumziko Alhamisi.
Lakini, kocha Maresca alifuta mapumziko hayo baada ya kuona kile ambacho wachezaji hao walifanya kwenye mechi ya kimazoezi Jumatano huko uwanjani Cobham na walishindwa kufurukuta mbele ya wachezaji wa kikosi cha U21.
Kocha huyo Mtaliano aliwaambia wachezaji wake hataki masihara tena kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu na hivyo kuwa mkali, ikiwamo kufuta mapumziko ili kuhakikisha timu inakuwa kwenye kiwango bora ili kukusanya pointi zitakazowafanya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, huku kikifukuzia pia taji la Europa Conference League msimu huu.
Wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa kocha Maresca alikuwa akifanya mazoezi na wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho, wakati wakati wengine akiwamo Reece James na Enzo Fernandez walikuwa kwenye majukumu ya timu za taifa. Mastaa ambao hawakuwa kwenye timu za taifa ni Jadon Sancho, Christopher Nkunku, Romeo Lavia, Benoit Badiashile, Tosin Adarabioyo na Malo Gusto.
Hata hivyo, haifahamiki kama mastaa hao walicheza kwenye mechi hiyo ya kimazoezi chini ya timu ya U21. Katika mechi hiyo, ambapo kikosi cha U21, ambacho kilichanganyika na wachezaji wa U16, kiliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya timu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza, jambo ambalo lilimkasirisha kocha Maresca.
Mastaa wa kikosi cha kwanza wa Chelsea ambao hawakucheza mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi ni Cole Palmer,
Nicolas Jackson, Noni Madueke, Marc Guiu na Omari Kellyman huku mchezaji Mykhailo Mudryk anatumikia adhabu.
MASTAA WA KIKOSI CHA KWANZA WA CHELSEA WALIOKUWA KWENYE TIMU ZAO ZA KIMATAIFA
Enzo Fernandez
Filip Jorgensen
Moises Caicedo
Levi Colwill
Reece James
Pedro Neto
Marc Cucurella
Josh Acheampong
Tyrique George
Mathis Amougou